Zaidi ya Sh. milioni 800 zimetumika kukarabati Chuo cha Ualimu Bustani kilichopo Halmashauri ya Mji Kondoa mkoani Dodoma.
Akizungumza mara baada ya kukagua miradi ya maendeleo chuoni hapo, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako amesema Serikali imetoa kipaumbele kwenye sekta ya elimu kwa kurabati, kujenga miundombinu ya taasisi za elimu ikiwa ni pamoja na kununua vifaa vya kufundishia na kujifunzia ili kuboresha dhana nzima ya ufundishaji na ujifunzaji.
Kuhusu ukarabati na ujenzi unaoendelea kwenye vyuo vya ualimu Waziri Ndalichako amasema serikali inaboresha miundombinu ya vyuo hivyo kwa awamu ambapo awamu ya kwanza imehusisha vyuo 10, awamu ya pili vyuo 8 na awamu ya tatu vyuo 9 na chuo cha Bustani kikiwemo na kufanya idadi kufikia 27 kati ya Vyuo 35 vya Elimu nchini. “Huu ni uwekezaji mkubwa ni vizuri miundombinu hii ikatunzwa kwa sababu serikali inatumia fedha nyingi kurudisha hadhi ya vyuo hivi. Fedha iliyoletwa katika Chuo cha Ualimu Bustani mwezi Februari ni sh milioni 874 kwa ajili ya kukarabati na kuongeza majengo mapya ambayo ni bweni nyumba za walimu ikiwemo ya mkuu wa Chuo na kuongeza baadhi ya majengo kama Hosteli za wanafunzi wa kike,”alisema Waziri Ndalichako
Amewataka wanafunzi kuwa wazalendo, kuipenda nchi yao, kujitambua na huku wakiilinda tunu za Taifa zilizoachwa na waasisi wa nchi hii. “Vijana uzalendo ni pamoja na kueleza mazuri yanayofanywa na serikali yenu, hata haya yanayofanyika hapa chuo cha Bustani, myaseme kwani hali ya miundombinu kabla ya ukarabati na baada ni tofauti sana ni jukumu lenu kueleza mafanikio ya serikali ndani ya Taasisi zenu na hata nje,” alisisitiza Waziri Ndalichako
Waziri Ndalichako ametumia fursa hiyo kuwatakia kila lakheri walimu tarajali wa mwaka wa pili wanaokwenda kuanza mitihani ya elimu ya ualimu Juni 29, 2020.
Recent Comments