Wakuu!
Wake kwa waume,
Salaam ya kheri na amani kwenu.
Ni mimi Mwl. Mbelwa Petro, aliyekuwa Mgombea Ubunge Jimbo la Biharamulo Magharibi 2020 kupitia CHADEMA.
Nimeona nitenge dakika 12 kuwaandikia haka ka waraka kafupi japo mjue naendeleaje baada ya shughuli ya uchaguzi mkuu uliopita. Kwa leo sitothubutu kusema mengi kupitia andiko hili, badala yake nitaweka hadharani mambo matano {5} tu ya kiuzoefu niliyoyapitia kwenye ushindani huu wa kisiasa.
Kwanza naomba mnisamehe kwa kuchelewa kuwahakikishia kuwa bado niko salama sana, mwenye moyo na nguvu zaidi kwa ajili ya mapambano yanayofuata hapo kesho kwa kile nilichokiamini na ambacho natamani kiwe kabla sijaiacha Dunia na historia yangu kusomwa mbele ya waombolezaji.
Pili, naomba kuwajuza matokeo ya jumla ya kura kwa kiti cha Ubunge Jimbo la Biharamulo Magharibi kwenye uchaguzi wa 28 Oct, 2020 yaliyotolewa mchana wa 29 Oct, 2020 na msimamizi wa uchaguzi wa jimbo la Biharamulo Magharibi ambaye pia ni Mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Biharamulo, Ndg. Waziri Kombo.
Jumla ya wapiga kura waliojiandikisha kupiga kura walikuwa 177,438 huku idadi ya waliopiga kura ilikuwa 58,758 ambapo kura halali zilikuwa 56,800 na zile zilizoharibika zikiwa ni 1,958.
Achilia mbali ‘sarakasi na tikitaka’, kura za Ezra Chiwelesa – CCM zilikuwa ni 40,526 na kura za Mbelwa Petro – CHADEMA zilikuwa 16,274.{ Kwa taarifa tu, kwa kuwa si wote tulikuwa tumeyapata matokeo haya}.
Kwa ngazi ya udiwani, CHADEMA hatukushinda kata yoyote ya jimbo la Biharamulo Magharibi.
Tatu, napenda kwa dhati kuendelea kutoa shukrani zangu nyingi kwenu wote na kwa kila mmoja kwa jinsi alivyoshiriki kunisaidia au kuniombea ili nimalize mchakato wa kugombea kiti cha Ubunge Jimbo la Biharamulo Magharibi 2020.
Matokeo ya uchaguzi huu uliofanyika mnamo siku ya jumatano 28 Oct, 2020 umekuwa na mambo makuu ya kueleza hata kwa ufupi ili kwa yeyote mwenye kutaka kujua mwendo wa safari hii.
Mosi, nimejua kushinda.
Binafsi nilishinda na nimeshinda katika michakato mikubwa minane (8) ya kiuchaguzi kwenye uchaguzi huu wa 2020, ikiwemo hii hapa chini;
1. Maandalizi ya kugombea kura ya maoni ndani ya chama kikuu cha upinzani nchini mwetu, CHADEMA,
2. Kuteuliwa na kamati kuu ya CHADEMA- Taifa kuwa Mgombea kiti cha Ubunge,
3. Kuteuliwa na tume ya Taifa ya uchaguzi (NEC) kuwa Mgombea kiti cha Ubunge,
4. Kushinda jaribio la kuenguliwa na ofisi ya msajili wa vyama vya siasa (ORPP) lililolenga kuniengua Mimi na madiwani wetu wote wa kata 17 mnamo 11 September, 2020.
5. Kushinda kufanya kampeni kwa siku zaidi ya 60 kwa changamoto za kuzuiliwa baadhi ya mikutano, mfano Mkutano mkubwa wa kufunga kampeni pale Nyakanazi mnamo 27 Oct, 2020.
6. Kushinda dhidi ya jaribio la kutowaapisha mawakala wa CHADEMA na wale wa vyama rafiki vikiwemo NCCR- Mageuzi na ACT waliokuwa wamejitolea kulinda maslahi ya wagombea katika vituo vya kupigia kura 449 jimbo zima la Biharamulo Magharibi. Ingawa baadae msimamizi wa uchaguzi aliwakataa mawakala wote wa ACT na NCCR-Mageuzi. Na miongoni mwa mawakala wa CHADEMA hawakutambuliwa vituoni kwa sababu za kutiana hasira tu.
7. Nimefanikiwa kushinda kiti cha Ubunge jimbo la Biharamulo Magharibi kwenye uchaguzi uliofanyika 28 Oct, 2020 kwa kura bila uhuru wa kitume kusimamia hatamu hiyo.
Ukiweka pembeni sarakasi na tikitaka zote nilishinda kwa kupata kura 53,470 kati ya kura 56,800 zilizopigwa. Ingawa katika uhalisia wa saeakasi na tikitaka rejea matokeo yaliyotangazwa na msimamizi wa uchaguzi.
Na mwisho
8. Nimefanikiwa kushinda uvumilivu wa kisiasa kwa maslahi ya Taifa (Political tolerance for the nation’s wider interests).
Ndugu zangu ushindi wangu katika michakato hiyo mizito ya kisiasa na kiuchaguzi ilitokana na si tu utayari na uwezo wangu kama Mgombea, HAPANA, ushindi huu ulitokana na watu waliokuwa wengi, ikiwemo hata wewe unayesoma andiko hili.
Jambo la nne nilitamani kueleza kuhusu welfare’s cross-section (umbilewima la kiustawi) ya jamii yetu ya Biharamulo tangu tulipopata uhuru (1961) na jinsi ya kujikwamua katika kufanya steppings za kisekta, kiafya, kielimu, kimitaji na kimiundombinu. Hii itamsaidia hata ‘mzawadiwa wa ushindi’ wa kiti cha ubunge wa jimbo letu kwa miaka mitano inayokuja, 2020-2025.
Naona ni hekima kumpa ushirikiano mkubwa huyu ‘mzawadiwa ubunge’ japo uzoefu wa ki changamoto na kimikakati ya kupambana na changamoto hizo kadri nilivyoiishi jamii ya Biharamulo na maeneo nyeti yote kabla na wakati wa kampeni.
Jimbo la Biharamulo Magharibi linazo kata za kiuchaguzi 17, vijiji vyenye mamlaka yake 79 na vitongoji 373.
Mwaka 2017/18 Halmashauri yetu ya wilaya ya Biharamulo pamoja ukongwe wake, ilitajwa kwenye ripoti za kiuchumi kuwa ni Halmashauri ya pili kwa umasikini.
Miongoni mwa live challenges za wilaya yetu kuanzia vitongojini mpaka kwenye Halmashauri ni hizi hapa;
i) Wananchi wa Biharamulo hasa Wakulima na Wafugaji wamenyanyaswa sana na urasmishaji wa hifadhi za Burigi na mapori ya Biharamulo, Nyantakara na Nemba. Wafugaji wetu wengi sasa hapa Biharamulo wanatembea na fimbo mabegani pasipo ng’ombe wao, wamedhulumiwa. Wakulima wamefukuzwa hawalimi Tena.
ii) Katika kilimo na biashara, leo hii Wakulima wetu masikini hapa wanauza pamba na kahawa zao kwa kupewa risiti ya malipo wala si pesa za malipo. Malipo huja nje ya muda wa kuijama tena. Kilimo chetu kimekufa kwa mfumo mbaya wa masoko.
iii) Kijasiriamali, tozo na kodi kwa wajasiriamali na Wakulima zimewakatisha tamaa vijana na wanawake kujiajiri.
Hata mtoto wa shule anayeuza Masungwe ya mwituni ili apate kalamu moja naye alipaswa kulipia kitambulisho cha ujasiriamali. Hapa tujipe muda wa kuwaelimisha watendaji wetu maana ya ujasiriamali.
iv) Kiafya, makundi ya msamaha kwenye matibabu kama Wazee, wanawake wajawazito na watoto under 5 years sasa ni makundi ya kukosa Dawa. Dawa hazipo na zilizopo zina gharama kubwa ukilinganisha na hali za vipato vya wananchi wangu Biharamulo. Mathalani Leo mwananchi mwenye BIMA anajutia kuwa nayo.
v) Kielimu, bado sana wanafunzi na walimu hapa Biharamulo hawana mazingira mazuri ya kupata elimu bora. Watoto Wengine hukaa chini ya miti, na walimu wanaishi mbali na shule.
vi) Kimitaji, vijana wenzangu, wanawake na walemavu hawajapatiwa mikopo kupitia mfuko wa jimbo kama ilivyotakiwa.
vii) Huduma ya maji imekuwa ngumu kwa wananchi wa Biharamulo, huko vijijini maji tunayokunywa mchana ndiyo wanayokunywa wanyama pori usiku. Hili tatizo la maji linakumbuka wananchi wengi kutoka kata zote 17, vijiji 79 na vitongoji vyetu 373.
viii) Ubadhirifu wa mali za umma, ukifuatilia ripoti za Mkaguzi na Mdhibiti wa hesabu za serikali (CAG), Halmashauri ya Biharamulo imekumbwa na matumizi mabaya ya fedha kwa miaka mitatu mfululizo (2017/18/19). Lakini pia hata kupitia ile ripoti ya tume iliyoundwa na RC Kagera ilibaini kutokukusanywa kwa zaidi ya million 300 katika akaunti sahihi.
ix) Na zaidi ya yote wilaya yetu ina udhoofu mkubwa wa mzunguko wa pesa (blocked money cycling).
Jambo la tano na la mwisho kwa leo katika ka waraka kangu haka kwenu ni jinsi gani tunaweza kumalizana na changamoto hizi na hatimaye wilaya yetu ya Biharamulo ku step mbele na kuwa jamii tunayoitamani iwe kwa miaka mitano ijayo (2020-2025).
Hatua hizo ziwe miongoni ama zote mwa hizi;
Hatua ya kwanza kabisa ni uimarishaji wa ushirikiano mwema na wa ki-uadilifu kati ya wananchi, watumishi wote wa sekta rasmi na zile zisizo rasmi, wakiwemo madiwani na Mbunge mwenyewe.
Hatua ya pili iwe uharakishaji wa mpango wa haraka wa upatikanaji wa Bima za afya kwa wananchi kupunguza gharama kubwa za matibabu zinazotufanya masikini kila siku.
Hatua ya tatu, ofisi ya Mbunge, ianzishe mpango wa mfuko vya visima virefu vya Maji kila kitongoji. Kama Mbunge pia aje na mpango pia wa kiwizara kusimika mtambo wa kusukuma Maji kutoka ziwa victoria.
Hatua ya nne, uharakishaji wa umeme vijijini kupitia wakala wa umeme vijiji – Rural Energy Agency (REA). Bado vijiji vingi havina umeme, maeneo mengine zimewekwa nguzo kama mitego ya kuombea kura pasipo umeme. Sasa kwa sababu uchaguzi umeisha na ‘mtego umenasa’ basi ni muda wa kutekeleza filosofia ya siasa kwa ajili ya uchumi, tuachane na hii ya uchumi kwa ajili ya siasa.
Hatua ya tano, yanahitajika mashirikiano makubwa kati ya marafiki wa Kilimo na wakulima ili kutambulisha kilimo cha umwagiliaji na masoko ya tija kwa Wakulima na wafugaji.
Hatua ya sita, kupitia upya mipaka ya hifadhi ili kurejesha haki za wafugaji na wakulima ambao wamedhulumiwa mashamba yao huku wafugaji wakibaki hawana pa kufugia mifugo yao
Hatua ya saba, yatolewe kwa vitendo mafungu ya mikopo kwa vijana, wanawake na walemavu kupitia mfuko wa jimbo ili kusaidia kukuza kiwango cha ajira (employment rate).
Hatua ya nane,
Ukamilishaji wa miradi iliyokwama mfano wa miradi minane 13 yenye matatizo hapa Biharamulo ni kama hii ifuatayo;
1. Mradi wa shule ya watoto wa mahitaji maalumu Biharamulo kujengwa chini ya viwango elekezi.
2. Kushindwa kukamilika Mradi wa Maji Ng’ambo – Biharamulo mjini.
3. Mradi wa ujenzi wa barabara ya lami hapa mjini kati kwa kushindwa kutoa tathimini ya gharama za ujenzi katika mazingira – Environment Impact Assessment.
4. Mradi wa hospital ya wilaya maeneo ya Katoke-Nyarubungo kutokamilika kwa wakati.
5. Mradi wa pembejeo feki na kuwasainisha Wakulima kuwa wamepokea huku si kweli, maeneo mengi.
6. Kukwama kwa Mradi wa maegesho ya magari Nyakanazi, Nyakahura, Biharamulo mjini na Runazi- Kabindi.
7. Kukwama kwa mradi wa ujenzi wa soko la kimkakati la Lusahunga.
8. Mradi wa ujenzi wa Stand ya magari Biharamulo Mjini, Kabindi na Nyakanazi.
9. Mradi wa ujenzi wa chuo kikuu kishiriki cha kikatoliki hapa Biharamulo.
10. Mradi wa ujenzi wa stand Ng’ambo.
11. Miradi ya barabara ya kuelekea hospitali ya Rukarakata – Oscar alikuja na wazo la barabara ya majaribio.
12. Miradi ya ukarabati wa barabara za mitaa na vijiji.
13. Ukamilishaji wa miradi ya nguvu ya wananchi iliyofia njiani pasipo usaidizi wa nguvu ya serikali, mfano madarasa ya shule nyingi za misingi na shikizi vijijini, maboma ya zahanati, madaraja, vituo vya afya, kliniki na ofisi za watendaji wa vijiji.
Hatua ya tisa, usimamiaji wa sera za matibabu bure kwa makundi ya msamaha kama inavyoelekezwa na wizara na huduma hizo.
Hatua ya kumi, ukarabati wa Miundombinu ya Barabara za mjini na vijijini ili kurahisisha usafirishaji wa watu na bidhaa zetu kwenda masokoni, makanisani, mahospitalini, mashambani, hifadhini na kwingineko kokote kuliko na maslahi. Lazima Tanzania Rural Roads Agency (TARURA) ishawishiwe na Mbunge kwa kushirikiana na madiwani wa kata zote 17 kuziweka Barabara muhimu vijijini kuwekwa katika mpango wa usimamizi na ukarabati wake ili kuunganisha kata na kata, wilaya na wilaya.
Hatua ya kumi na moja, kuundwe timu ya misaada ya kisheria kuwasaidia bure wananchi walioumizwa na wanaoendelea kuumizwa na uonevu katika vyombo vya kisheria.
Hatua ya kumi na mbili,
Bodaboda wanahitaji wawe ni watu wenye kuheshimika kama watumishi wengine kwani wana mchango mkubwa katika sekta ya usafirishaji zama za leo. Serikali na wadau wengine wa mambo ya usalama waingilie kati suala la usalama wao dhidi ya abiria wasio waaminifu. Ikumbukwe siku za hivi karibuni kumetokea matukio mengi ya mauaji na uny’ang’anyi wa vifaa vyao vya usafiri. Hawa bodaboda wanahitaji kusaidiwa kuunda jumuiya yenye nguvu kama vilivyo vyama vingine.
Hatua ya kumi na tatu, Mikutano ya hadhara baina ya wawakilishi wa wananchi na wananchi kama waajiri wao na washirika wao wa kimaendeleo kabla na baada ya vikao vya Bunge na Halmashauri.
Hatua ya kumi na nne ni kufanya uchumi wa kitalii kupitia hifadhi ya Burigi, Ibanda na Rumanyika zote za mkoa wa Kagera.
Nimalize kwa kusema ahsanteni sana misaada yenu, poleni sana kwa maumivu na HONGERENI kwa mapambano pevu tuliyokuwa nayo dhidi ya zuruzunga na sarakasi mlizoziona ama kusikia kwenye uchaguzi mkuu huu wa 28 Oct, 2020.
Nisichelewe kukubaliana na wahenga walioamini kuwa ‘asiyekubali kushindwa si mshindani’ huku nikiwa mwaminifu wa dhana ya ‘hakuna marefu yasiyo na ukomo’.
Imani yangu kuu mimi Mwl. Mbelwa Petro ni kuwa muda wowote kuanzia sasa nitakuwa niliyetamani kuwa hapo 28 Oct, 2020 kwa kuwa sijui namna ya kukata tamaa.
Mungu atubariki.
05-11-2020,
Biharamulo.
Recent Comments