KATIBU Mkuu wa Umoja wa Vijana Chama Cha Mapinduzi (UVCCM), taifa Mwalimu Raymond Mangwala, amebainisha mambo matatu ambayo ni mtaji wa ushindi wa kishindo wa chama hicho kuelekea uchaguzi Mkuu wa mwaka huu, ikiwemo kupita bila kupingwa kwa wagombea wake wa nafasi mbalimbali katika baadhi ya majimbo na kata nchini.
Amesema mambo mengine ni utekelezaji wa Ilani ya CCM, mwaka 2015/2020, uliofanywa na Rais Dk. John Magufuli, kwa kipindi cha miaka mitano ya uongozi wake na kukosekana kwa sera zenye mashiko kutoka kwa vyama vya upinzani nchini.
Hayo aliyasema jana wakati wa ziara yake ya kimkakati kwa vijana wa CCM, Wilaya ya Ubungo, ikiwa ni endelevu kwa wilaya zote za mkoa wa Dar es Salaam.
Alisema chama hicho tayari kinao mtaji wa kutosha unaoashiria ushindi wa kishindo kwa nafasi zote zinazogombea, hiyo ni kutokana na namna kilivyojiandaa kufanikisha hilo.
Kwa mujibu wa Mwalimu Mangwala, jambo la kwanza ni idadi kubwa ya wagombea wanaosubiri kuthibitishwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), kwani hadi sasa wanatajwa kukosa upinzani kwenye maeneo waliyogombea.
Alisema wagombea hao ni 722 katika Kata mbalimbali nchini kwa nafasi ya udiwani huku majimbo yakiwa ni 22, kwa nafasi ya ubunge.
âTunaingia kwenye uchaguzi huku tukiwa na mtaji mkubwa wa majimbo 22 na kata 722, ambazo wagombea wake wanasubiri maamuzi ya NEC ili wathibitishwe kuwa rasmi wamepita bila kupingwa,â alisema.
Kadhalika Mwalimu Mangwala, alisema jambo la pili ni kile kitendo cha mgombea wa Urais wa CCM, Dk. John Magufuli, kuwa wa kwanza kuchukua na kurudisha fomu NEC, hatua ambaypo inaashiria umakini wa chama hicho.
âMgombea wetu wa nafasi ya Urais ndiye aliyekuwa wa kwanza kuchukua na kurejesha fomu hivyo, kwa namna hii tulivyoonyesha kuwa viongozi ndivyo tutakavyofanya hata wakati wa uchaguzi, naamini tutaongoza kwa sababu tumejipanga vyema,â alisema.
Kuhusu jambo la tatu Mwalimu Mangwala, alisema ni nguvu ya utendaji wa serikali ya awamu ya tano ambapo hadi sasa imefanya mambo makubwa ikiwemo utekelezaji wa miradi ya kimkakati kama ilivyoainishwa kwenye ilani ya uchaguzi ya chama hicho mwaka 2015/2020.
Aidha Mwalimu Mangwala, aliwataka vijana kuwaepuka wanasiasa wa vyama vya upinzani ambao mara kadhaa wamekuwa wakijikita katika kampeni zisizo na msingi wa maadili ya nchi na kuhatarisha amani.
âKuna wanasiasa wanadai hadi leo Tanzania kuna Covid 19, uthibitisho wa kutokuwepo kwa ugonjwa huo, umedhihirika kufuatia umati wa watu waliojitokeza kushangilia vilabu vya soka nchini katika Siku ya mwananchi ya Klabu ya Yanga na Siku ya Mabingwa ya klabu ya Simba,â alisema.
Alisema kilichofanywa na serikali katika kupambana dhidi ya Covid 19, kimeyafikirisha mataifa mengi Duniani huku mengine yakianza kuiga mbinu zilizotumika.
Aliongeza kuwa kwa nana vijana walivypojipanga kuelekea uchaguzi kuna kila namna ya ushindi wa kushindo kwa CCM, kwa nafasi zote zinazowaniwa ambazo ni Urais, Ubunge na Udiwani.
Kwa upande wake Mgombea wa Ubunge wa jimbo la Kibamba wilayani humo, Issa Mtemvu, alisema tayari chama hicho kimeshajiandaa vya kutosha kuhakikisha jimbo hilo linarudi kwa CCM.
Alisema pamoja na mambo mengine wamekuwa wakitembea wananchi wa makundi mbalimbali ili kuzungumza nao na kuwaomba kura na kufanikisha ushindi wa chama hicho.
Aliongeza kuwa kabla ya nafasi hiyo anayogombea aliwahi kuwa Diwani wa Kata ya Kibamba iliyopo wilayani humo na kushika nafasi mbalimbali ndani ya chama ngazi ya Kata, wilaya na Mkoa, hivyo anao uzoefu nauelewa wa kutosha kuhusu utumishi ndani ya chama na serikali.
Recent Comments