MGOMBEA wa Ubunge Jimbo la Kibamba Issa Mtemvu, amesema hali duni ya maendeleo iliyopo katika Jimbo hilo na Ubungo, inatokana na kukosekana kwa utashi wa maendeleo ya dhati kwa wabunge waliomaliza muda wao katika majimbo hayo.
Hayo ameyasema leo wakati alipozungumza na simamia.com na kuongeza kuwa kwa kipindi cha miaka 10 majimbo hayo yalikuwa chini ya wabunge walioghubikwa na siasa za maneno bila utekelezaji.
Kwa mujibu wa Mtemvu, kitendo cha wananchi wa majimbo hayo kuwachagua wabunge hao kwenye uchaguzi wa mwaka 2010 na 2015, ni mithiri ya kuonja sumu iliyoangamiza maendeleo na kuwapa ugumu watendaji wengine wa Serikali kuitekeleza vyema ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM).
âWaliokuwepo katika majimbo haya ni dhahiri kwamba walikosa utashi wa maendeleo ya kweli na badala yake walijikita katika kufanya siasa za maneno mengi bila utekelezaji na wengine huku baadhi yao hawakuwahi hata kuishi kwenye majimbo yao,â amesema.
Mtemvu, amesema uwepo wake katika jimbo hilo ni chachu ya kuimarika kwa maendeleo kwa kile anachoamini kuwa ushirikiano baina yake na wananchi kupitia CCM, utaleta nguvu ya pamoja katika kutatua changamoto zilizopo.
Amesema amewiwa kugombea ubunge katika jimbo la Kibamba, kwani ndio eneo analoishi, hivyo anao utashi wa maendeleo ya dhati kwa watu wa jimbo hilo.
Ameongeza kuwa mwaka 2010 hadi 2015, aliwahi kuwa Diwani wa Kata ya Kibamba, kipindi ambacho kilimfanya kutambua changamoto nyingi za sehemu ya jimbo hilo, huku akishiriki kwa kiasi kikubwa kuzitatua zilizokuwa katika kata hiyo.
âNilipokuwa diwani kulikuwa na changamoto za huduma ya afya, maji, miundombinu na shule zilikuwa chache hususan za msingi, lakini nilitumia busara kuwaomba Wazee wenye ardhi, walitoa na ilifanikisha kujenga Zahanati, Kituo cha Polisi Gogoni na shule kadhaa,â amesema.
Amesema changamoto zilizopo katika Kata ya Kibamba zinatafsiri jimbo lote, muhimu ni kupata kiongozi mwenye utashi wa maendeleo ili kuzitatua.
Mtemvu, ameongeza kuwa amejipanga kushirikiana na wananchi na viongozi wengine akiwemo mgombea wa Jimbo la Ubungo Profesa Kitila Mkumbo, kuhakikisha CCM inapata ushindi katika jimbo hilo, Kata zote kadhalika na ushindi wa Dk. John Magufuli.
Ameongeza kuwa kinachowapa nguvu ni heshima iliyopo ndani ya chama hicho kwa sasa ambayo imetokana na utendaji wa Rais Dk. Magufuli kwa kipindi cha miaka mitano.
Amesema licha ya Dk. Magufuli, kutopata kura nyingi katika uchaguzi wa mwaka 2015 kutoka katika jimbo hilo na Ubungo lakini amekuwa akielekeza fedha mbalimbali kwa ajili ya ujenzi wa miradi ya kimkakati na uboreshaji wa huduma za wananchi.
Kadhalika Mtemvu, amesema Septemba 6, mwaka huu anatarajia kuzindua rasmi kampeni kwenye jimbo hilo, huku jimbo la Ubungo likitarajia kufanya hivyo Septemba 5, mwaka huu.
Recent Comments