MWANASIASA Mkongwe nchini Paul Kimiti, amemzungumzia kwa kina aliyekuwa Naibu Waziri wa Kilimo na Mifugo mwaka 1995, Njelu Kasaka, kuhusu uimara wake katika utumishi wa umma huku akitoboa siri ya kikao walichoitwa na Mwalimu Julius Nyerere Ikulu ndogo mkoani Mbeya, kuhusu nafasi ya urais.
Akizungumza na Simamia.com leo Mzee Kimiti amesema rasmi alimtambua Kasaka kutokana na uimara wake katika utumishi wa umma kwani aliwahi kufanya nae kazi wakati yeye alipokuwa Waziri wa Kilimo na Mifugo huku Kasaka akiwa Naibu wake.
Amesema Mzee Kasaka, alikuwa kiongozi asiyekubali kuyumbishwa, hivyo alisimamia kile alichoona kina afya kwa umma na kukitekeleza bila kumhofia yeyote.
âMzee Kasaka aliwahi kuwa Naibu Waziri wangu, hapo ndipo nilipoona utendaji wake na kwa sababu alikuwa Naibu Waziri wa Kilimo na Mifugo kabla ya mimi kuteuliwa Waziri wa wizara hiyo, tayari alishakuwa na uzoefu katika nafasi hiyo na alinisaidia kazi vizuri,â amesema.
WALIVYOFAHAMIANA
Mazee Kimiti, amesema alimfahamu baada ya yeye kuhamishwa kutoka Kagera na kuwa Mkuu wa Mkoa wa Mbeya mwaka 1990 ambapo alimkuta Mzee Kasaka akiwa Mbunge wa Chunya mkoani humo.
Amesema muda mchache baadae Mzee Kasaka aliteuliwa kuwa Naibu Waziri wa Kilimo na Mifugo nafasi ambayo alidumu nayo hadi yeye alipoteuliwa kuwa Waziri katika wizara hiyo.
Ameongeza kuwa walifanya kazi pamoja katika Wizara hiyo hadi hapo alipohamishiwa Wizara ya Kazi na kumuacha Mzee Kasaka akiwa Naibu Waziri wa Kilimo na Mifugo.
Amesema utendaji wake mzuri serikalini ndio uliomfanya asienguliwe katika nafasi ya Naibu Waziri hata aliteleza kwa kujiingiza katika sakata la G55.
SIRI YA KIKAO NA MWL. NYERERE
Katika mahojiano hayo Mzee Kimiti ametoboa siri ya kikao walichofanya yeye Mzee Kasaka na Mwalimu Julius Nyerere katika Ofisi za Ikulu Ndogo mkoani Mbeya.
Amesema alipokuwa Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Mwalimu Nyerere alikuwa na ziara mkoani humo kwa ajili ya kutembelea mashamba makubwa ya mpunga na ilibidi afanye na Naibu Waziri wa Kilimo ambaye ni Mzee Kasaka.
Mzee Kimiti amesema baada ya ziara hiyo jioni wakiwa Ikulu ndogo mkoani humo, Mwalimu Nyerere aliwaita yeye na Mzee Kasaka kwa ajili ya mazungumzo.
Amesema katika mazungumzo hayo Mwalimu Nyerere alimuhoji yeye kwamba anafikiria kugombea Urais.
âMimi nilikataa baada ya kuhojiwa hivyo kwa kujibu kwamba nafasi ya Mkuu wa Mkoa inanitosha hata hivyo niliona sina uwezo wa kushika nafasi hiyo na Mwalimu alinisifia kwa kusema kuwa nina akili sana,â amesema.
Amesema baadae Mwalimu Nyerere alimgeukia Mzee Kasaka na kumwambia kuwa hawezi kupata urais kwa sababu ya umaarufu aliojizolea kutokana na sakata la G55.
KUHUSU G55
Mzee Kimiti amesema Mzee Kasaka aliwahi kutereza katika uongozi wake ambapo mwaka 1993 pamoja na viongozi wengine walianzisha G55 iliyokuwa na lengo la kuvunja muungano kwa kuwa na serikali tatu.
Amesema hatua hiyo ilipingwa vikali na Mwalimu Nyerere kwa kusema kuwa jaribio hilo lingevunja Muungano.
Mzee Kasaka alifariki Dunia usiku wa kuamkia jana, kwenye Hospitali ya rufani mkoani Mbeya, alipofikishwa Ijumaa baada ya kuugua ghafla na kuacha mjane na watoto nane.
Hadi anafariki Mzee Kasaka alikuwa na umri wa miaka 78, ambapo alizaliwa mwaka 1942, Chunya mkoani Mbeya.
Kabla ya umauti Mzee Kasaka aliwahi kuhudumu nafasi mbalimbali serikalini ikiwemo Mbunge wa Chunya, Naibu Waziri wa Kilimo na Mifugo na baadae Mkuu wa Mkoa wa Iringa na Tabora.
Recent Comments