Recent Comments

WAKAZI ZAIDI YA 4,000 WA VIJIJI VIWILI WILAYANI SAME KUONDOKANA NA ADHA YA UKOSEFU WA MAJI. 

By Mussa Mathias Jun 1, 2024

WAKAZI ZAIDI YA 4,000 WA VIJIJI VIWILI WILAYANI SAME KUONDOKANA NA ADHA YA UKOSEFU WA MAJI.

Na Musa Mathias Njogolo.

Email. mussamathias573@gmail.com musamathiasnjogolo@gmail.com

 

 

Zaidi ya wakazi elfu nne hamsini na mbili (4052) pamoja na taasisi tano wa vijiji vya Msindo na Mbakweni Wilayani Same wapo mbioni kuondokana na adha ya upatikanaji wa huduma ya maji safi na salama baada ya Serikali kutoa kiasi cha shilingi bilioni 1.05 kwaajili ya utekelezaji wa mradi mkubwa.

 

Mradi huo unatekelezwa na Mkandarasi BUILD TECH ENGINNERINGI COMPANY LIMITED ambaye anatakiwa kuanza utekelezaji wake June 14, 2024 na kukamilisha ndani ya siku 365 yaani mwaka mmoja kwa kufanya kazi ya kuchimba mitaro na kulaza bomba umbali wa kilometa 21.3 na kukarabati dakio la maji.

 

Akizungumza mara baada ya kushuhudia utiaji saini wa mkataba huo ulioshuhudiwa na wananchi wa eneo hilo, Mkuu wa Wilaya ya Same Mhe. Kasilda Mgeni amemtaka mkandarasi kuhakikisha kunakuwa na uwazi wakati wa utekelezaji wa mradi kabla ya kuanza lazima ashirikiane na viongozi wa Serikali wa vijiji husika ili wananchi waufahamu mradi wao vizuri lakini pia mradi utekelezwe kwa mujibu wa mkataba unavyomtaka.

 

“Nimshukuru Mhe, Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa juhudi ambazo amekuwa akizifanya kupitia Wizara ya maji kuhakikisha kero za wakazi wa Same zinapatiwa ufumbuzi kwa wakati lakini pia nimpongeze Mhe. Jumaa Aweso Waziri wa maji kwa kutafsiri vyema maono ya Rais wetu ya kumtua mama ndoo kichwani”.Alisema DC Kasilda.

 

Kwaupande wake Katibu wa Chama cha Mapinduzi CCM Wilaya ya Same Amos Kusakula amemsisitiza mkandarasi huyo kuhakikisha anakamilisha mradi kwa wakati na kutekeleza kwa viwango vilivyoainishwa kwenye mkataba ili wananchi waweze kunufaika na fedha zilizotolewa na Serikali ziweze kutekeleza malengo.

 

Naye Diwani wa Kata ya Msindo ambaye pia ni Mwenyekiti wa Halmashauri ya Same Yusto Mapande amewasisi wananchi kuwa mradi utakapo kamilika wanapaswa kujiunga katika jumuiya za watumiaji maji ili waweze kuchangia huduma hiyo kiasi kidogo cha fedha kusaidia kuboresha miundombinu pamoja na uendeshaji wake.

 

Mwisho.