Serikali kupitia wizara ya Maji imetiliana saini mkataba wa ujenzi wa mradi wa maji kutoka ziwa victoria kwenda katika mikoa ya Shinyanga na Singida utakaogharimu shilingi bilioni 24.4 na kampuni ya Megha engineering ya nchini India.
Hafla ya utilianaji saini umefanyika katika mji mdogo wa Tinde ambapo serikali imewakilishwa na katibu mkuu wa wizara hiyo,mhandisi Athony Sanga huku kampuni ya Megha ikiwakilishwa na Meneja mkuu kampuni hiyo ya ujenzi Moral Mahan, mradi utakaotumia mwaka mmoja hadi kukamilika kwake.
Akizungumza na wakazi wa Tinde,Waziri wa Maji Jumaa Aweso ambaye alikuwa mgeni rasmi katika hafla hiyo alisema kuwa mradi huo utatekelezwa katika miji ya Shelui mkoani Singida na Tinde Shinyanga ili kutatua kero za maji kwa wananchi zaidi ya laki moja kwa wilaya hizo.
Alisema kuwa wizara ya maji itahakikisha inawasimamia wakandarasi hao kwa ukaribu huku akitoa onyo kali kwa watakaobainika kukwamisha mradi huo kwa makusudi licha ya serikali kutoa fedha za ujenzi wa mradi huo.
“Tumekuja kutekeleza ahadi ya Rais Dkt. John Pombe Magufuli aliyoitoa mwezi januari 29 mwaka huu kwa kuagiza wakazi wa miji ya Tinde na Shelui kupatiwa huduma ya maji safi na salama,”alisema Aweso.
Sambamba na hilo Aweso amewataka wakazi wa mikoa ya Shinyanga na Singida kuulinda mradi huo ili uweze kuleta tija kwa wananchi ambao wanatumia muda mwingi kwaajili ya kutafuta huduma ya Maji.
Nae mkuu wa mkoa wa Shinyanga Zainabu Telack amemuomba Waziri Aweso kuhakikisha wafanyakazi watakaotekeleza mradi huo wawe wametoka katika miji hiyo midogo ili kutoa fursa za kiuchumi kwa wananchi waofikiwa ‘na mradi huo.
“Sisi tuko tayari kuwapa ushirikiano wa kila aina wakandarasi watakaotekeleza mradi huu,tunaiomba wizara iuone mkoa wetu kama mfano katika utekelezaji wa miradi ya maji,”alisema Telack.
Mradi huu ni miongoni mwa miradi 28 inayotekelezwa kwa ubia kati ya serikali ya  Tanzania na India,katika mikoa mbalimbali ya Tanzania bara na Visiwani kwa gharama ya dola za kimarekani 500.
Recent Comments