Mwanza. Mgombea urais kwa tiketi ya Chadema, Edward Lowassa amesema anawatakia kila la heri wanaobeza nguvu ya umma.
Kutokana na umati wa watu waliojitokeza jana kumlaki kuanzia Uwanja wa Ndege wa Mwanza alikowasili saa saba mchana, iliuchukua zaidi ya saa mbili msafara wake kuingia Viwanja vya Furahisha saa tisa alasiri, ambako ni takriban kilomita nane.
Katika hotuba yake iliyochukua dakika 14 kuanzia saa 11.53 hadi 12.07 jioni, Lowassa alisema anawasikitikia wanaobeza nguvu hiyo ya umma.
âHaya siyo mapenzi, haya ni mahaba. Wanaobeza nguvu hii ya umma nawatakia kila la heri,â alisema Lowassa huku akishangiliwa na umati huo.
Akizungumzia idadi hiyo ya wananchi, mke wa mgombea huyo, Regina Lowassa alisema haijawahi kutokea maeneo yote waliyotembelea Dar es Salaam, Mbeya na Arusha.
âMwanza nimewapenda, nafikiri baba (Lowassa) akitoka hapa atalala usingizi mzuri mzito,â alisema Regina.
Lowassa aliwataka polisi kutoingilia mchakato wa uchaguzi na kutumiwa na CCM kupambana na wapinzani na kwamba, wakiendelea watakuwa wanajitafutia tiketi ya kupelekwa Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC), mjini The Hegue.
âNimesikitishwa sana kuwa watu wamepigwa mabomu asubuhi. Mkiendelea na mchezo huu tukimaliza uchaguzi tutawapeleka The Hague mkakipate cha mtoto na huko hamtarudi tena,â alisema.
Mabomu yarindima
Polisi mkoani hapa jana walilazimika kutumia mabomu ya machozi, kuwatawanya wafuasi wa vyama vinavyounda Ukawa ambao walifurika Uwanja vya Ndege wa Mwanza kumpokea Lowassa.
Lowassa aliwasili akiwa ameambatana na mgombea mwenza, Juma Duni Haji, Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe na Mwenyekiti wa NCCR Mageuzi, James Mbatia, Kaimu Mwenyekiti wa CUF, Twaha Taslima na Mwenyekiti wa NLD, Dk Emmanuel Makaidi.
Mabomu ya machozi yalianza kurindima saa tano asubuhi, baada ya baadhi ya wafuasi wa Ukawa kutaka kuingia kwenye lango la uwanja wa ndege, huku wengine wakijaribu kuwatunishia misuli polisi kwa kuwatupia mawe.
Hekaheka za mapokezi ya Lowassa zilianza saa mbili asubuhi, baada ya maelfu ya wafuasi wa Ukawa wakiwa na mabango yenye ujumbe mbalimbali ikiwamo: âOil chafu ni kiboko ya mchwaâ kutanda kwenye barabara inayoelekea uwanja wa ndege.
Magari ya polisi aina ya Land Rover Defender na Landcruiser yapatayo matano yalitanda kwenye barabara ya uwanja wa ndege, huku yakizuia magari kuingia uwanjani.
Kabla ya muda wa mkutano wa mgombea huyo wa urais kuanza kwenye Viwanja vya Furahisha, uwanja ulianza kujaa maelfu ya wakazi wa Mwanza kuanzia saa tatu asubuhi.
Msafara wa Lowassa kutoka uwanja vya ndege uliongozwa na pikipiki ambazo zilikuwa zinapeperusha bendera za vyama vya CUF, Chadema ,NCCR Mageuzi na NLD, huku viongozi hao wakiwa kwenye magari ya wazi.
Ampa Wenje kibarua
Lowassa alisema ziara yake hiyo inahusu kujitambulisha na asingependa kuwapa nafasi wapinzani wake kumtafsiri kuwa hajui sheria, lakini kero za Mwanza anazifahamu hivyo akaahidi kurejea na mikakati ya kuzitatua.
Alisema anafahamu Wamachinga, meli ya Mv Victoria, kiwanda kikubwa cha kusindika nyama, reli, ujenzi wa uwanja mkubwa wa ndege, bei ndogo ya pamba na tatizo la umeme.
Kuhusu suala la umeme, Lowassa alisema Mbunge wa Nyamagana, Ezekia Wenje ni kijana anayefanya uamuzi mgumu kama yeye hivyo alimtaka leo kwenda kwa Meneja wa Tanesco Mwanza ili kujua tatizo, asipopewa majibu ya kuridhisha ampigie simu yeye (Lowassa).
Masha aahidi ushindi
Aliyewahi kuwa Waziri wa Mambo ya Ndani na Mbunge wa Nyamagana, Lawrence Masha alisema: âNdugu zangu nimerudi nyumbani, naomba niwaambie Watanzania wote kwa ujumla hapa tulipo tupo kwenye harakati za kuikomboa nchi yetu.
Leo nasimama hapa kama mwana Mwanza, lengo ni kuhakikisha tunapambana na kuikomboa Tanzania, naomba Oktoba 25 tufanye kazi moja tu ya kuchagua viongozi wa Ukawa.â
Masha kwa mara ya kwanza aliahidi kumsaidia Wenje kwenye kampeni na kueleza kuwa, atakuwa bega kwa bega na Wenje, jambo ambalo lilisababisha umati kulipuka kwa nderemo.
Mgeja: Makapi yanafua umeme
Aliyekuwa Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Shinyanga, Hamis Mgeja alisema alipotangaza kuhama CCM alipigiwa zaidi ya simu 800 za kumpongeza na sita za kumlaumu, lakini amejifunza kuwa alikuwa kwenye nyumba inayoteketea.
âWanasema makapi, hivi hawajui kuwa hivi sasa makapi ndiyo mali, yanafua umeme,â alisema na kuongeza: âWanamlinganisha Lowassa na mgombea wao (bila kumtaja), wanamdhalilisha Lowassa huyo siyo saizi yake.â
Recent Comments