Bungeni Dodoma
Leo 11.02.2021, Mbunge wa Jimbo la Ngara alipata nafasi ya kuchangia mpango wa Taifa wa miaka 5 na kuishauri serikali mambo mbali mbali ya msingi yanayotakiwa kutekelezwa na Serikali ili kuongeza uzalishaji wa mazao ya kilimo na Mifugo.
Mh Ndaisaba George Ruhoro amesema kuwa, elimu ya sasa haiwaandai wanafunzi kwenye kujitegemea. Elimu inawaandaa wanafunzi kuwa tegemezi na kutaka kufanya kazi za maofisini ambazo hazipo.
Vijana wanaomaliza kidato cha nne, cha sita hadi vyuo vikuu, wanakuwa wamepishana na ujuzi wa kuandaa na kupanda mazao mbalimbali pamoja na ufugaji. Wanapotoka majumbani mwao kwenda kusoma, huachana na majukuma hayo ya shamba na kupoteza kabisa mapenzi na kazi hizo za kilimo. Wanaporudi majumbani wanachokuwa wamejifunza vyuoni kinakuwa hakiwezi kuwasaidia katika mazingira wanayoyakuta mtaani.
Hivyo Mh. NDAISABA GEORGE RUHORO, ameishauri serikali KUREJESHA MASHAMBA DARASA KWENYE SHULE ZOTE ZA SEKONDARI NCHINI HASA ZILE ZA KATA ili wanafunzi wajifunze kulima na kufuga ili hata wanapomaliza elimu zao wakakosa kazi, wajikite kwenye kilimo. Bila kurejesha mashamba Darasa, vijana wataendelea kukionea kinyaa kilimo na ufugaji na matokeo yake tatizo la ajira litaendelea kuwa kubwa nchini.
UNYWAJI WA VILEO MUDA WA KAZI.
Mh. Ndaisaba George Ruhoro amesema kuwa, jamii nyingi za kitanzania bado zinakunywa pombe mda wa kazi. Wanaume wanaanza kulewa kuanzia saa tatu hadi saa nne za asubuhi hasa maeneo ambapo pombe kama vile ULANZI zinapatikana kirahisi.
Unywaji wa pombe mida ya kazi unasababisha kupotea kwa nguvu kazi ya Taifa na huathiri Afya za watanzania.
Mh. Ndaisaba George Ruhoro, ameishauri serikali kuhakikisha unywaji wa pombe muda wa kazi unapigwa marufuku na mamlaka za serikali zinasimamia vizuri eneo hili.
Vile vile Mh. Ndaisaba George Ruhoro amesema kuwa, kasi ya serikali imewaacha wananchi nyuma. Wakati serikali inalenga kukuza uchumi kwa 8% na ukuwaji huu ukiwa unawahitaji wananchi kufanya kazi kama nyuki, na kwa bidii kubwa, wananchi wengi wameridhika na hali zao. Hawana haraka ya kuzalisha. Kaya yenye ekari 2 za shamba, mbuzi 9 na ngombe mmoja unakuta imeridhika kabisa. Kiu ya kufanya kazi kwa Bidii haipo.
Hivyo, Serikali ihakikishe mpango ujao unaweka utaratibu wa kuhamasisha wananchi kuongeza kasi ya uzalishaji, muda wa kazi uongezeke, ukubwa wa mashamba yao uongezwe, serikali iwawezeshe kupata mbegu na pembejeo za kilimo ila ihakikishe inawasimamia wananchi ili wachape kazi kwa bidii ili kufikia malengo ya kuongeza uzalishaji katika kilimo.
Recent Comments