Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa Joyce Ndalichako leo Juni 17, 2020 ametangaza tarehe za kuanza kwa mitihani ya Taifa ya Darasa la Saba, Kidato cha Nne na Upimaji wa kitaifa wa Darasa la Nne na Kidato cha Pili.
Akizungumza na Waandishi wa habari Jijini Dodoma, Prof. Ndalichako amesema Darasa la Saba watafanya Mtihani kuanzia tarehe 7 – 8 Oktoba, 2020 wakati Kidato cha Pili wataanza mitihani Novemba 9 – 20, 2020. Darasa la Nne watafanya Novemba 25 – 26, 2020 wakati Kidato cha Nne watafanya kuanzia Novemba 23 hadi Disemba 11, 2020.
Profesa Ndalichako amezungumzia mihula mipya ya shule ambapo amesema shule za msingi na sekondari watamaliza muhula wa kwanza wa masomo Agosti 28, 2020 na kuanza muhula wa pili utakaoishia Disemba 18, 2020. Amesema kuwa ili kukamilisha muhtasari wa masomo, shule zitalazimika kuongeza saa 2 za masomo kila siku ili kufidia muda uliopotea huku akisisitiza kuwa maelekezo ya kuongeza muda hayatahusu madarasa ya awali.
Aidha, Profesa Ndalichako ametoa ufafanuzi kuhusu mihula kwa wanafunzi wa Kidato cha Tano ambapo amesema wanafunzi hao wataanza masomo Juni 29, 2020 kama ilivyoagizwa na kukamilisha muhtasari wa masomo yao na kufanya mitihani yao ya kumaliza Kidato cha Tano ifikapo Julai 24, 2020. Wanafunzi hawa wataanza rasmi masomo ya Kidato cha Sita Julai 27, 2020.
Waziri Ndalichako ameagiza Uongozi wa shule zote kuhakikisha wanafunzi, walimu na wafanyakazi wengine wote wanazingatia maelekezo ya kujikinga na maambukizi ya virusi vya Corona kama yalivyotolewa katika Mwongozo wa Wizara ya Afya ikiwemo kuhakikisha kuwa shule zote zinanunua vifaa vya kutosha kwa ajili ya kunawa mikono kwa maji tiririka na sabuni.
Recent Comments