MGOMBEA urais wa Chadema anayeungwa mkono na vyama vingine vitatu vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), Edward Lowassa amewapa pole wanachama wa Chama cha Wananchi (CUF) kwa mshituko wa kuondokewa na Mwenyekiti wao wa Taifa, Profesa Ibrahim Lipumba aliyejiuzulu, huku akiwataka kutovunjika moyo, bali waongeze mshikamano ili dhamira ya kuingia Ikulu iweze kutimia.
Aidha, Mwenyekiti wa Chadema Taifa, Freeman Mbowe ameonya kuwa, hawatamvumilia yeyote atakayeonekana kutaka kukwamisha umoja wao unaoundwa na vyama vya Chadema, CUF, NCCR-Mageuzi na NLD.
Akizungumza na wananchi waliofika kumpokea alipotembelea ofisi za CUF Buguruni, Dar es Salaam jana ambako pia alihudhuria kikao cha Baraza Kuu la CUF, Lowassa aliwapa pole wanaCUF akisema endapo watatetereka, safari yao ya kuelekea Ikulu itakuwa ngumu.
Alitumia fursa hiyo kuwaomba wafuasi wa CUF kumsindikiza kwa wingi leo kwenda ofisi za Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kuchukua fomu ya kuwania urais baadaye mwaka huu, huku akisisitiza ana imani ya kushinda.
Awali, mgombea mwenza wa Lowassa, Juma Duni Haji ambaye alijiunga Chadema hivi karibuni akitokea CUF alikokuwa Makamu wa Mwenyekiti wa Taifa, alisema endapo wanachama wa vyama vinavyounda Ukawa watakosea katika kupiga kura zao na kushindwa kuingia madarakani, basi watalazimika kusubiri miaka 50 ijayo ili kuingia Ikulu.
âTusipoweza kuingia Ikulu sasa litakuwa kosa kubwa na itatulazimu kusubiri miaka 50 ijayo ili kuweza kuchukua madaraka. Vijana pekee ndio watakaoweza kuleta mabadiliko,â alisema Duni.
Akizungumzia shughuli ya kuchukua fomu leo, Lowassa aliwataka wanachama wa chama hicho kujitokeza kwa wingi kumsindikiza na kusisitiza kuwa amejiunga na Ukawa ili kutafuta mabadiliko nje ya CCM na kuwa ana imani ya kushinda kwa asilimia 90.
Lowassa alisema endapo Ukawa itashinda na kuchukua madaraka wataendesha nchi kwa utulivu na kubadilisha maisha ya Watanzania kwa kuwaondolea umasikini ambao umekuwa ukipigwa vita tangu mwaka 1962. Naye Mwenyekiti wa Chadema Taifa, Freeman Mbowe alisema kiongozi ndani ya Ukawa ambaye atakuwa akipingana na malengo yao kutokana na kukosa fursa binafsi, mtu huyo hafai kuwa katika umoja huo.
Alisema pamoja na umoja huo kukumbwa na misukosuko, bado wamekuwa wamoja na kutetea hatua ya wao kumteua Lowassa ambaye wiki mbili zilizopita alikuwa CCM kwa sababu ni Mtanzania. Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad alisema silaha pekee ya ushindi kwa Ukawa ni kuwa na umoja, ushirikiano na mshikamano na kuwa ana uhakika Lowassa atashinda, sambamba na yeye kwa upande wa Zanzibar.
âLowassa ni rais anayesubiriwa kuapishwa, na Zanzibar kuna mtu anaitwa Maalim Seif ameshamaliza kazi naye anasubiri kuapishwa,â alisema na kuongeza kuwa amefarijika kwa Lowassa kutembelea CUF, jambo ambalo linadhihirisha umoja wao.
Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi Taifa, James Mbatia alisema Ukawa haitahubiri siasa za chuki ili uchaguzi ufanyike kwa amani na kuwaonya viongozi wa CCM kuchunga ndimi zao. Kwa upande wa Mwenyekiti wa Taifa wa Chama cha NLD, Dk Emmanuel Makaidi alisema watakaoiondoa CCM madarakani ni wananchi wenyewe kwa kujitokeza kupiga kura.
Lowassa leo atachukua fomu ya uteuzi wa urais katika ofisi za Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), akiambatana na mgombea mwenza Duni. Msafara wa kumsindikiza Lowassa, utaanzia Makao Makuu ya CUF, Buguruni asubuhi saa 2:00 na kupitia Makao Makuu ya NCCRMageuzi na baadaye kwenda NEC ambapo saa 5:00 asubuhi mgombea huyo atachukua fomu.
Baada ya kuchukua fomu, Lowassa ambaye alijiuzulu uwaziri mkuu kwa kashfa ya kuiingiza Serikali katika mkataba wa kufua umeme wa kampuni feki ya Richmond na baadaye kuchujwa katika kinyangâanyiro cha kuwania urais kupitia CCM, atakwenda Makao Makuu ya Chadema, Kinondoni.
Wakati huohuo, Emmanuel Ghula anaripoti kuwa Chama cha Wananchi (CUF) kimechagua kamati ya watu watatu ambao watafanya kazi zilizokuwa zikifanywa na Mwenyekiti wa chama hicho aliyejiuzulu, Profesa Ibrahim Lipumba pamoja na makamu wake, Juma Duni Haji.
Walioteuliwa ni Twaha Taslima ambaye atakuwa mwenyekiti wa kamati, Abubakar Khamis na Severina Mwijage. Kuundwa kwa kamati hiyo kunatokana na kujiuzulu kwa aliyekuwa mwenyekiti wa chama hicho, Profesa Lipumba huku makamu mwenyekiti wake kujiunga na Chadema kama mgombea mwenza wa urais kupitia Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa).
Akitangaza uamuzi wa baraza kuu la uongozi wa taifa wa chama hicho, Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad alisema kuwa chama hakiwezi kukaa kwa kipindi cha miezi sita bila kuwa na mwenyekiti wala makamu wake, wameamua kuteua kamati ya watu watatu kama ambavyo katiba yao inawataka.
âKwa mujibu wa katiba ya chama chetu, hatuwezi kuteua mwenyekiti wala makamu wake hadi kipindi cha miezi sita na badala yake katiba inaturuhusu kuteua kamati ya watu watatu watakaofanya kazi ambazo zilikuwa zinafanywa na viongozi hao wa juu,â alisema Maalim Seif.
Recent Comments