MGOMBEA urais kwa tiketi ya Chadema anayeungwa mkono na vyama vingine vitatu vya upinzani vinavyounda umoja unaofahamika kwa jina la Ukawa, Edward Lowassa jana alichukua fomu za kuwania rasmi nafasi hiyo kutoka Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC).
Lowassa, Waziri Mkuu wa zamani aliyejiunga Chadema hivi karibuni baada ya kushindwa katika mchakato wa kumpata mgombea urais kwa tiketi ya CCM, sasa ameungana na wagombea wengine kujitokeza NEC kuchukua fomu za kuwania urais.
Ametanguliwa na mgombea wa CCM, Dk John Magufuli ambaye pia ni Waziri wa Ujenzi na Mwenyekiti wa UPDP, Fahmi Dovutwa. Wengine ni Mchungaji Christopher Mtikila wa DP, Mac-Millan Lyimo wa TLP, Hashim Rungwe wa CHAUMMA, Chifu Lutasola Yemba wa ADC na Dk Godfrey Malisa wa CCK.
Lowassa alianza msafara wake saa tano asubuhi akitokea ofisi za Chama cha Wananchi (CUF), Buguruni alikuwa kwenye msafara mrefu huku akisindikizwa na mamia ya wafuasi wa vyama hivyo na kupita barabara ya Uhuru, na baadaye Bibi Titi na kuja hadi Ohio.
Akiwa kwenye gari aina ya Toyota Land Cruiser lenye namba T 878 CFU alifika ofisi za NEC zilizopo makutano ya mitaa ya Ghana na Ohio, katikati ya Jiji la Dar es Salaam, majira ya saa 7:30 mchana akiambatana na mgombea mwenza Juma Duni Haji, Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad, Mwenyekiti wa Chadema-Taifa, Freeman Mbowe, Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi James Mbatia, Mwenyekiti wa NLD, Dk Emmanuel Makaidi.
Pia walikuwapo baadhi ya wabunge wa vyama vya Chadema, Cuf na NCCR-Mageuzi na viongozi wa juu wa vyama hivyo. Baada ya kuchukua fomu na kuonesha wananchi, Lowassa alianza safari ya kuelekea Kinondoni kwenye ofisi za makao makuu ya Chadema kwa gari huku akisindikizwa na maelfu ya wafuasi vya vyama hivyo waliokuwa wanatembea kwa miguu kutoka ofisi za NEC.
Kutokana na umati wa watu uliofurika katika ofisi za Chadema, Lowassa na msafara wake walilazimika kutumia uwanja wa Biafra kwa ajili ya kuwaaga wafuasi waliotembea kwa miguu kumsindikiza.
Akizungumza akiwa kwenye ofisi za Chadema, Lowassa mbali na kuwashukuru wafuasi wao kwa kujitokeza alisema agenda yake ya kwanza akiingia Ikulu ni kuondoa umasikini kwa makundi yote.
Alisema asilimia 72 ya wapiga kura katika uchaguzi wa mwaka huu, ni vijana hivyo anawaahidi kushughulikia matatizo yao kupitia ilani ya Chadema ambayo inatarajia kutolewa muda si mrefu.
âNikiingia Ikulu nachukua dhamana ya kushughulikia matatizo ya vijana, nitaunda serikali ambayo ni rafiki kwa mama ntilie na waendesha bodaboda. Tutakuza uchumi kwa kasi kubwa,â alisema.
Recent Comments