NI ukomavu wa aina yake, ndivyo inavyoweza kusemwa kuakisi kinachodhihirika kwa waliotia nia ya ubunge kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), katika Majimbo ya Kibamba na Ubungo, ambao licha ya kutoteuliwa na chama hicho, lakini wameunda umoja wa kufanikisha ushindi wa walioteuliwa.
Kitendo cha kukatwa kwao kilidhaniwa na kutabiriwa na wanasiasa kadhaa hususan wa vyama vya upinzani kuwa kitasababisha wao kuunda makundi ya kukisaliti na kukihujumu chama hicho kama ilivyotokea mwaka 2015, badala yake wameunda timu za kufanikisha ushindi wa waliopata nafasi ya kuteuliwa kugombea ubunge majimboni humo.
Mchakato wa kutia nia katika majimbo hayo ulihusisha wagombea wengi zaidi ya yote nchini, ambapo Kibamba pekee walikuwepo 176 huku Jimbo la Ubungo walikuwa 111, hivyo ilidhaniwa pengine kukatwa kwa wengine kungezua makundi yatakayokiangusha chama hicho.
Kinachoendelea kushudiwa sasa, kwa mujibu wa watia nia wenyewe kinatokana na dhamira ya dhati ya kila mmoja wao ya kuyakomboa majimbo hayo kutoka mikononi mwa vyama vya upinzani.
Ikumbukwe kuwa kwa kipindi cha miaka 10, tangu kuanzishwa kwa Jimbo la Kibamba na Ubungo chini ya Wilaya mpya ya Ubungo, yamekuwa katika utawala wa chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kwa nafasi za ubunge na kata nyingi kwa nafasi za Udiwani.
Watia nia wafunguka, mshikamano uliopo
Dismas Mwakatundu, aliyetia nia katika jimbo Ubungo, anasema siri ya kutokuwepo kwa makundi ya hujuma kwa chama hicho kwa watia nia waliokatwa mwaka huu, ni kwamba wote walikuwa na dhamira moja ya kukomboa majimbo hayo kutoka katika utawala wa upinzani.
âWote tulijikuta tunajinadi kwa utayari wa kushirikiana na yeyote atakayepata nafasi ilimradi CCM ishinde,â anasema.
Anasema kilichowasukuma kuwa na dhamira hiyo ni utendaji duni wa wabunge waliomaliza muda wao, kutotekeleza ahadi zao huku baadhi yao waliishi nje ya majimbo hayo, hivyo hawakutambua changamoto.
Anasema siri nyingine ya muungano huo wa wagombea ni ukweli kwamba, mchakato wa kura za maoni uliendeshwa bila kuzua hofu, sintofahamu wala malalamiko ya kuhujumiwa kutokana na uwazi uliotawala.
âKila mgombea aliridhika na alichokipata kutokana na uwazi uliotawala, hivyo ukilalamika kwanini haukuteuliwa na chama ilhali hata ukiangalia kura zako hazikutosha na ulihesabu hadharani, hakuna sababu ya kumchukia mtu,â alisema.
Kwa mujibu wa Mwakatundu, kuna kila sababu ya CCM kushinda kwenye majimbo hayo kwani tayari kina mtaji wa kura za watia nia wote na wafuasi wao.
Naye Benard Kihiyo, aliyetia nia kugombea jimbo la Kibamba wilayani humo, anasema umoja na mshikamano unaoonekana sasa ni matunda ya utofauti wa mchakato wa kura za maoni ndani ya CCM ukilinganisha na miaka ya nyuma.
Anasema katika mchakato huo, mwaka huu, chama kiliona hekima ya kuwaweka wanachama wake tayari na matokeo yoyote ya uteuzi yatakayofanywa na viongozi wa chama.
Anasema pia namna mchakato huo ulivyoendeshwa, ulifanya kila mgombea ajione ana thamani kwa chama na viongozi wake, kwani hakukuwa na watu kujikweza kwa umaarufu wao wa kisiasa.
âBila kujali unajulikana ama laa, chama na viongozi wake walitupokea kwa usawa, hii ilitufanya sote tujione na thamani kwa chama chetu, hivyo hakuna sababu ya kukisaliti, zamani watu wenye uwezo wa kifedha na wenye umaarufu wao walikwenda hata kuchukua fomu kwa shangwe nyingi,â anasema.
Kihiyo anasema kutokana na sababu hizo, kuna kila ishara ya ushindi wa kishindo kwa CCM katika majimbo hayo na Kata zake.
Anasema ushindi wa CCM wilayani humo unasukumwa na mshikamano uliopo, pia utendaji wa Dk. John Magufuli, umekiheshimisha na kukithaminisha chama hicho.
Issa Mtemvu, aliyeteuliwa na CCM kuwania nafasi hiyo katika jimbo la Kibamba, anasema siri ya mshikamano uliyopo ni uendeshwaji mzuri wa mchakato wa kura za maoni uliofanywa na viongozi wa chama wilayani humo.
âUongozi umejitahidi kuweka usawa juu ya maelekezo na kuzingatia kanuni za chama, katika kuwapata wateule watakaopeperusha bendera katika nafasi za ubunge,â anasema.
Anasema siri kubwa zaidi ni uwazi uliotawala kwenye mchakato huo ambao ulimfanya kila mgombea kuona alichokipata ndio haki yake na kuondoa imani za kuwepo kwa hujuma.
âKura zilihesabiwa hadharani, ulifanyika uchunguzi wa kutosha juu ya hila, hayo yameleta amani ambayo imefanya watia nia wote wajione na wajibu wa kushirikiana na aliyeteuliwa kwa sababu ni mteule wa kweli,â anasema.
Anasema pia katika kuondoa makundi, chama kiliamua kufanya uamuzi wa kuwateua wote walioongoza kwa kura wakati wa mchakato wa ndani.
Kwa mujibu wa Mtemvu, siri nyingine ni sifa za wateule, kwamba ndio waliokuwa matarajio ya wajumbe na wananchi kwa ujumla hivyo, kujitokeza kwao kumefanya wajumbe waamini kutatuliwa kwa changamoto zao.
Katibu CCM, Ubungo atoboa siri ya mshikamano huo
Katibu wa CCM Wilaya ya Ubungo, Chief Yaredi, anasema kinachoonekana sasa ni matunda ya utendaji haki uliofanywa wakati wa mchakato wa kura za maoni.
Anasema kama ilivyoagizwa na Mwenyekiti wa CCM taifa Dk. John Magufuli, kuwa mchakato wa kura za maoni uwe na uwazi, kila mgombea ameona alichokipata ndio stahili yake hivyo hakukuzuka dhana za kuonewa au upendeleo.
Yaredi anaongeza pia siri ya mshikamano huo, ni wanachama wa chama hicho kutambua mapema kuwa katika kutia nia mwisho wa siku chama kitamteua mgombea mmoja atakayewakilisha chama kwa nafasi ya ubunge katika kila jimbo.
âWalijiandaa kisaikolojia, kwamba pamoja na kujitokeza wengi kugombea lakini hatimae mamlaka za juu za chama zitafanya maamuzi ya kumteua mmoja hivyo maandalizi waliyokuwa nayo yamewafanya wawe na utambuzi na kuondoa manungâuniko,â anasema.
Anasema pamoja na yote, CCM wilayani humo ilikutana na watia nia wote na kuzungumza nao, ili watambue namna chama kinavyofanya katika mchakato huo hivyo wawe tayari kwa maamuzi yoyote yatakayofanywa na uongozi wa juu wa chama.
Anasema hilo lilifanywa kwa wagombea wa nafasi zote wilayani humo kwa maana Ubunge na Udiwani, hivyo mshikamano uliopo ni uhakika wa ushindi wa kishindo.
Wajumbe walonga
Reinhad Chikando, Katibu wa Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM), Kata ya Msigani wilayani Ubungo, ambaye ni miongoni mwa wajumbe waliopiga kura kupendekeza wagombea ubunge, anasema CCM iliingia kwenye mchakato huo ikiwa na mkakati wa ushindi.
Anasema ubora, hekima na busara za chama hicho, zimefanya kiunde mfumo wa uendeshaji wa mchakato utakaomfanya kila mtia nia kuona anastahili kupata alichokipata.
âUtamlalamikia nani kama umepata kura mbili, zimepigwa wazi, umepewa mwenyewe uzishike na umehesabu mwenyewe, hii imeondoa vinyogo kwa watia nia na kuimarisha mshikamano baina yao,â anasema.
Anasema hata wajumbe waliridhishwa na mchakato huo kwani aliyepita ndio chaguo la wengi hivyo hakukuwa na ujanja ujanja.
Recent Comments