WAKAZI wa Kijiji cha Busonzo, Runzewe mkoani Geita, wameilalamikia Kampuni ya STRABAG baada ya kuvamia eneo la kijiji hicho, kumfukuza Mwekezaji mzawa aliyekabidhiwa eneo hilo na kuharibu mitambo yake ya kusagia kokoto huku kinu cha mtambo huo wakikifanya mlingoti wa bendera yao.
Kwa mujibu wa wakazi hao, Mwekezaji huyo mzawa Kitururu General Works and Supplies, walimkabidhi eneo hilo kwa mkataba wa miaka mitano na kwamba kila baada ya muda huo akifanyie kijiji chochote ambacho kingehitaji.
Wanasema kwa miaka mitano hiyo kijiji kilimtaka awajengee Ofisi ya Serikali ya Mtaa na Matundu mawili ya choo na kwamba alifikia hatua ya kupaua ndipo STRABAG walipovamia eneo hilo na kuharibu mitambo yake.
Akizungumza kwa simu kutoka mkoani Geita mmoja wa wakazi hao Thomas Mwengengwa, anasema walikubaliana kumkabidhi eneo mwekezaji mzawa kwa mkataba wenye maslahi kwa kijiji na mwekezaji huyo.
Anasema kwa hatua za mwanzo alionyesha kutekeleza masharti ya mkataba na kutoa msaada mkubwa kwa wananchi kwani aliajiri takriban wanakijiji 200, hadi wazee walikuwa wakifanya kazi ya ukusanyaji kokoto na kujipatia kipato.
âUjio wake ilikuwa ni mithiri ya ukombozi kwa kijiji kwani hakuna aliyekosa ajira kila mtu alikwenda kufanya kazi hapo hadi wasio na nguvu walikuwa wakifanya kuokota kokoto moja moja wanazikusanya na alikuwa akiwalipa lakini hilo liliharibika baada ya kuvamiwa na STRABAG,â anasema.
Mwengengwa anasema mkataba waliokubaliana wanakijiji na mwekezaji huyo ni wa miaka mitano ili awafanyie jambo lolote la maendeleo ambalo wangehitaji na kwamba kwa hatua za awali waliomba kujengewa ofisi ya serikali za mtaa na choo cha matundu mawili na tayari alishaanza kutekeleza.
Anasema baada ya STRABAG kufika hapo walivamia eneo hilo bila hata kwenda kwa serikali za mitaa kujitambulisha na waliharibu mitambo ya Kitururu huku kinu chake cha kusagia kokoto wamekifanya mlingoti wa bendera yao.
Anaongeza kuwa Kitururu hakupewa nafasi ya kuhamisha kifaa chochote kilichokuwepo eneo hilo na hata pia kulikuwa na kokoto za wananchi ambazo nazo walizisambaratisha kwa Katapila hivyo kuwasababishia wananchi kukosa ajira na kupoteza nguvu zao bure.
Mwengengwa anasema STRABAG walipofika hapo hawakutoa ajira hata ya mlinzi kwa wakazi wa eneo hilo walikwenda na watu wao na kwamba shughuli zote walizokuwa wakifanya hazikuwahi kukinufaisha kijiji na badala yake zilikiathiri kwa kiasi Fulani.
Kuhusu athari zilizojitokeza kufuatia uwepo wa STRABAG kijijini hapo Mwengegwa anazitaja kuwa ni kuweka ufa kwa ukuta wa shule ya msingi Busonzo kutokana na mitambo na baruti walizotumia karibu na ukuta wa shule hiyo.
Kwa upande wake Mwekezaji huyo mzawa ambaye ndiye mmiliki wa Kampuni ya Kitururu General Works and Supplies Kitutu Kitururu, anasema uvamizi huo uliathiri shughuli zake katika eneo hilo na hata mitambo yake yote.
Anasema kwakuwa hakupewa hata nafasi ya kuondoa chochote kila kilichokuwepo kiliharibiwa na hivyo kumsababishia hasara kubwa.
Kitururu anasema baada ya kufanyiwa hivyo aliungana na wanakijiji ambao ndio waliomkabidhi eneo hilo na kwenda Wilaya ya Bukombe iliyopo mkoani humo ili kulalamika wakati huo Mkuu wa Wilaya alikuwa Meja Bahati Matala.
Anasema vilifanyika vikao kadhaa kuhusu kujadiliwa kwa suala hilo na baadae STRABAG walidai kuwa eneo hilo wamepewa na Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS), ambao inadaiwa kuwa eneo lilikuwa lao.
Anaongeza kuwa walipoulizwa kuhusu mipaka ya eneo hilo na mkataba wa makabidhiano kati ya STRABAG na TANROADS hawakuonyesha lakini TANROADS kupitia Mhandisi wake mkoa wa Shinyanga wakati huo Ndilimbi, walithibitisha kuwa eneo hilo la kwao.
Kitururu anasema TANROADS walipohojiwa kuhusu mipaka na ukubwa wa eneo hilo walishindwa kubainisha.
âPia vilifanyika vikao vya kutathmini athari zilizosababishwa na STRABAG ikiwemo shule ya msingi Busonzo nao walikubali kulipa fidia za athari walizosababisha lakini hawakufanya hivyo,â anasema.
Anasema katika vikao hivyo STRABAG walikubali kuleta maji ya kunywa mara tatu kwa wiki katika kijiji hicho kilichokuwa na ukame wa maji, huku michakato ya kuchimba Visima vitatu vya maji ya kunywa ikiendelea lakini yote yaliishia kuahidiwa hayakutekelezwa.
Naye Mwenyekiti wa Kijiji hicho, Thomas Dotto, anasema ni takriban miaka 10, tangu STRABAG wamevamia eneo hilo na kufanya shughuli zao bila kijiji kunufaika na chochote.
Anasema hakuna kielelezo chochote kinachoihalalisha Kampuni hiyo ya Kijerumani kuwepo kwenye eneo hilo na kuendeleza shughuli zao kwani kijiji kwa pamoja kinamtambua mwekezaji mzawa Kitururu ambaye ndiye alifika kijijini hapo na kilifanyika kikao na kupewa masharti ya kuyatekeleza naye alishaanza utekelezaji.
Anaongeza kuwa katika vikao vya sakata hilo chini ya Ofisa wa Madini wa Kanda na Mkuu wa Wilaya vilivyofanyika miaka ya 2010, STRABAG walidai eneo hilo walipewa na TANROADS ambapo nao walishindwa kuwasilisha vielelezo vya uhalali wa umiliki wao.
Mwenyekiti huyo anasema pia vilifanyika vikao vya kutathmini athari za STRABAG baada ya kuingia kijijini hapo, nao walikubali kulipa fidia za athari walizozisababisha na kupewa sharti la kuwa wanakiletea maji kijiji na kumwaga maji katika barabara ya kijijini hapo pamoja na mabaki ya kokoto wanazosaga katika kiwanda chao hicho lakini yote hawakuyatekeleza.
âKwa sasa wameshaanza kuondoa baadhi ya mitambo yao wanaondoka kijijini hapo ikiwa tayari walishalitumia eneo kwa miaka zaidi ya 10 na kuharibu mitambo ya Kitururu bila kumlipa pia madarasa mawili ya Shule ya Msingi Busonzo hayatumiki kutokana na ufa wa ukuta uliosababishwa na baruti walizokuwa wakitumia karibu na shule hiyo,â
âKuna wakati tulijenga Zahanati ya kijiji ikafikia hatua ya kukamilisha lakini tulishindwa kupata kokoto, tuliwaandikia barua watusaidie wakajibu kuwa tuiandike kwa kiingereza maana kiongozi wao hajui Kiswahili, tulipofanya hivyo hawakujibu wala kutoa msaada wowote hadi leo wanaondoka,â anasema.
Anasema tumaini lao ni Rais Dk. John Magufuli, aingilie kati na kushughulikia changamoto yao kwani wameathirika pamoja na mwekezaji Kitururu huku Kampuni hiyo iliyovamia inaendelea kuhamisha vifaa vyake ikiwa imeingiza faida pasi na kijiji kunufaika na chochote.
Meneja wa TANROADS Geita, Mhandisi Haroun Senkunku, anasema mgogoro huo umefikishwa ngazi ya Mkoa suala hilo lipo nje ya uwezo wake.
Akizungumza na Uhuru Mkuu wa Mkoa wa Geita, Mhandisi Robert Gabriel, anasema bado mgogoro huo haukumfikia hivyo hawezi kuzungumza lolote kwa sababu hajatambua uhalisia wake.
Recent Comments