UZINDUZI wa kampeni ya mgombea urais kwa tiketi ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Edward Lowassa leo ulishuhudiwa na umma mkubwa wa wananchi huku ukipambwa na kila aina ya vivutio na burudani. Anaandika Sarafina Lidwino ⦠(endelea).
Uzinduzi huo kwenye viwanja vya Jangwani ulitangazwa hewani na vyombo vya habari mbalimbali nchini hasa kuanzia saa 9 mchana ratiba ya viongozi kuhutubia ilipoanza.
Kabla ya hapo, jukwaa lililotengenezwa kisasa likisheheni maspika makubwa yakiwemo yaliyowekwa nje ya eneo la mkutano, kwa ajili ya watu wengi zaidi walioshindwa kufika katikati ya viwanja, kulikuwa na burudani zilizooneshwa na wasanii mbalimbali.
Lowassa ambaye pia anapeperusha bendera ya Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA) aliambatana na viongozi wote wakuu wa vyama vinavyounda umoja huo katika uzinduzi huo.
Baadhi ya wasanii maarufu walioporomosha burudani ni Wanawake Band, Juma Kassimu maarufu Juma Nature na Msaga sumu.
Mbali na burudani za muziki, pia kulikuwa na watu wengi waliokuwa wamebeba mabango yaliyoandikwa ujumbe mzito kwenda kwa Lowassa huku wakizunguka nayo kila kona.
Yapo yaliyoandikwa âMzee ukifika Ikulu tuletee Balali ana pesa zetu nyingiâ na âMalofa katika ubora wetu.â Mingine ni âTutawaonyesha ulofa wetu Oktoba 25.â
Mwandishi wa Mwanahalisi Online aliyefika mapema eneo la viwanja ambavyo awali serikali kupitia Manispaa ya Ilala walikataa visitumiwe na UKAWA, alikuta watu wengi wakiwa wamefika, huku simulizi zikisema baadhi ya watu walilala kutoka jana usiku sambamba na kikosi kilichokuwa kikifunga mitambo ya mawasiliano jukwaani.
Barabara zilianza kufurika maeneo ya Magomeni Mapipa hadi Fire njia panda ya Muhimbili, watu wakionekana kukikimbia huku na kule na wakiimba nyimbo za kuhamasishana na zile zilizolenga kukishutumu Chama cha Mapinduzi (CCM) kwa ufisadi na kushindwa kutimiza ahadi ya âmaisha bora kwa kila Mtanzania.â
Wimbo uliotia fora katika nyingi zilizoimbwa na wana-UKAWA, ni âKama sio juhudi zako Kikwete, Lowassa tungempata wapi?â âSisisi si mnaona? Muziki wa Lowassa kuucheza hamuwezi.â
Katika kufunga mkutano wa uzinduzi wa kampeni, muongozaji wa mkutano, Mkurugenzi wa Bunge wa Chadema, John Mrema, amesema UKAWA wamemaliza mkutano saa 11.55 jioni ili watu wapate kuondoka salama viwanjani, lakini akataka Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) iwahoji kwa barua CCM waliomaliza mkutano wao wa uzinduzi saa 1 usiku.
Recent Comments