KUKOSEKANA kwa sera za kuzungumza kwa wananchi, bado linaonekana kuwa jinamizi linaloendelea kughubika majukwaa ya kampeni za mgombea wa Urais wa Chama cha CHADEMA, Tundu Lissu, kusababisha wakati mwingine kujikuta akitoa ahadi ambazo  serikali ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) chini ya Rais Dk. John Magufuli, imeshazitekeleza.
Kampeni za mgombea huyo, zimejaa kile kinachoweza kusemwa kuwa ni vibweka, na kudhihirisha kuwa mgombea huyo hatambui kilichofanywa na serikali, kutokana na kunadi sera zinazohusu mambo ambayo tayari yalishatekelezwa.
Kadhalika majukwaa ya kampeni za Lissu, yamekuwa yakinadi malalamiko badala ya kueleza sera, vitendo ambavyo vinatajwa kusababishwa na maandalizi duni ya vyama vya upinzani kuelekea uchaguzi wa mwaka huu.
Ushahidi wa hilo, ni kile kilichotokea Septemba 13, mwaka huu, ambapo mgombea huyo akihutubia wananchi Ifakara, wilayani Kilombero, mkoa wa Morogoro, katika kampeni zake za kuwania urais, aliahidi kutaifisha ardhi iliyochukuliwa na matajiri mkoani humo, jambo ambalo serikali ya CCM imeshalitekeleza.
Alidai atakapopata nafasi ya kuchaguliwa na wananchi jambo atakaloanza nalo ni kutaifisha ardhi iliyochukuliwa na Matajiri ambayo kwa mujibu wa maelezo yake, ndio sababu ya migogoro ya wakulima na wafugaji mkoani humo.
WIZARA YA ARDHI YAMUUMBUA
Akizungumza na simamia.com Naibu Kamishna wa Ardhi, Utawala wa Ardhi, Frank Minzikuntwe, amesema kilichozungumzwa na mgombea huyo ni ishara tosha kuwa hatambui hata kilichofanywa na serikali katika nchi yake.
Amesema idadi kubwa ya wananchi wanaolalamikia kutokuwa na ardhi katika mkoa huo, ni wageni, wengine wameuza ardhi kiholela.
âMbali na kutambua kuwa baadhi ya wananchi wameuza ardhi zao kwa wageni kisha wanalalamika, wengine wanaolalamika ni wageni wa mkoa huo, lakini serikali kupitia Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, imetekeleza na inaendelea kufanya kila namna ya kuhakikisha ardhi ya Morogoro inawanufaisha wananchi wake,â amesema.
Amesema kwa kipindi cha mwaka 2015 hadi 2019, tayari wizara hiyo, imeshahakiki jumla ya mashamba 67 yenye ukubwa wa Ekari 221,902.24, na kuandaliwa mpango wa matumizi ya ardhi.
Amesema kati ya ekari hizo, ekari 43,499.8, zinatarajiwa kugawiwa kwa wananchi huku ekari 178,402.45, zitaendelea kubaki serikalini kwa matumizi ya kilimo.
Ameongeza kuwa katika jumla ya mashamba 67, yaliyohakikiwa 49 yenye jumla ya ekari 45,788.5, yapo Wilaya ya Kilosa pekee, eneo ambalo Lissu, anadai mashamba mengi yamemilikishwa kwa matajiri.
Amesema katika jumla ya ekari hizo za mashamba ya Kilosa yaliyohakikiwa ekari 30,672.2, zitagawiwa kwa wananchi kwa ajili ya shughuli za kilimo huku ekari 15,116.3, zitaendelea kubaki serikalini kwa ajili ya matumizi ya baadae.
Kwa mujibu wa Minzikuntwe, mwaka huu wa fedha mashamba 78, yamehakikiwa katika wilaya ya Kilosa pekee, ambapo 11 yenye jumla ya ekakri 24,159, yapo katika hatua za mwisho za kufuta hati zake, huku mengine 18, yalibainika kuwa yametelekezwa.
Amesema katika hayo yaliyotelekezwa bado wanaendelea na hatua za mwisho za ukaguzi na kwamba timu ya wizara ipo maeneo hayo tangu mwezi Julai, mwaka huu, kwa ajili ya kukamilisha kazi hiyo.
âPia timu iliyopo eneo la tukio tangu mwezi Julai, imekagua mashamba mengine 44 na hatua za utumaji wa ilani inafanyika kila baada ya ukaguzi kubaini uvunjifu wa masharti ya umiliki,â amesema.
Minzikuntwe, amesema katika kulinda miliki kwa wananchi wa mkoa wa Morogoro, Wizara ilitekeleza mradi katika wilaya tatu ambazo ni Ulanga, Malinyi na Kilombero ambapo kwa kipande cha ardhi ya vijiji imepangwa, kupimwa na wananchi wameendelea kupewa hatimiliki za kimila.
âMiliki hizi zinasaidia katika kuongeza usalama wa umiliki kwa mwananchi mmoja mmoja,â amesema.
Amesema katika mradi huo wa wilaya tatu, vijiji vyote 129, vimepimwa na mipango ya matumizi ya ardhi katika vijiji 114, imeshakamilika, ambapo vipande vya ardhi ya wananchi 346,000, vimepimwa na jumla ya hatimiliki 218,016 zimetolewa kwa wananchi.
Ameongeza kuwa hatua za ukamilishaji kwa vipande vilivyobakia, unaandaliwa utaratibu na wizara kwa kushirikiana na Halmashauri za wilaya husika.
Pia amesema ili kulinda kila kipande cha ardhi cha mkoa huo wizara imeanza kuhakiki na kujiridhisha kuwa kila mwananchi anatumia ardhi yake kwa muktadha wa uzalishaji.
Kwa mujibu wa Minzikuntwe, utafiti walioufanya umebaini kuwa Mkoa wa Morogoro unaongoza kwa kuuza ardhi kwa wageni.
Amesema serikali imepanga kugawa mashamba yake kwa wananchi waliojiunga vikundi ili kupunguza uwezekano wa kuuza ardhi kwa wageni na kuondoa malalamiko ya wakazi wa eneo husika kutokuwa na ardhi.
Kufuatia vitendo vya Lissu, Mchambuzi nguli wa siasa za Kimataifa na kitaifa, Deus Kibamba, aliwahi kuiambia simamia.com kuwa, vituko vinavyoonekana kwa wagombea wa vyama vya upinzani kuelekea uchaguzi wa mwaka huu, ni matokeo ya mandalizi duni ya vyama vyao.
Alisema kwa tathmini ya kawaida kila kinachofanywa nao, kinaipa nguvu na uelekeo wa ushindi wa kishindo CCM.
Aliongeza kuwa vitendo hivyo ni kujikanganya kwa mgombea kunakosababishwa na kukosa cha kuzungumza.
Recent Comments