‘ALAJI’ JELA MIAKA 90 KWA KOSA LA KUBAKA WATOTO WATATU.
Na Musa Mathias Njogolo.
Email. Mussamathias573@gmail.com musamathiasnjogolo@gmail.com
Morogoro.
Mahakama ya Wilaya ya Kilombero imemuhukumu Leonce Athanas Matea maarufu kwa jina la Alaji (55), Mkulima na Mkazi wa Chicago A’ Kata ya Kidatu Wilaya ya Kilombero Mkoani Morogoro kifungo cha miaka 90 Jela kwa mashtaka matatu ya kubaka watoto watatu.
Hukumu hiyo ilitolewa Mei 27, 2024 mahakamani hapo na Hakimu Bestina Saning’o, Mkaguzi wa Polisi Thomas Kamsini alieleza mahakama kuwa adhabu kali itolewe kwa mshitakiwa huyo ili iwe fundisho kwa watu wengine wenye tabia kama hizo za kubaka watoto wadogo.
Upande wa mshitakiwa Leonce Athanas Matea maarufu kama Alaji aliiomba mahakama kumpunguzia adhabu kwani umri wake umeenda na mara baada ya pande zote mbili kutoa maombi yao Hakimu Saning’o alimtia hatia mshitakiwa huyo kwa kumfunga kifungo cha miaka 30 kwa kila kosa alilokuwa anashitakiwa nalo.
Hakimu Saning’o aliendelea kusema kuwa ili iwe fundisho mahakama imemtia Hatiani katika mashitaka yote matatu ya kubaka na kila shitaka ataenda jela miaka 30 ambapo adhabu hizo zinaenda sambamba na baada ya Hakimu Saning’o kusoma hukumu hiyo mtuhumiwa alichukuliwa na kupelekwa katika gereza la kiberege.
Novemba 24, 2023 mshitakiwa huyo alifikishwa mahakamani hapo na kusomewa mashitaka matatu ya kubaka ambapo shitaka la kwanza alidaiwa kufanya kati ya Juni 01,2023 na Novemba 16,2023 huko kijiji cha Chikago Kata ya Kidatu Wilaya ya kilombero mkoa wa Morogoro alimbaka mtoto wa miaka tisa jina lake limehifadhiwa.
Katika shitaka la pili tarehe hizo hizo sehemu hiyohiyo alimbaka mtoto wa miaka kumi jina lake limehifadhiwa, na shitaka la tatu alidaiwa kulifanya kati ya Novemba 01, 2024 hadi Novemba 16,2023 alimbaka mtoto wa miaka mitano jina lake limehifadhiwa na mara baada ya kusomewa mashitaka hayo alikana kutenda makosa hayo mahakamani hapo.
Upande wa Jamhuri ulileta mashahidi 12 wakiwemo na wahanga katika shauri hilo ambapo katika ushahidi wao ilionekana kuwa mshitakiwa huyo alikuwa akiwarubuni watoto hao wa miaka 5, 9 na 10 kwa kuwaita ndani ya Nyumba yake na kuwafanyia kitendo hicho kwa zamu kisha kuwapa Tsh 200 kila mmoja.
Mwisho.
Recent Comments