IMEELEZWA kuwa kukosekana kwa huduma za kijamii zilizoahidiwa na aliyekuwa mgombea ubunge wa Chama cha CHADEMA, John Mnyika, kwenye uchaguzi wa mwaka 2015, ndio sababu zilizomkimbiza kugombea tena nafasi hiyo katika Jimbo la Kibamba.
Kwa mujibu wa wakazi wa Kata ya Goba, iliyopo jimboni humo, tangu Mnyika, alipochaguliwa kuwa mbunge wao, hakuwahi kuonekana huku changamoto ya maji ikiwa miongoni mwa kero kuu katika kata hiyo.
Katika uzinduzi wa kampeni za mgombea Udiwani wa Kata ya Goba kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), wananchi hao kwa nyakati tofauti wameeleza namna mbunge wa upinzani alivyosababisha kukithiri kwa kero katika Kata hiyo.
Lilla Mwandaliwa, mkazi wa kata hiyo, amesema kwa kipindi cha miaka mitano hawakuwahi kumuona Mnyika akienda kusikiliza kero zao.
Amesema kwa kipindi hicho chote kata hiyo imekosa huduma za maji, hali inayowasababishia kutumia gharama kubwa kupata huduma hiyo ambapo wanalazimika kununua Ndoo ya lita 20, kwa sh. 700 hadi 1,000.
Ameongeza kuwa katika hata hiyo ni Mtaa wa Kinzudi pekee, ndio umefikiwa na huduma ya maji na mradi huo unatekelezwa na serikali kuu.
âHakuwahi kuja hata kujua changamoto tulizonazo, hii imefanya tubaki na ukame na changamoto nyingine za huduma za kijamii,â amesema.
Wakati akijinadi katika uzinduzi huo Mgombea Udiwani wa Kata hiyo, Ester Doha, amesema Mnyika amekimbizwa na utendaji wake katika jimbo la Kibamba.
Amesema isingewezekana kwa mgombea huyo kuomba ridhaa ya ubunge kwa uchaguzi wa mwaka huu, ukizingatia hakuna chochote alichowafanyia wananchi wa jimbo hilo.
Aliongeza kuwa utendaji wa Mnyika katika jimbo hilo ni kielelezo tosha cha utendaji wa wagombea wa vyama vya upinzani nchini, kwa nafasi zote wanazowania.
âUtatambua kuwa sio watendaji wazuri kwa kusikiliza kile wanachokizungumza majukwaani, wanaishia kulalamika badala ya kusema watawafanyia nini wananchi, tuwapime kwa hili kisha tufanye maamuzi sahihi siku ya uchaguzi kwa kuichagua CCM,â alisema.
Amesema miongoni mwa vipaumbele vyake atakapopata ridhaa ya kuchaguliwa ni kushirikiana na viongozi wa serikali za mitaa pamoja na wananchi ili kujua kero zao na kuziwasilisha kwenye mamlaka husika na kusimamia utekelezaji wake.
Amesema anatambua changamoto kubwa katika Kata ya Goba ni upatikanaji duni wa huduma ya maji, afya, mikopo kwa makundi mbalimbali na uchache wa shule, mambo ambayo atasimamia kuhakikisha yanashughulikiwa.
Ameongeza changamoto nyingine ni miundombinu hususani barabara za kuingia mitaani ambazo husababisha wanafunzi kutoka usiku nyumbani ili kuwahi shuleni, hivyo atasimamia kwa kushirikiana na mamlaka husika kutatua kero hiyo.
Naye Mgombea Ubunge wa CCM, Jimbo la Kibamba Issa Mtemvu, amesema pamoja na kushughulikia changamoto zilizoainishwa na mgombea udiwani, pia atasimamia kuhakikisha vijana wa jimbo hilo wananufaika na ajira zinazotokana na miradi ya kimkakati inayotekelezwa jimboni humo.
Amesema atahakikisha mikopo iliyoainishwa kwenye Ilani ya CCM, inawafikia walengwa kwa usawa na kwa wakati ili wajiinue kiuchumi.
Ameongeza kuwa atasimamia mikopo ya wafanyabiashara kupitia mifuko mbalimbali iliyotengwa na Serikali kuu ili kuwanufaisha wananchi wa jimbo hilo.
Amesema pamoja na mambo mengine pia atahakikisha wazee wananufaika na huduma za matibabu bure na kupambana na wauguzi wanaokiuka kanuni na taratibu za kazi zao na kuwasababishia wazee hao kuchelewa kupata huduma.
Recent Comments