MATUMIZI ya Teknolojia za Nishati Jadidifu katika shughuli za kilimo, yametajwa kuwa msingi wa uzalishaji wenye tija katika sekta hiyo, kwamba inasaidia kuleta uhimili wa mazingira na kudhibiti hatari kubwa ya kutokea kwa athari za mabadiliko ya tabianchi.
Imeelezwa kuwa ni muhimu shughuli za kilimo zifanywe kwa urafiki wa mazingira badala ya kuwa chanzo cha uharibifu kwani matokeo yake huathiri zaidi uzalishaji katika sekta hiyo.
Ikumbukwe kuwa kauli hiyo inafuatia muendelezo wa hatua mbalimbali za kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi ambayo yanatajwa kuathiri sekta nyingi nchini na hata uhai wa viumbe.
Hayo yalibainishwa na Mkurugenzi wa Ushirika wa Wajasiriamali Waliosoma katika Chuo Kikuu cha Kilimo mkoani Morogoro (SUGECO), Revocatus Kimario, walipotembelewa na wanachama wa Asasi ya Kiraia ya FORUMCC mkoani humo, ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa Mradi wake wa kuhamasisha matumizi ya nishati jadidifu unaofadhiliwa na Shirika la Hivos.
Alisema kuna haja ya jamii kutambua kuwa shughuli za kilimo zinapaswa kuwa rafiki wa mazingira hivyo ni muhimu kwa wakulima kuhamasika kutumia teknolojia za nishati jadidifu katika shughuli hizo hali ambayo italeta tija katika uzalishaji na kupunguza hatari ya kutokea kwa athari za mabadiliko ya tabianchi.
âShughuli za kilimo kwa sehemu kuwa zinachangia uharibifu wa mazingira kuanzia maandalizi ya shamba, matumizi ya teknolojia za kufanikisha kilimo, hii inatokana na kwamba pengine jamii haitambui kuwa kuna mbadala wa teknolojia sasa kuna haja ya kuielimisha ili ihamasike na kuanza kutumiaâ.
Kimario alisema katika shughuli zao za kilimo biashara wamekuwa wakitumia teknolojia mbalimbali za nishati jadidifu ikiwemo nishati ya umeme wa jua kwa ajili ya umwagiliaji, kulima kwa matuta ambapo hutumia ardhi ndogo huku uzalishaji ukiwa mkubwa zaidi.
Alisema shughuli za kilimo zinahitaji zaidi mazingira yenye uhimili, yasiyohelemewa na hewa ya ukaa ili kupata mavuno makubwa, hivyo ni ajabu kwa mkulima kuharibu mazingira wakati wa uzalishaji kwani hiyo itaathiri shughuli hiyo na hatimaye kushindwa kufanyika kabisa.
Aliongeza kuwa SUGECO imekuwa ikifanya uhamasishaji na uelimishaji jamii hususan vijana kujikita katika kilimo biashara badala ya mazoea ili wanufaike na sekta hiyo, huku utunzaji wa mazingira ikiwa ndio nguzo ya shughuli hiyo.
âWakulima wenyewe wengi huamini kuwa kilimo ni adhabu na wengine hufanya shughuli hiyo kwa sababu tu, wazazi wao walikuwa wakifanya na mbaya Zaidi ni kwamba nao wanatumia mbinu za zamani kuifanya shuguli hiyo hivyo SUGECO imejikita katika kuondoa dhana hiyo.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa FORUMCC, Rebecca Muna alisema wanayo kiu ya kuona wanachama wake wanatekeleza walichojifunza katika ziara hiyo badala ya kuishia kubaki nayo kwa nadharia.
Alisema msingi wa kuyaishi mafunzo hayo ni kujitambua, kujitathmini na kujua nafasi yako kwenye jamii.
âKila mtu anaweza kuwa chochote anachohitaji kama tu, atatambua wajibu wake. Tujitathmini ili kujua nafasi zetu kwenye jamii hakuna kitakachoshindikana kwenye lolote,â alisema.
Alisema pasi na kujitambua kila mtu atabaki kulalamika na hatimaye kujiona hatoshi kufanya anachopaswa kufanya na hapo ndipo wengi hujikuta wakiendelea na kilimo kisicho na tija huku wakiharibu mazingira maradufu.
Recent Comments