Sawa, sherehe za miaka 46 ya Chama Cha Mapinduzi zimepita vizuri, ila zina kipi tunachoweza kujitambia: umeme, nyumba za kisasa zenye maji na vyoo ndani?
Hizi ni salaamu za upendo kwenu www.simamia.com. Mtandao makini usio na upendeleo sala kujikomba komba kwa walevi na wenye uchu wa madaraka walio tayari kujitangaza kama watawala ambao sisi wana Ngara tunaona kama Wakoloni weusio waliopokea kutoka kwa mzungu.
Mimi naitwa Ndikumudyango Ngendavyanka Bhakavuga. Ni mfuatiliaji wa karibu wa vipindi vyenu na nafurahia sana kusoma makala zenu simamia.com. Ingawa muda mwingine naonaga story hazijanyooka – labda kutokana na timu yenu kuwa ndogo huku vijijini, nashukuru sana kwa kudondosha makombora moja kwa moja kwa walengwa maana huku wengine tunaweza kujikuta pabaya zaidi. Ni ukweli mchungu ambao ni funzo, hasa kwa wale wanaguswa ama ukweli unatishia ugali wao. Muda mwingine ni bora ujinga uliotuletea huu umasikini uendelee ili mradi uhakika wa ugali uwepo maana watu hatuna jinsi.
Jana nilikua kwenye maadhimisho ya miaka 46 ya Chama Cha Mapinduzi hapa Ngara. Niliangaza angaza macho nikitegemea kuona labda kati ya wale watu 20 walioandikwa na gazeti hili kuwa wanauonekano onekano kupokea kijiti cha uongozi wa ubunge, jimbo la Ngara, wanashiriki kikamilifu kwenye hii sherehe ya kusherekea nusu karne ambapo Chama Cha Mapinduzi, CCM, kimeweza kuongoza nchi hii. Nilitegemea angalau maendeleo yaliyozalishwa na uongozi wa hiki chama kinara kwenye siasa nchini Tanzania. Wachache walihudhuria na baadhi yao walitoa risara nzuri ingawa ni risara zile zile zilizotolewa mara nyingi tuu hapo awali.
Natumaini mnawasiliana na watu wengi na mnasikia na kuona mengi yanayoendelea hapa Ngara na kwingineko duniani mlipo. Pia, natumaini mtakua mmeshapokea simu kutoka kwa wale mliowaorodhesha kama wanaweza kushiriki katika kinyang’anyiro cha kiti cha ubunge wa jimbo la Ngara mwaka 2025.
Kutokana na ile makara, labda mlisahau kuorodhesha wengineo. Ama kuna watu ambao mnaona hawatoweza kupita kwenye mchujo wa kwanza, kama kweli hata watashiriki kutetea haki yao ya kuongozo wilaya yetu ya Ngara. Mnaweza kutupatia 10 bora na pengine 5 bora hapo mbeleni ya wataoweza kugombea na kushinda uchaguzi wa ubunge, jimbo la Ngara mwaka 2025?
Kama mkazi wa Ngara, mimi na kama vijana wengi tuu, natumia nguvu zangu kuishi na kutimiza mahitaji ya familia yangu. Sijikombi kombi kwa viongozi na vijana wengi hapa, sisi ni walipa kodi za kila aina. Kwa hiyo, ninatoa mchango wangu wa kulijenga taifa langu kupita shughuli mbali mbali hususani biashara ya boda boda. Nategemea viongozi wa Ngara na wa nchi nzima watambue michango vijana tunayoiletea taifa letu. Nategemea mbunge wa Jimbo la Ngara alitambue hili na hata yule atakayempokea kijiti cha uongozi mwaka 2025 alitambue michango ya wananchi. Pia viongozi watambue kuwa kutoa huduma bora kwa wananchi wote katika jimbo lake ni wajibu wa serikali. Viongozi wasitegemei wale wanaomenyeka mitaani na shughuli zao na kulipa kodi ndio waje kupiga magoti ili wapatiwe huduma ambazo zinagharamiwa na shuru tunazotozwa. Leo katika jimbo la Ngara, ingawa tumeadhimisha miaka 46 ya Chama Cha Mapinduzi, na amini ungebahatika kutembelea nyumba 20-20 kila kata na kuuliza ni lini walifaidika na uwepo wa umeme kwa siku 25 mfurulizo, na ni siku ngapi mfururizo mabomba yalitoa maji majumbani kwao, hapo ungepata picha halisi ya uwezo wa wale wanaoitwa viongozi katika jimbo la Ngara. Wanaonekana kupendeza katika sare za vyama vyao ila ukilinganisha yale yanayotoka mimdomoni mwao na uhalisia unaoonekana katika kaya tofauti tofauti utajua ukweli na uhalisia ulipo. Hata wale wanaoonekana kuwa ni matajiri hapa wilayani Ngara bado maji ni changamoto. Kwa swala la umeme, ni afadhari Tanesco wasingesimamisha nguzo za umeme kila sehemu na kutuacha tuendelee kutumia vibatari na mishumaa. Hizi nguzo za umeme ni vituo vya ndege wanavyotumia kusambaza mbolea ama kujisaidia.
Mimi kama mkazi wa Ngara, muda mwingine naona kama tunaishi kama matwekwa kwenye nchi yetu. Iweje mgombea atupigie magoti akiwa anataka kura zetu. Akishashinda na kuwa kiongozi inakua zamu yetu kuwapigia magoti ili kupata huduma zinazonunuliwa kupita kodi tunazolipa? Na mito yote iliyopo wilani Ngara, ni chini ya asilimia 1% ya wanakazi wa Ngara wana maji majumbani kwao. Sasa hatujui kama tuna viongozi ama wasimamizi na kama ni viongozi wanaongoza nini maana hatujaona maendeleo yoyote. Kama ni viranja, wanasimamia mapato yanayokusanywa hapa kwetu na kuperekwa ambapo kuna viongozi maana viongozi ndio watapasua mbao kwenye miti inayotolewa misituni ili nyumba zijengwe. Kwa sasa ngoja nikachaji simu yangu ili nikirudi kuchungulia hili gazeti, labda utakuwa umechuja 10 bora ya wale waoonekana kutingisha ulingo wa kinyang’anyiro cha ubunge wa jimbo la Ngara, mwaka 2025. Ila wajue kabisa, Ngara inakiu cha kupata kiongozi na sio kiranja. Tunajua tupo msituni, na ingawa wanachuma miti, hata sisi ni binadamu, tunahiji nyumba nzuri za kisasa na zenye maji na vyoo vya kuvuta.
Recent Comments