WAZIRI Mkuu, Mizengo Pinda ameacha alama ambayo haijawekwa na kiongozi yeyote katika shule ya msingi alikosomea, baada ya kuijenga upya na kuifanya ya kisasa.
Hali hiyo imesababisha wenyeji kutaka iwe ya sekondari au ya mchepuo wa Kiingereza, kutokana na ubora wake.
Shule hiyo ya Msingi Kibaoni iliyopo mkoani Katavi ambayo Pinda amesisitiza kuwa itabaki ya mchepuo wa kawaida, kwa kuwa naye alisoma vivyo hivyo na kujua Kiingereza vizuri, imejengwa upya na wanafunzi wake wanatarajiwa kupewa jozi mbili za sare mpya na viatu kila mmoja.
Akizungumza jana wakati akipokea msaada wa vifaa vya shule hiyo kutoka Kampuni ya Huawei ya China na Benki ya NMB, Pinda alisema alikuwa na ndoto tangu akiwa mtumishi wa Serikali, Mbunge na hata Waziri Mkuu, ya kitu atakachoacha kwa watu wa kijiji alichokulia.
Kwa mujibu wa Pinda, mara nyingi alipopita na kuona shule hiyo, wazo la atawaachaje wananchi hao lilimjia, ndipo aliona ili kumshukuru Mungu na wanakijiji, ajenge shule hiyo iwe ya kisasa.
Katika kutekeleza ndoto hiyo, Pinda alisema baada ya kujenga majengo ya kisasa, aliamua kuiwekea teknolojia ya kisasa ya kompyuta, ambayo wanafunzi watatumia ipads, zenye uwezo wa kuhifadhi vitabu zaidi ya 200 na walimu watatumia kompyuta zenye skrini kubwa katika ufundishaji wake.
âNiliona teknolojia hiyo katika shule moja mkoani Arusha, ndipo nikaona niige mfumo huo katika shule hii ya kihistoria,â alisema jana wakati akipokea vifaa hivyo. Katika maboresho ya shule hiyo, Pinda alisema aliomba kuongezewa eneo la shule hiyo yenye wanafunzi 800, ambapo alipewa eneo lenye ukubwa wa ekari 65.
Baada ya kupewa eneo, mbali na kujenga madarasa makubwa na ya kutosha, aliamua kujenga jengo la kisasa la utawala, maktaba na nyumba za walimu na viwanja vya michezo ya aina mbalimbali kwa kuomba ufadhili kutoka taasisi mbalimbali za ndani na nje ya nchi.
Waziri Mkuu alisema mpaka sasa tayari madarasa 14 yamekamilika, jengo la utawala na jengo la teknolojia ya habari na mawasiliano (Tehama) kwa wanafunzi kwa ajili ya kusoma vitabu katika ipads, vyoo matundu 48 na nyumba sita za walimu.
Akifafanua alivyotafuta fedha, alisema alianzisha jitihada za kukamilisha ndoto hiyo kwa kufungua akaunti iliyokusanya Sh milioni 785.01 na Dola za Marekani 237,834, ambapo Ubalozi wa China ulianza kumchangia mwaka 2013 kwa kumpa Sh milioni 320.
Pinda alisema jana walipokea msaada wa vifaa kutoka kampuni ya Huawei kwa ajili ya jengo la Tehama, vyenye thamani ya Dola za Marekani 150,000.
Vifaa hivyo vilivyokabidhiwa na Balozi wa China, Dk Lv Youging ni kompyuta 50, ipads 100 zenye uwezo wa kuhifadhi vitabu 2,000, kompyuta mpakato tano, printa mbili, scanner mbili, projekta mbili na skrini za kufundishia mbili.
Pinda alisema Benki ya NMB nao walitoa vifaa vya michezo vyenye thamani ya Sh milioni 30, vilivyokabidhiwa na Ofisa Mkuu wa Fedha, Waziri Barnaba ambavyo ni jezi za michezo jozi 192, mipira 40, madawati yenye thamani ya Sh milioni 10 kwa ajili ya Kituo cha Walimu na kompyuta nne.
Aidha, kampuni ya Huan Jian kutoka nchini China, ilitoa jozi 1,000 za viatu kwa shule ya msingi na sare 512 vilivyokabidhiwa na fundi wa kampuni hiyo, Saleh Mustafa.
Recent Comments