JAMII nchini imetakiwa kujenga utamaduni wa kutunza mazingira hasa ya fukwe, ili kulinda uhai wa viumbe vinavyoishi humo, pia kudumisha uhalisia wake.
Wito huo umetolewa hivi karibuni na Katibu Tawala Wilaya ya Kinondoni, Sofia Msofe, wakati wa tukio la usafishaji fukwe ya Kawe lililoratibiwa na FORUMCC kwa kushirikiana na Umoja wa Ulaya (EU).
Amebainisha kuwa tukio hilo ni mfano kwa jamii nyingine, hivyo zinapaswa Kujenga utamaduni wa kusafisha fukwe kwa maslahi ya viumbe hai na ulinzi wa uhalisia.
“Tunawashukuru FORUMCC na Umoja wa Ulaya kwa uamuzi wa kuja kufanya usafi na hii itatuamsha wananchi kuwa na utamaduni wa kufanya usafi,” amesema.
Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi wa FORUMCC, Sarah Ngoy, amesema wamekuwa na utaratibu huo ili kuikumbusha na kuielimisha jamii juu ya umuhimu wa utunzaji mazingira.
Ameeleza kuwa tukio hilo pamoja na mambo mengine limelenga kuyafikia makundi mbalimbali na kuzungumza nayo yaone umuhimu wa kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.
“Wote ni mashahidi tumeshuhudia athari kadhaa zikiwemo kuongezeka kwa kina cha Bahari, kasi ya upepo, kuongezeka kwa maji chumvi maeneo ya maji baridi, hizi zote ni athari za mabadiliko ya tabianchi hivyo kuna haja ya kuchukua hatua,” amesema.
Mwakilishi wa Balozi wa Ireland nchini, Mary O’Niel, taifa lake linatambua na kuthamini uhifadhi wa mazingira, ndiyo maana imekuwa rahisi kushirikiana na FORUMCC katika tukio hilo.
Amesema jukumu la kutunza mazingira linapaswa kurithishwa kwa vizazi mbalimbali ili kila anayekuja akute uhalisia.
Amesisitiza haja ya kubalidi mitazamo kuwa jukumu la utunzaji wa mazingira linalihusu kundi fulani, badala yake limuhusu kila mmoja.
“Nakumbuka zamani nikiwa na baba yangu tukisafiri kwa gari, tulikuwa tunafungua madirisha ya gari na kutupa uchafu nje lakini kwa sasa haiwezekani kwasababu mtazamo umebadilika,” amesema.
Ameongeza kuwa nchi yake kupitia mpango kazi uliopo katika kutunza mazingira, itaendelea kushirikiana na serikali ya Tanzania kufanikisha Uhifadhi.
Naye Mwakilishi wa Balozi wa EU, C’edric Merel, amesisitiza umuhimu wa utunzaji mazingira na kueleza kuwa jumuiya hiyo ina mpango wa miaka saba na mabadiliko ya tabianchi ni moja yanvipaumbele.
Amesema kupitia mpango huo, jamii itafanya kazi kwa pamoja ili kushirikiana kutunza mazingira.
Ametaja jamii isiwe sehemu ya wachafuaji wa mazingira na badala yake ijikite katika kuyasafisha ili kurejesha uhalisia
Muta Rwakatare ni Diwani wa Kata ya Kawe, jijini Dar es Salaam, amesema kutokana na tukio hilo, wananchi wanapaswa kuendelea kufanya usafi katika maeneo yao.
Amesema suala la usafi wa mazingira liwe tabia ya jamii ambapo wakati wote wahakikishe wanakuwa katika mazingira Safi na salama.
Recent Comments