Na Waandishi Wetu, Zanzibar
CHAMA cha Wananchi (CUF) kimezindua kampeni za Urais Zanzibar kwa kishindo huku mgombea wake, Maalimu Seif Sharif Hamad, akiahidi ajira kwa Wanzibari wote ndani ya miaka mitano na kubadilisha uchumi wa nchi hiyo kuwa imara kama ule wa Singapore.
Akizungumza na maelfu ya wananchi wa visiwa hivyo waliojitokeza jana kwenye uwanja wa Kibanda Maiti Unguja, Maalim Seif alisema endapo atapatiwa ridhaa ya kuongeza nchi, atapigania pia mamlaka kamili ya Zanzibar ikiwa ni pamoja na kupata katiba inayotambua Muungano wenye usawa.
Ndoto yangu ya kuifanya Zanzibar kuwa Singapore ya Afrika Mashariki ipo palepale, nitahakikisha tunakuwa na uchumi imara ambao utakuwa unakua kwa haraka,âalisema Maalim Seif.
Alisema katika uongozi wake atahakikisha nchi hiyo inajenga bandari ya kisasa kwa vitendo na si maneno kama wanavyofanya wengine.
Alisema pia kuwa serikali inayomaliza muda wake ilikuwa na mipango ya kujenga Uwanja wa Ndege wa Zanzibar na kuahidi kuuzindua Oktoba mwaka huu lakini dalili zinaonyesha suala hilo halitawezekana.
âAirport (uwanja wa ndege) ilisemwa itazinduliwa Oktoba lakini juzi nilitembelea ujenzi wa uwanja huo inaonekana haiwezekani,âalisema Maalim Seif.
Alisema uboreshaji wa miundombinu ya Zanzibar ikiwa ni pamoja na bandari, kutafanya watu wawe wanafika visiwani hivyo kununua bidhaa kama ambavyo sasa wanapoenda Dubai.
Alisema serikali yake pia itafungua Benki ya Uwekezaji ya Zanzibar(ZIB) ambayo itakuwa inatoa mikopo kwa watu mbalimbali wakiwamo vijana lengo likiwa ni kuwapa mitaji watu wote.
âBenki itakuwa inatoa mikopo ya masharti nafuu, lengo ni kuwasaidia vijana wasiokuwa na mitaji kujiendesha katika maisha,âalisema Maalim Seif na kuongeza:
âHakuna jambo linaloniuma kama kuona vijana wakiwa wanarandaranda (kutembea)barabarani, matumaini yangu nikimaliza miaka mitano kutakuwa hakuna mtu asiyekuwa na ajira,âalisema Maalim Seif.
Akizungumzia mafuta na gesi, alisema ataanzisha wizara maalumu ya kushughulika na nishati hiyo na kwamba ndani ya siku 100 atakuwa ametengeza sheria na sera yake wananchi waweze kuonja matunda yake.
Muungano
kuhusu muungano alisema ahatakikisha visiwa hivyo vinapata mamlaka kamili viweze kufanya uamuzi kwa masuala yanayowahusu.
âWazanzibari wanataka kuona nchi yao imepata mamlaka kamili, walio madarakani hivi sasa wameshindwa, zimefanyika juhudi za kuleta Tume ya Jaji Joseph Warioba kwa kukusanya maoni.
âMlio wengi mlitaka muungano wa mkataba lakini tume wakasema tupate serikali tatu kwa bahati mbaya CCM waliikataa na kuweka vitu vyao.
âHata waliokuwa mbele katika mambo hayo walishindwa kuitetea Zanzibar na badala yake walipofika huko waliufyata wakaandaa rasimu yao wakakubali Zanzibar iendelee kudhalilishwaâ.
Alisema endapo atachaguliwa yeye pamoja na mgombea urais wa Muungano, Edward Lowassa, watashirikiana na kuhakikisha wanaitisha upya bunge la katiba na kurudisha maoni ya wananchi ambayo yataelekeza kuwapo serikali tatu ambazo zina mamlaka.
Misingi ya utawala bora
Maalim Seif alisema atahakikisha anaimarisha misingi ya utawala bora ambayo itazuia Wazanzibari kunyanyaswa na kuteswa ndani ya nchi yao.
âMambo ya watu kuvaa soksi usoni wanapiga watu mwisho Oktoba 25, siwezi kukubali Wazanzibari wanadhalilishwa ndani ya nchi yao,âalisema Maalim Seif.
Alisema pia hataruhusu Mzanzibari aliyefanya kosa visiwani humo kwenda kusomewa mashtaka Tanzania Bara.
âMahakama ya Dar es Salaam na Zanzibar ni sawa ila leo wameamua kuwatoa watu huku kuwapeleka huko, nasema watarudi kama wana makosa watahukumiwa huku kwa mahakama ya Zanzibar,âalisema Maalim Seif.
Lowassa alaani uchanaji mabango yake
Naye Mgombea urais wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo(Chadema) anayewakilisha Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), Edward Lowassa, amekemea vikali tabia ya wanachama wa Chama Cha Mapinduzi(CCM) kuchana mabango yake akisema ni kinyume na sheria.
Alisema katika kipindi hiki cha kampeni, mambo mengi yanaweza kujitokeza hivyo wanachama hao wanapaswa kuwa na moyo wa uvumilivu kuepusha matatizo.
Alisisitiza kauli yake kuwa Ukawa wataendelea kufanya kampeni za ustaarabu kuhakikisha wanapata ushindi kwa sababu uwezo huo wanao huku akiwataka CCM kuacha tabia ya kufikiria kuiba kura.
âSiku hizi wameanza tabia ya kuchukua mabango yetu na kuyaangusha, wakimaliza wanayatupa porini, nawaambia waache kabisa mchezo huo, sisi tutandelea kufanya kampeni za ustaarabu kuhakikisha tunapata ushindi kwa sababu uwezo tunao.
âMtanipa kuraâ¦? Wangapi watamchagua Lowassaâ¦wanyooshe mikono juu, uwezo wa kushinda tunao, ninawaambia CCM waache kuiba kura,âalisema Lowassa.
Lowassa pia alimzungumzia mgombea urais wa Zanzibar wa Chama cha CUF, Maalim Seif Sharif Hamad kuwa ni kiongozi aliyepigania ukombozi wa taifa hilo hivyo anapaswa kuungwa mkono aweze kupata ushindi.
Naye Mwasisi wa CCM, Mzee Nassoro Moyo alisema Wazanzibari wanaopenda amani na utulivu hawana budi kuwachagua wagombea wa CUF waweze kupata ushindi na kuwaletea wananchi maendeleo.
âKama kuna Mzanzibari anapenda amani na utulivu, anapaswa kuwapigia kura ya ndiyo viongozi wa CUF waweze kuendeleza amani,âalisema Mzee Moyo.
NCCR-MAGEUZI
Katibu Mkuu wa Chama Cha NCCR-Mageuzi, Mosena Nyambabe alisema CCM kimekuwa kikikataa kutoa ushindi kwa CUF lakini mwaka huu kitautoa kulingana na wanavyotaka wenyewe.
Naye Naibu Katibu Mkuu wa Chadema Zanzibar, Salum Mwalimu aliwataka Wazanzibari wasijisahau kwa madhira na kero zilizofanywa na CCM, hivyo wafanye uamuzi mgumu kuhakikisha wanapata ushindi.
âWazanzibari tusijisahau kwa matatizo yetu yaliyotukuta, tunapaswa kuwa bega kwa bega kuhakikisha tunapata ushindi,âalisema Mwalimu.
Naibu Katibu Mkuu wa CUF Zanzibar, Ismail Jussa Ladhu alisema leo ni siku ya kumbukumbu kwa wananchi waliofariki dunia kwenye meli ya MV Spice Islanders ambayo imetimiza miaka minne tangu ilipozama katika Bahari ya Hindi.
Ilivyokuwa
VIWANJA vya Kibanda Maiti jana vilifurika umati wa watu waliokuja kushuhudia uzinduzi wa kampeni za mgombea urais wa Chama cha Wananchi (CUF) Zanzibar, Maalif Seif Sharif Hamad.
Mkutano huo uliopangwa kuanza saa 9:00 alasiri, lakini kuanzia saa 4:00 asabuhi tayari baadhi ya wanachama wa chama hicho walianza kuwasili uwanjani hapo.
Ilipotimu saa 7 mchana uwanja huo ulikuwa umefurika umati wa watu huku wengine wakigombea mahali pa kukaa.
Makundi mbalimbali ya vijana walikusanyika uwanjani hapo huku wakiimba nyimbo mbalimbali, huku baadhi yao walikuwa wakipeperusha bendera za CUF na zile za chama cha zamani cha Afro Shirazi (ASP).
Hata hivyo vikundi mbalimbali vya ngoma navyo havikuwa nyuma, ambapo wasanii walijipanga wakituimbuiza nyimbo mbalimbali za kuisifia CUF na vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa).
Vikundi hivyo vya ngoma vilikuwa vikiimba âMwaka huu tumeamua, CCM hata wafanye nini sisi tumeamua kuwapa kura zetu Seif na Lowassa, tuna imani mabadiliko yataletwa na ninyi, kura zetu tutawapaâ¦CCM waone kinguzungu.
Recent Comments