Na Steven Samwel – Zanzibar
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein, amesema kuwa azma ya Chuo Cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere ya kuandaa Kongamano la Kumbukumbu ya kumuenzi Marehemu Sheikh Abeid Amani Karume ni ya kupongezwa kutokana na kutambua juhudi za kiongozi huyo aliyewapigania wanyonge.
Dk. Shein amesema hayo leo alipokutana na Bodi ya Chuo Cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere chini ya uongozi wa Mwenyekiti wa Bodi hiyo Profesa Mark Mwandosya, Ikulu mjini Zanzibar.
Katika maelezo yake, Dk. Shein amesema kuwa Marehemu Mzee Abeid Amani Karume ana heshima ya pekee kwa Zanzibar na kwa Tanzania nzima kwa jumla, hivyo uamuzi wa Chuo hicho kuandaa kongamano hilo ni hatua moja wapo ya kumuenzi na kumthamini muasisi huyo.
Ameongeza kuwa Mzee Karume alikuwa na Dira na ndio maana aliweza kufanya mambo mengi makubwa ambayo yataendelea kukumbukwa kutokana na umuhimu wake.
Ameeleza kuwa Mzee Karume ndiye aliyeweza kusimamia Mapinduzi matukufu ya Januari 12, mwaka 1964 ambayo yamewakomboa Wazanzibari na kuwatoa katika unyonge na hatimaye kuondosha ubaguzi wa aina zote.
Aidha, Rais Dk. Shein amefafanua kuwa kufanyika kwa Mapinduzi ni jitihada za Mzee Karume na viongozi wenzake ambapo jitihada hizo zinafaa kuenziwa pamoja na kutunzwa na kudumishwa ili na vizazi vijavyo viweze kuzifahamu.
Dk. Shein amesema kuwa kuna kila sababu ya kutoa pongezi kwa chuo hicho kwa kwa hatua hiyo ya kutambua mchango mkubwa wa Marehemu Sheikh Abeid Karume ambaye pia, ni muasisi wa Muungano wa Tanganyika na Zanzibar na hatimaye kuundwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Ameongeza kuwa Marehemu Mzee Karume na Marehemu Mwalimu Julius Kambarage Nyerere waliziunganisha Tanganyika na Zanzibar Aprili 26 mwaka 1964 na hadi hivi leo Muungano huo umeweza kujijengea sifa kubwa ndani na nje ya Bara la Afrika na kuwa wenye manufaa makubwa kwa Watanzania wote.
Sambamba na hayo, Rais Dk. Shein ametumia fursa hiyo kuupongeza uongozi wa Chuo hicho kwa kuimarisha Kampasi yake ya Zanzibar ambayo hivi sasa imekuwa ikisomesha kada mbali mbali sambamba na kuongezeka kwa wanafunzi na kusisitiza kuwa hiyo yote inatokana na uongozi thabiti uliopo katika chuo hicho.
Nae Mwenyekiti wa Bodi ya Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere, Profesa Mark Mwandosiya ametoa pongezi kwa Dk. Shein kwa kuendelea kuiongoza vyema Zanzibar ambayo imeweza kupata maendeleo makubwa pamoja na kuimarika kwa mshikamano uliopo kati ya Wazanzibari wote huku wakiwa na amani na utulivu mkubwa.
Profesa Mwandosya amesema kuwa Kongamano linalotarajiwa kufanyika Aprili 5, mwaka huu katika ukumbi wa Kampasi ya Chuo hicho Bububu nje kidogo ya mji wa Zanzibar, ni miongoni mwa kumbukumbu za Maremu Mzee Abeid Amani Karume.
Nae Mkuu wa Chuo hicho Profesa Shadrack Mwakalila amemueleza Rais Dk. Shein mafanikio yaliyopatikana na chuo hicho kwa upande wa Zanzibar na Tanzania Bara na kumueleza jinsi Kampasi ya Zanzibar ilivyopiga hatua kwa kuwa na wanafunzi zaidi ya 1000 kutoka 21 pale Dk. Shein alipolifungua jengo jipya la Kampasi ya chuo hicho mwaka 2013.
Amesema kuwa chuo hicho kina historia kubwa na wasingependa kuipoteza ikiwa ni pamoja na kuwaenzi waasisi wa Taifa hili ambapo kwa upande wa Zanzibar, Chuo kimeamua kwa mara ya kwanza kuanzisha Kongamano la kumuenzi Mzee Karume ambalo litakuwa ni endelevu.
Pia, ungozi huo wa Bodi umezungumzia haja ya kuwa na kituo cha kumbukumbu kwa lengo la kumtunza na kumuenzi Mzee Karume huku wakisisitiza kuwepo kwa vituo vya kumbukumbu kwa Maraisi wote wastaafu wa Zanzibar ili jamii ipate kusoma na kutambua mafanikio yao na changamoto walizokumbana nazo.
Pamoja na hayo, viongozi hao wameahidi kuendelea kuwatunza na kuwaenzi viongozi wote wa Taifa hili wakiwemo waasisi wake kwa lengo la kuendelea kutekeleza Sheria ya Kuwaenzi viongozi wa Taifa hapa nchini.
Recent Comments