CHAMA Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimeibua tuhuma mpya dhidi ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), kikisema kimebaini shahada zaidi ya milioni mbili za kupigia kura zinazotarajiwa kuingizwa kinyemela katika Daftari la Wapiga Kura na kugawiwa kwa wana CCM ambao hawakujiandikisha.
Chama hicho kimedai kwamba, mbali na shahada hizo pia wakimbizi zaidi ya 70,000 mkoani Kigoma wameandikishwa katika daftari hilo kwa ajili ya kupiga kura.
Tuhuma hizo zilitolewa jijini Dar es Salaam jana mbela ya waandishi wa habari na Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake wa Chadema (Bawacha), Halima Mdee na kada wa chama hicho, Saed Kubenea.
Akizungumza katika mkutano huo, Kubenea aliwaonyesha takribani shahada 100 alizosema ndizo zitakazoingizwa kwenye dafatari hilo kinyume cha taratibu.
Shahada hizo hazina jina la mpiga kura, picha, tarehe ya kuzaliwa, sehemu na eneo alilojiandikisha pamoja na taarifa nyingine muhumu zinazowekwa kwenye shahada halali.
âChadema tumebaini kuwepo kwa mpango wa kuingizwa kwa shahada za kupigia kura zaidi ya milioni mbili, ambazo zinatarajiwa kutumiwa na wana CCM ambao walikuwa hawakujiandikisha katika daftari la kupigia kura,â alisema Kubenea.
âInawezekana kabisa NEC kwa kushirikiana na CCM wamepanga kuingiza majina yao katika shahada hizi, na ndiyo maana hata kuna baadhi ya watu walikamatwa wakiwa na mashine nyumbani kwa watu,â alisema.
Kubenea alisema vitambulisho hivyo vimetengenezwa ili kuongeza kura za CCM kwa wanachama wake ambao hawakupata nafasi ya kujiandikisha.
âWizi wa kura hapa nchini unaanzia kwenye utangazaji wa idadi ya wapiga kura waliojiandisha, kwa mfano wananchi waliojiandikisha milioni 23 kwenye taifa lenye wakazi wanaokadiriwa kuwa milioni 45, huo ndio wizi wenyewe kwa sababu wakati wa sensa waislamu wengi waligomea kuandikishwa.
âNchi yenye idadi hiyo ya watu haiwezi kuwa na wapiga kura milioni 23, kwa mujibu wa takwimu za Tume ya Takwimu ya Taifa wanasema asilimia 60 ya Watanzania wako chini ya miaka 18, hivyo ukichukua nusu ya Watanzania milioni 45 itakuwa ni milioni 22.5 kama wote wangeingia kwenye sensa hivyo kwa tathmini hiyo nyongeza hiyo ni wizi,â alisema.
Kubenea alitoa wito kwa NEC kufanyakazi kwa uaminifu na uadilifu ili kuondokana na mipango ya kuongezwa kwa kura za watu ambao hawakujiandikisha katika daftari la wapiga kura.
Kwa upande wake Halima Mdee alisema kuwa chama hicho kimepata taarifa kutoka kwa wafanyakazi wa Tume wakisema kuwa kuna wakimbizi 70,000 walioandikishwa kutoka mkoani Kigoma.
âKuna wafanyakazi wa tume ambao ni wasamaria wema wametupatia taarifa za ndani zinazosema kuwa katika kuhakikisha ushindi unapatikana wamewaandikishwa wakimbizi 70,000 kutoka mikoa ya kigoma,â alisema.
Mdee alisema kuwa ujanja wa kutafuta kura za kupata bao la mkono imekuwa sababu ya NEC, kuchelewa kufanya uhakiki wa daftari la kupigia kura kwa mkoa wa Dar es Salaam.
âKazi hiyo ya uhakiki kwa upande wa mikoani imefanyika ikiwa na kasoro za majina kutobandikwa kwenye vituo husika, ikiwa imekwenda kinyume na tangazo la awali la Tume lililokuwa likisema kuwa majina lazima yabandikwe kwenye vituo ili wananchi wakahakiki kwenye vituo husika na wasipoona majina yao watoe taarifa,â alisema.
Mdee alisema hadi sasa NEC bado haijashusha vitabu vya kuhakiki majina katika ofisi za kata jambo ambalo linatoa tafsiri kwamba uchaguzi utakuwa tata.
âMbaya zaidi tumeelezwa kwamba kitabu kitaletwa kimoja kwenye ofisi za kata ili wananchi wakahakiki majina yao.
âKwa mfano nina wapigakura 70,000 walioandikishwa kwenye kituo kilichokuwa na kamera zaidi ya 4 na kilitumia siku 14. Je, inawezekanaje kuhakiki daftari kwa mtu mmoja baada ya mwingine kwa siku nne pekee,â alisema Halima.
Kiongozi huyo aliongeza kuwa Chadema haitaki kuamini kwamba NEC inafanyakazi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), ila mwenendo unaoendelea unaweza kutoa tafsiri ya kuwepo kwa mpango wa kukipa chama hicho ushindi.
Akielezea kuhusu mbinu watakazotumia Halima alisema wanawatumia wajumbe wa nyumba kumi wanaopita kila nyumba na kuhakiki wanachama wao.
âInawezekana taarifa hizo za wajumbe wa CCM wanazohakiki wanazipeleka NEC ili wakati wa maboresho waweze kuondoa taarifa za watu ambao si wanaCCM na baadaye kuingizwa wana CCM ambao hawakujiandikisha kwenye daftari hilo,â alisema.
Halima alitoa wito kwa Tume kueleza siku ambayo watatangaza kufanyika kwa uhakiki wa wapiga kura kwa jiji la Dar es salaam na waeleze wananchi kwamba kazi ya kuhakiki majina yao ifanyikie mahali walipojiandikishia.
Recent Comments