WATANZANIA wengi bado hawana ufahamu wa kutosha kuhusu Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), hivyo kusababisha wengi wao kupokea au kutoa taarifa za upotoshaji. Kwa tafsiri nyepesi tunaweza kusema JKT ni sawa na chuo cha mafunzo kwa vijana wanaomaliza kidato cha sita wanaojiunga kwa mujibu wa sheria kwa miezi mitatu na wanaoshiriki kwa kujitolea kwa miaka miwili.
Lakini kwa usahihi, JKT ni zaidi ya tafsiri hiyo kwa kuwa imesaidia kuwajenga vijana kuwa wazalendo kwa taifa lao na hata kutoa elimu kwa vijana wanaoshiriki mafunzo kuhusu shughuli za kiuchumi. Mafunzo ya JKT yamerejeshwa baada ya kusitishwa mwaka 1994. Mkuu wa Utawala na Mafunzo wa JKT, Brigedia Jenerali Jacob Kingu anasema kurejeshwa kwa mafunzo hayo kutachochea mafanikio kwa vijana wengi, kwa kuwa vijana wanaonekana kuwa wazalendo kwa taifa lao.
Kingu anatoa rai kwa wananchi wakiwemo wazazi waamini kuwa JKT ni sehemu salama kwa vijana, wapuuze upotoshaji kwa kuwa jeshi hilo ni sehemu bora kwa kufanikisha ndoto za wananchi na kubadili fikra kutokana na yale wanayoyapata katika mafunzo. Vijana wanapojiunga na mafunzo ya jeshi hilo hujenga mshikamano na umoja wa kitaifa ili kulinda uhuru wa taifa lao baada ya kufunzwa uzalendo, stadi za kazi zinazowawezesha kujiajiri wanapomaliza mikataba ya kujitolea kwa miaka miwili.
Mafunzo hayo yamekuwa yakitolewa kwenye kambi za jeshi zilizopo nchini ikiwemo ya JKT Kikosi cha 832 KJ iliyoanzishwa Januari mwaka 1964. Kambi hiyo imepata umaarufu kutokana na utendaji wake na imekuwa mfano wa kuigwa baada ya kuonesha ufanisi bora kwa kuongozwa na mkuu wa kambi hiyo, Luteni Kanali Charles Mbuge. Imefanikiwa kwa kiasi kikubwa kufanikisha malengo ya JKT, ikiwa ni pamoja na kujenga nidhamu kwa vijana waliomaliza kidato cha sita kwa mujibu wa sheria na wale wanaojitolea.
Mafunzo ya JKT yamesaidia wanafunzi wanaohitimu kidato cha sita wanaojiunga na vyuo kutoshiriki migomo iliyokuwa ikisababisha baadhi yao kushindwa kuhitimu masomo. Vijana hao wamejengewa moyo wa uzalendo kwa kuipenda nchi yao sanjari na kuwa na umoja na ushirikiano kwa muda wote hivyo kuweza kulijenga taifa lao baada ya kujifunza ujasiriamali. Mafunzo ya JKT yanawawezesha vijana kuwa na uwezo wa kujiajiri na hivyo kutokuwa mzigo kwa taifa baada ya kuondokana na mawazo mgando kuwa lazima kijana aajiriwe na serikali.
Mkuu wa kambi hiyo, Luteni Kanali Mbuge anasema, mafunzo hayo kwa mujibu wa sheria yanahusisha vijana wanaomaliza elimu ya kidato cha sita kabla ya kujiunga na vyuo vikuu. Anasema kwa vijana wanaojiunga katika mafunzo ya kujitolea wanajiunga wenyewe na wanatoka kwenye mikoa mbalimbali. Mbuge anasema, mafunzo kwa miezi sita huwa ni mafunzo ya kijeshi, na ya miezi 18 huwa ya stadi za kazi na ujasiriamali ikiwemo ushonaji, kilimo, ufugaji na nyinginezo.
Katika kundi hilo wapo pia walemavu wa viungo na ngozi (albino), jamii ya wawindaji (Wahadzabe) hivyo kuonesha kuwa jeshi hilo halina ubaguzi, linatoa fursa sawa kwa wote. Mshiriki kutoka jamii hiyo ya wawindaji, Oraph George anasema, uwepo wake katika Kambi ya JKT Ruvu ni msaada mkubwa katika maisha yake kwa maana imefanikisha kubadili mtindo wa maisha yake.
Anasema awali ilikuwa vigumu kwake kuendana na mazingira ya kambi hiyo kwa kuwa alizoea kuishi katika maisha ya uwindaji na kula vyakula vya matunda na nyama tu. âNaishukuru kambi ya JKT Ruvu kwa kunibadilisha na sasa naweza kuishi na jamii nyingine vizuri na kula vyakula vya kawaida bila tabu sanjari na kuzungumza kiswahili vema, ingawa mwanzoni nilitaka kutoroka lakini viongozi wa hapo walinipa ushauri mzuri,â anasema George.
Mhadzabe mwingine anayeshiriki mafunzo hayo yaliyopewa jina la Operesheni Kikwete, Pili Maduru anasema, anajisikia vema kuwemo katika kambi hiyo kwa kuwa amejifunza mambo mengi. âNimejifunza kula vyakula vya aina mbalimbali tofauti na nilivyokuwa kijijini kwetu Endamakhi mkoani Arusha, ukweli nawashukuru viongozi wa JKT Ruvu kwa kutupa muono mwingine katika maisha yetu,âanasema Maduru.
Mlemavu wa viungo, Anderson Antoni, ambaye amemaliza kidato cha sita katika Shule ya Sekondari Jamhuri Dodoma, anasema amechaguliwa kujiunga na kambi hiyo kwa mujibu wa sheria, lakini awali wazazi wake walimkatalia asiende huko. âHata wazazi wangu walikuwa wagumu kunikubalia kuja hapa Ruvu, kwa sasa mimi ni shuhuda mzuri kuwa mtu yeyote anaweza kuhudhuria mafunzo ya JKT bila kujali ulemavu wake,â anasema.
Mlemavu wa ngozi aliyepo katika kambi hiyo, Heriel Mlay ambaye amesoma katika shule ya sekondari ya Ruvu mkoani Pwani, anasema mafunzo hayo kwa kiasi kikubwa yamebadili mtindo wa maisha yake kwa kuwa awali alikuwa akijitenga na wenzake. âSitaondoka bure katika kambi hii, kwani nimejifunza mengi ikiwemo ufugaji wa kuku, kilimo na mambo mengine ambayo yatakuwa msaada tosha katika maisha yangu,â anasema.
Recent Comments