MWENYEKITI Mwenza wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA), Dk. Emmanuel Makaidi amesema mpira katika nchi hauwezi kuwa mzuri iwapo siasa za nchi ni mbaya. Anaandika Jabir Idrissa ⦠(endelea).
Dk. Makaidi amesema kwamba maendeleo ya mpira wa miguu ambao ni mchezo unaopendwa zaidi na sehemu kubwa ya Watanzania, unahitaji kukua kupitia siasa nzuri ambazo hujengwa na uongozi wenye watu waadilifu.
Akihutubia mkutano wa uzinduzi wa kampeni ya UKAWA, umoja unaoundwa na vyama vinne vilivyoshirikiana kuanzia wakati wa Bunge Maalum la Katiba, Dk. Makaidi amesema serikali itakayoundwa na UKAWA itainua michezo.
Amesema yeye alikuwa mwanachama wa klabu ya Simba, yenye makao makuu yake mtaa wa Msimbazi, Dar es Salaam, akiwa na kadi ya uanachama wa maisha.
Dk. Makaidi amesema katika kuonesha mapenzi ya kimichezo juu ya Edward Lowassa na mgombea mwenza Juma Duni Haji, inafaa kutengeneza mpira na kuubandika picha ya Lowassa.
âAu sio, si inawezekana⦠tunatengeneza mpira na kuubandika picha ya Mhe Lowassa iwe kama kitu cha kumuonesha mapenzi ya wananchi,â amesema Dk. Makaidi ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chama cha NLD (National League for Democracy).
Mwanasiasa huyo mkongwe aliyeanzisha chama hicho tangu Juni 1992, viliporuhusiwa vyama vingi, zaidi ya CCM kilichokuwapo chini ya mfumo wa chama kimoja nchini Tanzania, amepata nafasi ya kugombea ubunge jimbo la Masasi, mkoani Mtwara, ambako ndiko nyumbani kwao kwa asili alikozaliwa.
Naye ni miongoni mwa viongozi wakuu wa vyama hivyo vinne waliokuwa wajumbe wa Bunge Maalum la Katiba, waliogomea bunge hilo pamoja na wajumbe wote wa vyama vyao waliporidhika kuwa CCM kwa kutumia wingi wao uliopitiliza, wamefanikisha mpango wao wa kuivuruga rasimu ya katiba iliyojaa maoni ya wananchi, ikiandikwa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba iliyokuwa chini ya Mwenyekiti Joseph Warioba.
Chama cha NLD, kimepata majimbo matatu ya kugombea, yakiwemo pia Lulindi na Ndanda, yote ya mkoani Mtwara.
Recent Comments