MAJOGOO mawili ya kisiasa Zanzibar, Maalim Seif Shariff Hamad na Dk. Ali Mohamed Shein wanapasha moto misuli kujiandaa na safari ngumu ya kampeni ya kugombea urais inayotarajiwa kuanza baada ya uteuzi unaofanyika Jumapili hii. Anaandika Jabir Idrissa ⦠(endelea).
Maalim Seif ambaye amemzidi kwa kila hali Dk. Shein ikizungumziwa uzoefu wa siasa na uwezo wa kiuongozi, anagombea wadhifa huo kupitia Chama cha Wananchi (CUF) wakati Dk. Shein anawakilisha Chama Cha Mapinduzi (CCM) akiingia kutetea kiti alichotwaa 2010.
Kiongozi huyo wa CUF (Katibu Mkuu) alirudisha fomu ya uteuzi kwenye ofisi za Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar juzi, na jana ikawa zamu ya mshindani wake mkuu huyo, Dk. Shein, mwenye elimu ya udaktari wa falsafa katika magonjwa ya binadamu.
Ingawa wapo wanasiasa 13 wengine waliochukua fomu hiyo, inatarajiwa kuwa ushindani wa maana utabakia kwa majogoo hao wawili ambao pamoja na kufanya kazi pamoja kwa miaka mitano, uhusiano wao kisiasa ni wa mfano wa paka na panya.
Dk. Shein aliyetangazwa mshindi wa urais mwaka 2010 kwa kupata asilimia 50.1 (kura 179,809) dhidi ya asilimia 49.1 (kura 176,338), anamaliza kipindi cha miaka mitano ya kuongoza Zanzibar, chini ya mfumo wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK) iliyoundwa kufuatia mabadiliko ya Katiba ya Zanzibar ya mwaka Agosti 2010.
Katika uchaguzi uliopita, kulikuwa na wagombea wengine wane, ambao hakuna aliyepata kura zilizofikia asilimia tano, kiwango ambacho kingewezesha chama husika kushirikishwa katika serikali.
Safari hii, majogoo hao wanasubiri kama kutakuwa na mgombea yeyote atakayemudu kurudisha fomu na kukidhi vigezo vya kupitishwa na tume kugombea. Jumla walichukua fomu wawaniaji 15.
Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar, Jecha Salim Jecha, anatarajiwa kesho Jumapili, kutangaza majina ya wagombea waliopita kwenye chekeche la vigezo vya kikatiba vya kugombea urais.
Uchaguzi utakaopigwa Oktoba 25, unafanyika huku wanasiasa hao wawili wakivutana kwa hoja kwamba aliyeshika madaraka ameshindwa kurekebisha tume na hivyo kuibakiza na sekretarieti ileile ya tangu 1995, ukiacha tu Mkurugenzi Said Kassim Ali aliyekuwepo 2010.
Maalim Seif alisema siku alipochukua fomu kwamba Rais Dk. Shein ameshindwa kutimiza ahadi yake ya kuisuka upya sekretarieti na kumlaumu kwamba hakuchukua hatua makusudi kwa kuwa hana utashi kwa vile kasoro iliyopo inamsaidia kushinda kwa upendeleo.
Dk. Shein aliulizwa kuhusu malalamiko ya makamu wake wa kwanza huyo wa rais, lakini aliwaambia waandishi wa habari mjini Zanzibar tarehe 24 Agosti, âHakuna makubaliano yoyote niliyoyafanya na upinzani kuhusu tume.â
Hata hivyo, Maalim Seif amesema katika mazingira hayohayo ya tume isiyoaminika kiuadilifu, ameingia kugombea na ânina matumaini makubwa ya kushinda iwapo uchaguzi utakuwa huru na wa haki.â
Kama alivyo Dk. Shein, Maalim Seif ambaye ni mtaalamu wa siasa mwenye shahada ya kwanza, naye ni mzaliwa wa kisiwani Pemba katika kijiji cha Mtambwe, Wilaya ya Wete. Daktari alizaliwa Mkanyageni, Wilaya ya Mkoani.
Maalim Seif anagombea kwa mara ya tano safari hii, mara zote zilizotangulia akiwa amelalamika kuwa amehujumiwa kwa mkakati uliosukwa kwa ushirikiano wa CCM na vyombo vya usalama wakiitumia Tume kufanya upendeleo.
Recent Comments