Recent Comments

Mzee Robert Mugabe: Kiongozi Aliyepania Kuwakomesha Wazungu Wakakoma Watu Wake!

By Denis Mpagaze Sep 13, 2019

Ukisikia watu wanasema tuko nyuma yako ‘be careful’ maana ukigeuka unaweza usiwakute. Hii nimeiona ‘live’ kwa Robert Mugabe pale alipojitoa muhanga kuwakwida mabeberu kwa maslahi ya Afrika, wakaumia wananchi wake kwa vikwazo vya uchumi na diplomasia, viongozi wa Afrika wakamtelekeza, leo hii amekufa viongozi wanashindana kumsifia Mugabe kwa mbwembwe na mikogo kwa sababu marehemu hatukanwi. Haya ndiyo maajabu makuu ya viongozi wa Afrika!

Tatizo la Afrika ukiwa kiongozi mzuri ni sawa na kuchagua kifo, wasipokuua basi watakukwamisha kama walivyomkwamisha Nyerere na ujamaa wake, Mandela na msahama wake, Kaunda na suti zake na Mugabe na misimamo yake.

Tatizo la misimamo husihia kuwaumiza maskini na mlengwa akibaki kutafuna miguu ya kuku. Mugabe na mke wake Grace na watoto wao Bonna,Chatunga na Robert Jr na washikaji zake wamekula bata mpaka Wazungu wakawazuia Grace kwenda wao kufanya shopping ati anafuja mali za taifa. Hivi mnaujua Grace au mnasikia? Alitengeneza keki yenye thamani ya bilioni moja na nusu za Kitanzania kwa ajili ya birthday ya mume wake na wakati mwenzangu girlfriend wako akikuomba buku teni ya keki unasusa wiki nzima na wakati mwanaume hasusi.

Huyu Mugabe tunayemzungumzia leo ni mtoto wa fundi seremala aliyeiitikisa dunia ikatikisika nchi yake. Umaarufu wake uligeuka ajenda za vyombo vya habari Duniani na kitanzi kwa watu wake. Tabia yake ya kuwachana wazungu live bila chenga ilimgharimu kifungo cha miaka 12 jela. Ni baada ya kugoma kufuta kauli zake za kichochezi kwa sababu maneno yakiishatoka hayarudishiki mdomoni. Alisota jela kuanzia 1963 mpaka 1975. Halafu Mugabe akikuchana lazima usahau njia. Alimchana Rais Donald Trump wa Marekani kwamba ni mjukuu wa Hitler anayetaka kuleta vita ya tatu ya Dunia. Barrack Obama naye akaambiwa kama anataka ushoga basi akubali kuolewa na Mugabe.Kwa majibu ya shomba mshikaji alijaaliwa.

Mugabe akiwa jela mtoto wake Nhamodzenyika alifariki dunia kwa ugonjwa wa malaria. Hakuruhusiwa kwenda kumzika. Halafu ndo alikuwa mtoto wake wa pekee kwa mke wake Francisca. Nhamodzenyika yaani Nchi Yenye Mateso, alizaliwa 1963 na kufa 1966. Huyo mama hakuzaa tena mpaka alivyokufa mwaka 1992. Nasikia akiwa mahututi kitandani Mugabe alianzisha mahusiano na Grace mke wa Rubani Stanley Goreraza mpaka Grace akazaa na Mugabe watoto wawili bila rubani kujua. Mama akaomba talaka na 1996 akafunga ndoa na Mugabe, wakapata mtoto wa tatu Mugabe akiwa na umri wa miaka 73 na Grace 32, Mugabe akamuita mtoto wake wa uzeeni Chitunga Mugabe, rubani naye hakuachwa hivihivi, alipandishwa cheo na kuhamishiwa China na India.Hizo ndo raha na karaha za wakubwa, omba zisikukute.

Anyway hiyo siyo hoja ya msingi kivilee kwa sababu mafiga mawili hayaivishi ugali. Hoja ni kwamba Mugabe alijaaliwa akili, hekima na majibu ya kuudhi sana. Shuleni alikuwa mpole wa mwili lakini mwingi wa akili mpaka mapadri kumsomesha chuo kikuu. Alisoma pale Fort Hare University, akaajiriwa kufundisha kwa mshahara wa pound 2 kwa mwezi, familia ya baba yake ikapata pa kuponea. Kwao walizaliwa sita, kaka zake wawili walikufa, akabaki yeye, wadogo watatu kwa mama na wengine watatu kwa baba. Baba yake aliwahi kwenda mjini kutafuta pesa akarudi na watoto wengine watatu kwa sababu kitanda hakizai haramu, baba akafa Mugabe akaibeba familia kwa mshahara wa ualimu. Hii ndo Afrika. Ukoo mzima kuhamika kwako kwa mshahara wa ualimu ni suala la kawaida sana kwa sababu ukarimu ni jadi yetu.

Mwaka 1958 Mugabe alikwenda zake nchini Ghana kufundisha. Huko alikutana na Sarah Francesca yakazaliwa mapenzi ya urafiki, uchumba ndoa ndoa wakati huo wote ni walimu. Siku hizi mwalimu anaoa mwanafunzi wake kwa sababu hana adabu.

Sarah naye alikuwa mwanaharakati kama mume wake maana Mungu hukupa wa kufanana naye. Ukiwa janja janja Mungu anakupa janja janja, ukiwa mwizi anakupa mwizi ili uzae wezi wa kutosha. Hata Sarah aliwahi kutupwa jela kwa kosa la kuongoza maandamano ya wanawake kupinga utawala wa kikoloni.

Kwa neema ya Mungu wafungwa Mugabe na Sarah wakaingia Ikulu kama Rais wa Pili wa Zimbabwe na First Lady, wahenga wakasema hakika baada ya dhiki faraja.

Rais wa kwanza wa Zimbabwe alikuwa Canaan Banana, Mtumishi wa Mungu wa Kanisa la Methodist aliyetupwa jela kwa kosa la ulawiti. Ilikuwa 1997. Mtumishi wa Mungu alizingua.

Tangu Mugabe ameingia kwenye siasa mpaka anaacha mwili amewasumbua sana wazungu. Bifu lilipamba moto kuanzia mwaka 2000 alipotaifisha mashamba yao.

Issue yenyewe ilikuwa hivi. Serikali ya mkoloni ilipochoshwa na vurugu za kina Mugabe kutoka misituni Malkia aliitisha kikao Lancaster Uingereza kujadili namna watakavyoongoza nchi bila vurugu. Moja ya makubaliano ilikuwa ugawanyaji wa ardhi kati ya wazawa na wazungu kwa makubaliano yaliyoitwa Lancaster House Agreement. Walitoa grace period ya miaka 20 ili USA na UK kuwalipa fidia wakulima wa kizungu lakini Mugabe akagoma, alijua ni zengwe, alitaka wazungu waondoke fasta. Mwl. Nyerere, akamshauri akubali tu maana mambo mazuri hayataki papara, jamaa akakubali, akasaini makubaliano, wakarudi Zimbabwe, ukapigwa uchaguzi wa vyama vingi,Mugabe akachukua nchi kama waziri mkuu na Banana Rais asiye na meno.

Sasa kila akikumbushia yale makubaliano ya Lanacaster wazungu wanapiga chenga.Ndipo akataifisha mashamba kwa nguvu, bifu likaanza, akawekewa vikwazo vya kiuchumi na diplomasia akazuiliwa kusafir kwenda kwaoi, media zote za nje BBC, CNN, Fox news full kumshambulia, zikamuita majina yote machafu ili wamuue. Uchumi wa Zimbabwe ukaanguka kifo cha mende, watalii wakaacha kuja Zimbabwe, wawekezaji kwenye madini wakasepa, pesa yao ikadorola mpaka basi, wakachapisha noti ya TRILLIONI 100 na TRILLIONI 25,000 lakini wapi.

Sasa badala ya nchi za Afrika kuungana na shujaa wa Afrika kwa kuvikataa vikwazo na kufanya naye biashara, zikamchunia. Viongozi wengine wakaungana na mabeberu kumlaani Mugabe, Laila Odinga wa Kenya akiwa PM akapanga kumvamia, watu wake wakasema bora ukoloni kuliko Mugabe. Kwamba enzi za Smith Zimbabwe iliexport chakula lakini leo ni ombaomba.

Ukiona mtu mweusi kama mkaa anamtetea mtu mweupe ujue mwisho umekaribia.Hata kule Zanzibar tayari wameanza kumsafisha mwarabu kwamba hakufanya biashara ya utumwa, isipokuwa yeye ndo alikomesha biashara hiyo. Hizi fikra za ‘niguse ninuke’ ni hatari kwa Afrika Unite.

Mugabe alivyohojiwa kuhusu afya yake alijibu,” Nimekufa mara nyingi, hapo ndipo nimemshinda Yesu Kristo. Yesu alikufa mara moja na akafufuka mara moja,”

Kuhusu imani yake alisema yeye si mkristo kivileee! Hakuwa mnafiki kama wewe hapo unayesengenya kuanzia jumatatu mpaka Ijumaa na kuwahi kanisani Jumapili full kupretend utadhani msaidizi wa Yesu.

Kuhusu Mandela Mugabe alisema kumuita Mandela mkombozi wa Afrika ni kupotosha historia. Mandela alipigania ukombozi wa nchi yake tu, lakini Nyerere alipigania ukombozi wa nchi nyingi za Afrika na bara zima.

Prince Katega wa 2 anasema Mugabe alikuwa na mahusiano mazuri na asili ya kiafrika ndo maana wazungu walishindwa kumuua kama walivywaua Thomas Sankara, Patrice Lumumba,Kwake Nkrumah, Muammar Gadaffi na wengine wengi. Hapo hata mie nakubali maana kuwapinga IMF na WB, na kugoma kulipa madeni ya nje lazima Mungu wake yuko hai. Waliishia kumnyang’anya digrii na tuzo zote walizomuhonga wakidhani ataingia kingi lakini mwanaume alikomaa.

Mugabe ameondoka lakini matatizo ya Zimbabwe ni yale yale na wajinga hawaoni.Afrika yote ni moja na matatizo ni yaleyale. Siku zote huwa nasema tatizo kubwa la Afrika ni Utumwa wa Fikra. Hatujielewi. Tulinyang’anywa akili tukaachiwa miili. Tumevurugwa. Ukitaka kuamini nachokwambia fuatilia chattings za jamaa zako. Kama nikijana utamkuta yuko busy akipost ujinga na kufurahia likes na kama ni mzee ni full kulaumu kwamba vijana wa siku hizi hawajui kitu. muulize yeye na uzee wake anayejua vitu ameifanyia nini nchi hii zaidi ya kuzungumza kingereza kigumu hata kama hakimsaidii maana anajua elimu ni kingereza.Ukimpa makala fikirishi yeye atasoma kutafuta kosa ili atukane badala ya kusoma ili aelewe.

Tupandikize fikra za kujitambua. Tuanze na watoto wadogo maana hao ndo taifa la kesho. China leo inatetemesha dunia kwa sababu Mao Tse Tung alivyoshika Uchina alianza na watoto na kusema kwamba hawa ni mali ya taifa na watoto walifundishwa kuwatemea mate wazazi wao mapebari na adui wa Ujamaa. Fikra za kikomunisti zikamea kwenye akili za watoto. Adolf Hitler alivyokama nchi alichoma vitabu vyote vya shule na kuanza kupandikiza sera za kinazi kwenye akili za watoto. Tuwajenge vijana wetu, hawajui mengi kwa sababu hawasomi, ndo maana akisimama kujenga hoja utadhani kuna mtu kafungia akili zake stooni.

Siku za kufa kwake Mugabe zilipokaribia chama chake kilipasuka, upande mmoja ukimuunga mkono mke wake Grace upande mwingine Emmerson Mnangagwa. Huyu Mnangagwa ni mshikaji wake wa muda mrefu toka msituni,wamehaso pamoja, lakini Grace ndo usingizi wa mzee.

Mugabe akamtimua Makamu wake Mnangagwa kwamba alitaka kumpindua kwa sababu wanawake ni jeshi kubwa. Jeshi, likaongoza waandamanaji, Mugabe akashauriwa kujiudhuru, akakaza kamba kama kawaida yake, Bunge likatishia kumng’oa, akaona bora nikubali yaishe, kwa shingo upande, akajiuzulu Urais Novemba 21, 2017, Mnangagwa akachukua nchi wazimbabwe wanasubiri neema ishuke kutoka kwenye kifua cha Mnangagwq.

Mugabe amefariki Septemba 6, 2019 akiwa na umri wa miaka 95, mjini Singapore kama ilivyo kawaida ya viongozi wengi wa Afrika kufia nje. Jeneza lake nasikia limewekewa mpaka air condition kwa sababu kilichoumbwa na Mungu hakifi. Prince Katega anasema Mugabe hajafa, Mugabe ameacha mwili tu, anaendelea na kazi kama muzimu hai.

Afrika tutaendelea kuhenya mpaka pale tutakapotimiza lile Agano la Kwame Nkrumah la, “We must unite now or perish”.

Pumzika kwa Aman Comrade Robert Gabriel Matibiri Mugabe!