Marekani inajiandaa kuondowa wanadiplomasia wake nchini Iraq baada ya kuionya serikali ya nchi hiyo kwamba huenda ikaufunga ubalozi wake.
Hayo yameelezwa na maafisa wawili wa Iraq na wanadiplomasia wawili wa nchi za magharibi wakati hatua hiyo ikiwatia hofu wairaq kwamba huenda ikairudisha nchi yao kuwa uwanja wa vita.
Duru zimefahamisha kwamba waziri wa mambo ya nje wa Marekani Mike Pompeo wiki iliyopita kupitia mawasiliano yake ya simu na rais Barham Salih alitishia kuufunga ubalozi wa nchi yake.
Baadae mazungumzo ya viongozi hao wawili yaliripotiwa na tovuti moja ya habari ya Iraq. Imeelezwa na duru kwamba kufikia jana Jumapili Marekani ilikuwa imeanza maandalizi ya kuwaondowa wafanyakazi wake wa ubalozi endapo uamuzi utachukuliwa.
Wasiwasi uliopo miongoni mwa Wairaq ni kwamba kuondolewa kwa wanadiplomasia wa Marekani kunaweza kukafuatiwa mara moja na hatua ya kijeshi dhidi ya vikosi ambavyo Marekani imevilaumu kwa mashambulizi.
Recent Comments