BARUA YA WAZI KWA KATIBU MKUU WA CHAMA CHA MAPINDUZI (CCM) KUHUSIANA NA VITENDO VYA UTOVU WA NIDHAMU NA UKIUKWAJI WA MAADILI VINAVYOFANYWA NA ALIYEKUWA MBUNGE WA JIMBO LA NGARA BW. NDAISABA GEORGE RUHORO.
Mheshimiwa Balozi Daktari Emmanuel Nchimbi,
Katibu Mkuu wa CCM. _Kidumu chama cha Mapinduzi!_
YAH: TAARIFA KUHUSU UKIUKWAJI WA MAELEKEZO YA CHAMA, UNAOFANYWA NA BWANA NDAISABA GEORGE RUHORO.
Kwa heshima, taadhima na unyenyekevu mkubwa, mimi MwanaCCM mtiifu na muumini wa misingi, maadili na kanuni za chama chetu, naandika barua hii ya wazi kukufikishia taarifa ya vitendo vya utovu wa nidhamu na kukosa utii kwa maagizo halali ya chama, vinavyofanywa na aliyekuwa Mbunge wa jimbo letu la Ngara Bwana Ndaisaba George Ruhoro.
Utakumbuka mnamo tarehe 23.06.2025, kupitia taarifa yako kwa umma, ulitoa maagizo mahususi ambayo pamoja na mambo mengine ulitoa maelekezo ya kuzuia na kudhibiti mwenendo usiofaa wa kwa Wagombea wa ngazi zote kwa kuzuia mikutano, semina au makongamano yanayowahusisha wajumbe wa vikao vya maamuzi mpaka baada ya mchakato wa kura za maoni.
Kimsingi maelekezo hayo yalitolewa kwa hekima kubwa kwa nia ya kulinda heshima ya Chama chetu, umoja na mshikamano wetu, na nidhamu miongoni mwa WanaCCM kuelekea kipindi hiki cha kupata wagombea.
Hata hivyo, katika hali isiyokuwa ya kawaida, licha ya maelekezo hayo wazi na ya moja kwa moja, WanaCCM tunashangaa kuona kuwa Bwana Ndaisaba George Ruhoro, ameendeleza ziara, mikutano na shughuli zinazohusisha wajumbe wa vikao vya maamuzi, kinyume na maelekezo yako rasmi. Kuwa na kiburi na jeuri ya kuendeleza shughuli zilizozuiliwa na Chama chetu kwa uwazi si tu ni cha kuidhalilisha ofisi yako, bali kinadharau mamlaka yako, hadhi na madaraka yako hali inayosababisha sintofahamu na mgawanyiko usio wa lazima miongoni mwa Wanachama.
Baadhi ya ziara na mikutano iliyobainika kwa ushahidi ni kama ifuatavyo:-
(i) Tarehe 29/06/2025 alikuwa
Kata ya Mugoma, alikukutana na wajumbe nyumbani kwa Diwani mstaafu na kuwapa kiasi cha Tsh. 20,000/=
(ii) Tarehe 30.06.2025 alikutana na Wajumbe Kata ya Mabawe.
(iii) Tarehe 01.07.2025 alikutana na wajumbe kata ya Murusagamba.
(iv) Tarehe 03.07. 2025 alikutana na wajumbe Kata ya Mbuba.
(v) Tarehe 03.07.2025 alikutana na wajumbe Kata ya Kabanga na kila mjumbe alipewa Tsh. 30,000/=
(vi) Tarehe 03.07.2025 akikutana na wajumbe Kata ya Ngara na Kata na Kibimba nyumbani kwake na kila mtu alipewa Tsh.30,000/=
(vi) Tarehe 03.07.2025 alikutana na wajumbe Kata Kasulo nao walipewa Tsh. 30,000/= na usiku wa siku hiyo katika eneo la Kapfua Hotel Benako-Kasulo alikutana na Madiwani wasitaafu 19 kati ya 22 (Ambao hawakuhudhuria ni Diwani wa Kabanga, Nyamiaga na Mbuba) kupongezana kwa kuratibu zoezi la kumkutanisha na wajumbe na kila mmoja alipewa mkono wa akhsante Tsh. 1,000,000/=
Kinachoshangaza zaidi ni kwamba anatumia miradi ya maendeleo ya kielelezo cha kazi kubwa na nzuri sana iliyofanywa na Mheshimiwa Rais Daktari Samia Suluhu Hassan kwa Chama na Serikali katika jimbo letu kwamba katika kipindi chake kaleta fedha nyingi kutekeleza miradi hiyo ya maendeleo mfano kuweka taa za barabarani, ujenzi wa Hospitali ya Wilaya na Chuo cha Veta, pikipiki wa Viongozi wa Chama ngazi ya kata na Baisikeli za mabalozi.
Kwa mkutadha huo, ili kulinda hadhi na heshima ya Ofisi yako na Chama chetu kwa ujumla, kwa unyenyekevu mkubwa, ninaomba kupitia barua hii utumie mamlaka yako kuchukua hatua za dharula za makusudi kujiridhisha na mienendo hiyo mibovu ili kuhakikisha kwamba vitendo vya namna hiyo vinadhibitiwa na kutokomezwa haraka iwezekanavyo ili kudumisha heshima ya chama, nidhamu ya kiuongozi, na kutekeleza misingi ya maamuzi ya pamoja yanayolinda umoja wetu.
Nina imani kuwa uongozi wako thabiti na madhubuti utaendelea kulinda misingi ya haki, nidhamu na utiifu katika chama chetu pendwa.
Kwa heshima na unyenyekevu mkubwa, ninaomba kuwasilisha.
MwanaCCM Mtiifu.