MGOMBEA Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk John Magufuli, ameendelea kuchanja mbuga katika kampeni zake, huku akitoa ahadi zenye kuyagusa makundi mbalimbali ya Watanzania, safari hii akiahidi kuwakomboa wakulima kwa kuwaondolea mzigo wa ushuru wa mazao.
Aidha, amewataka Watanzania bila kujali itikadi zao, wamchague awe Rais wa Awamu ya Tano, ili akawafanyie kazi ya kuondoa kero zinazowazunguka, ikiwemo za miundombinu, afya, elimu, ujenzi wa viwanda na fursa ya kuanzisha na kukuza biashara zao.
Aliyasema hayo jana katika mikutano ya hadhara ya kampeni kuanzia Mkinga, Korogwe, Bumbuli mpaka mjini Lushoto.
Alisema Serikali atakayoiongoza, itafuta ushuru wa mazao katika masoko mbalimbali, kwa kuwa hakuna haja ya kumtoza mkulima ushuru wakati alilima mwenyewe na kubeba mazao yake bila kusaidiwa na mtu kuyaleta sokoni.
Pamoja na kukabiliana na kero hizo, aliwasisitizia wananchi kuhakikisha wanalinda amani ya nchi ili isipotee kwa kuwa bila amani, kero hizo hazitaondoka na hata mali kidogo walizonazo watazikimbia.
Alitoa mifano ya nchi jirani zilizowahi kupoteza amani kuwa ni pamoja na Kenya ambao walipoteza amani baada ya uchaguzi, Uganda ambao walipoteza amani wakati wa uongozi wa Iddi Amini na Rwanda na Burundi wakati wa vita vya wenyewe kwa wenyewe na kuhadharisha kuwa amani lazima itunzwe Tanzania kwa kuwa imebaki yenyewe kuwa kisiwa cha amani.
Alitumia fursa hiyo kuvisifu vyombo vya ulinzi na usalama, ikiwemo Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), Jeshi la Polisi, Jeshi la Magereza, Uhamiaji na Zimamoto kwa kutunza amani na kuongeza kuwa Serikali yake itahakikisha inaboresha maslahi ya askari hao.
Katika afya, aliahidi kuhakikisha hospitali za umma, hazikosi dawa huku Serikali ikilenga zahanati katika kila kijiji na mtaa, kituo cha afya katika kila kata, hospitali ya wilaya katika kila wilaya na hospitali ya rufaa katika kila mkoa.
Katika elimu mbali na kuongeza maslahi ya walimu na kujenga nyumba zao, Dk Magufuli alisema kuanzia mwakani wanafunzi wote wa elimu ya awali mpaka kidato cha nne watasoma bila kulipa ada.
Katika kuongeza fursa za kuanzisha biashara na kuboresha zilizopo, Dk Magufuli alisema Serikali yake itatoa Sh milioni 50 kwa kila mtaa na kila kijiji, kwa ajili ya kukopesha wanawake na vijana.
Mbali na kukopesha vijana hao, Dk Magufuli alisema atahakikisha wafanyabiashara wadogo wakiwemo bodaboda na mama ntilie, hawasumbuliwi katika biashara zao, ili wafanye kazi na kujipatia kipato halali kwa kuwa hata Mungu amesema, asiyefanya kazi na asile.
Kada wa CCM na Naibu Waziri wa Jinsia, Wanawake na Watoto, Ummy Mwalimu, alisema Dk Magufuli ana upendo kwa wanawake, ndio maana amemteua mgombea mwenza mwanamke, Samia Suluhu Hassan na kuwataka wanawake, aliosema kati ya wapigakura 100, 51 ni wanawake, wampigie kura Dk Magufuli.
Makamba anena
Katibu Mkuu mstaafu wa CCM, Yusufu Makamba, aliwataka Watanzania wakati huu wakitafakari kiongozi wanayetaka awaongoze katika miaka mitano ijayo, wapime vyama vilivyosimamisha wagombea urais, na chama hicho tawala kwa kutumia vigezo mbalimbali.
Akizungumza katika mikutano ya kampeni ya Dk Magufuli, Makamba alisema moja ya kigezo cha kupima vyama hivyo, ni uzoefu wa viongozi na wanachama wa vyama hivyo katika uongozi wa nafasi mbalimbali ndani ya vyama hivyo, kwa wananchi na serikalini.
Alisema wananchi wanapoiangalia CCM, wasisahau kuwa ndiyo aliyokuwemo Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, na ndiyo chama cha Rais wa Awamu ya Pili, Ali Hassan Mwinyi, Rais wa Awamu ya Tatu, Benjamini Mkapa na Rais wa Awamu ya Nne, Jakaya Kikwete.
Makamba alisema wako wengi wanaoweza kuangaliwa ndani chama hicho, akiwemo Katibu Mkuu, Abdulrahman Kinana, na kuhoji ndani ya Chadema, anaonekana nani zaidi ya Mwenyekiti wake, Freeman Mbowe?
Makamba aliwataka Watanzania wasifanye makosa katika kutathimini vyama kabla ya kutathimini wagombea, kwa kuwa chama kina mchango mkubwa katika uongozi wa nchi.
Recent Comments