Recent Comments

ZIJUE TARATIBU ZA UPEKUZI (SEARCH) KISHERIA ZITAKAZO FANYWA NA POLISI DHIDI YAKO.

By Simamia Journal Aug 19, 2020

Na. Comred Mbwana Allyamtu.
Thursday -28/6/2018.
+255679555526.

Leo tutaendelea katika mfululizo wa utoaji wa elimu ya sheria katika nyanja ambazo ni changamoto katika jamii yetu hivyo kwa msingi huu leo tutaangazia katika kipengere cha upekuzi na taratibu zake kisheria.

?Kupekua ( search) ni tendo ambalo hufanywa na mamlaka za usalama katika maeneo mbalimbali hasa katika makazi ya watu. Mbali na makazi ya watu kupekua pia kwaweza kufanyika katika magari, treni, na vyombo vyote vya usafiri zikiwemo ndege na meli.

Pia kupekua kwaweza kufanywa kwa mtu kwa maana kuwa mtu kama mtu naye anaweza kupekuliwa(search). Iwe mifukoni au wapi lakini mtu naye hupekuliwa. Kwa jina la mtaani kupekua hujulikana kwa jina la kupiga sachi. Hivyo basi kupekua na kupiga sachi ni kitu kilekile.

Mbali na kuwa upekuzi waweza kufanyika sehemu nyingi kama tulivyoona makala haya yatagusa upekuzi katika maeneo ya nyumbani kwa maana kwenye makazi au maofisi. Suala la upekuzi kwa ujumla wake huongozwa na Sura ya 20, Sheria ya Mwenendo wa makosa ya Jinai yani Criminal procedure Act Cap 20 kama ilivyofanyiwa marekebisho 2002 na wakati mwingine Sheria ya Jeshi la Polisi Sura ya 322 yani The police force and auxiliary service Act Cap 322)

Katika sheria ya Mwenendo wa mashtaka ya jinai (Criminal procedure Act Cap 20) pamoja Kanuni za jumla za jeshi la police (General police order) zimetoa na kuelekeza upekuzi halali kisheria ikiwa ni pamoja na ule unaokubalika kisheria.

kimsingi upekuzi umegawanyika katika aina Tatu (3)

1- upekuzi kwa mtu (search for person) chini ya Kifungu cha 27,41 CPA.
2- upekuzi kwa makazi (search for premises) chini ya Kifungu cha 38,40 cha CPA.
3- upekuzi kwa vyombo vya moto (search for motor vehicle) chini ya Kifungu cha 25 cha CPA.

Mambo ya msingi ya kuzingatia katika upekuzi ni kuzingatiwa kwa sheria na Kanuni zote za haki za msingi wakati Wote wa upekuzi unapo fanyika.

ZIFUATAZO NI VITU VYA KUZINGATIA KABLA YA UPEKUZI KUFANYIKA.

Kabla ya askari ajakupekuwa au kupekuwa nyumba yako anatakiwa kuwa na vitu vifuatavyo:

  1. KITAMBULISHO.
  2. BARUA YA SEARCHING ORDER INAYOONESHA KITU KINACHOKUJA KUTAFUTWA ( hii ni kwa mujibu wa sheria ya Mwenendo wa mashauli ya jinai Kifungu cha 45(1),112(1),121 cha sheria CPA.
  3. AWE AMEFUATANA NA KIONGOZI WA MTAA WAKO (ANAWEZA KUWA MJUMBE, MTENDAJI N. K)

?KABLA YA ZOEZI LA KUPEKUWA.

  1. Unatakiwa kumuuliza askari anataka kutafuta nini.
  2. Unaruhusiwa kumsachi askari Kwanza kabla hajaanza upekuzi (kuepuka kubambikiwa vitu usivyokuwa navyo)
  3. Una haki ya kukataa kupekuliwa na huyo askari endapo unamtilia mashaka.

katika kitendo cha search kiliweza kufafanuliwa kwenye kesi ya #OlothoV_R. (1970) HCD No 204. Ambapo mahakama ilisema ya kwamba upekuzi wowote uta tafsilika ni batili kama sheria inayoongoza upekuzi haitafuatwa.

1.SABABU ZA KUPEKUA.

Kisheria sababu za kupekua lazima iwe ni katika kutafuta ushahidi ambao utawezesha kupatikana kwa ukweli wa jambo fulani ambalo lipo katika ngazi za upelelezi katika mamlaka fulani. Hauwezi kufanyika upekuzi nyumbani kwa mtu kwa lengo jingine na hilo likitokea basi itakuwa ni kinyume cha sheria.

Sehemu inayopekuliwa ni lazima kuwepo na tetesi au uhakika wa kuwa eneo hilo upo ushahidi unaotafutwa kwa ajili kuanzisha,kuendeleza au kukamilisha upelelezi fulani. Kwa hiyo sababu kubwa ya upekuzi(search) ni kutafuta ushahidi.

Hakuna upekuzi kwa ajili ya sababu binafsi.

  1. NANI HUTAKIWA KUFANYA UPEKUZI (SEARCH).

Askari polisi anayo mamlaka ya kufanya upekuzi katika nyumba ya mtu hii ni kwa mujibu wa Kifungu cha 38 cha sheria ya Mwenendo wa makosa ya jinai. Nyumba yaweza kuwa ya makazi au ya biashara kama duka, mgahawa, hoteli, nyumba za wageni, na vyuoni na mashuleni.

Zaidi maafisa wengine kama taasisi ya kuzuia na kupambana na rushwa au wale wa mamlaka ya chakula na dawa ( TFDA) n.k.nao wanaweza kufanya upekuzi . Isipokuwa maafisa hawa wengine kama mamlaka ya chakula na dawa wanaruhusiwa kufanya upekuzi katika yale maeneo yanayohusu ile kazi yao tu, kwa mfano dukani kukagua bidhaa basi na si kuingia mpaka chumbani kwa mtu.

Hata hivyo wanashauriwa kuambatana na afisa wa polisi mara zote wanapoamua kufanya upekuzi.

  1. HAIRUHUSIWI KUFANYA UPEKUZI USIKU BILA KIBALI CHA MAHAKAMA.

Kifungu cha 40 cha Sheria ya Mwenendo wa makosa ya Jinai kinasema kuwa hati ya upekuzi inaweza kutolewa na kutekelezwa siku yoyote na inaweza kutekelezwa kati ya muda kuchomoza au kuchwa kwa jua lakini mahakama inaweza kwa maombi ya afisa polisi au mtu mwingine yeyote ambaye imeelekezwa kwake kumruhusu kutekeleza muda wowote.

Katika tafsiri ya kifungu hiki kuna mambo mawili ya msingi.

?Kwanza tunaona kuwa upekuzi kawaida unatakiwa ufanyike siku yoyote kati ya jua kuchomoza na jua kuchwa. Jua kuchwa ni jua kuzama. Kawaida muda wa jua kuchomoza maeneo mengi ya Tanzania ni kuanzia Sa 12 za asubuhi na ,maeneo mengine saa 11 za asubuhi. Na muda wa jua kuzama maeneo mengi ni kati ya saa 12 za jioni hadi saa moja jioni. Kwahiyo huo ndio muda wa kawaida ambao upekuzi unatakiwa kufanyika kwenye nyumba za watu. Kimsingi ni muda wa mchana( day time).

?Pili, tafsiri inayofuata katika kifungu hicho ni pale kinaposema kuwa kwa kibali maalum cha mahakama upekuzi unaweza kufanyika muda wowote. Hapo juu tumeona upekuzi unatakiwa kufanyika katika muda maalum ambao kimsingi ni asubuhi mpaka jioni (mchana).

Hapa sasa tunaona kuwa upekuzi unaweza kufanyika muda wowote ikiwemo usiku wa manane lakini hii itakuwa kwa kibali maalum cha mahakama. Kwahiyo tunaona wazi kuwa ili upekuzi ufanyike usiku yapaswa kuwepo kibali cha mahakama ambacho kimeruhusu kufanya hivyo vinginevyo upekuzi wote hutakiwa kufanyika masaa ya mchana. Kwa maana hii unapogongewa usiku na askari wanaojitambulisha kuhitaji kufanya upekuzi kwako basi kabla ya kuruhusu zoezi hilo kufanyika omba kuona kibali cha mahakama hata kupitia dirishani kwanza.

Pia ikumbukwe kuwa upekuzi unaweza kufanyika bila kuwepo na kibali (Search without warrant) na hii ni kwa mujibu wa sheria hii ya Mwenendo wa makosa ya jinai Kifungu cha 38 na 42.

Pia sheria ya Mwenendo wa makosa ya jinai yani Criminal procedure Act Cap 20 R. E 2002 imeipatia police uwezo wa kushikilia (seize) kitu chochote itakacho kitilia shaka wakati wa ufanyaji wa upekuzi kama sehemu ya ushahidi katika upelelezi wa uendeshaji wa shitaka.

ACHA KUNYANYASWA, TAMBUA HAKI YAKO, CHUKUA HATUA.

By Simamia Journal

Tangaza nasi. www.simamia.com YouTube Chanel: www.youtube.com/c/SimamiaTv