Mwanafunzi Mwita Juma mwenye umri wa miaka 19, mkazi wa Kijiji cha Kyakoma, Kata ya Kiagata wilayani Butiama mkoani Mara, amefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi wilaya ya Musoma kwa kosa la kumjeruhi Mwalimu wake kwa Panga siku za hivi karibuni.
Akisoma hati ya mashitaka Wakili wa Serikali Mwanadamizi Valence Mayenga mbele ya Hakimu Tumaini Marwa, katika kesi namba 13 ya mwaka 2020, amesema mnamo Septemba 22, 2020, mshtakiwa huyo alitenda kosa hilo akiwa eneo la shule ya sekondari ya Kiagata kwa kumkata kwa panga mwalimu Majogoro John.
Mara baada ya mtuhumiwa huyo kusomewa shtaka lake, mtuhumiwa hakutakiwa kusema chochote kutokana na Mahakama hiyo kutokuwa na mamlaka ya kusikiliza kesi hiyo na Hakimu Tumaini Marwa, alisema uchunguzi wa kesi hiyo bado unaendelea na kuihairisha Oktoba 12, 2020.
Hakimu Marwa amesema dhamana ipo wazi na mshtakiwa anatakiwa kuwa na mdhamini mmoja na masharti ya dhamana ni shilingi milioni 10, mali isiyo hamishika iwe na hati ya umiliki na mdhamini aambatanishe na barua ya utambulisho kutoka makazi anayokaa, lakini mshtakiwa huyo alikosa mtu wa kumdhamini hivyo akarudishwa rumande.
Recent Comments