UTAFITI wa Taasisi ya Twaweza umeonesha kuwa, mgombea urais wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. John Magufuli anayo fursa ya kushinda Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu kwa zaidi ya asilimia 65. Anaandika Charles William na Sarafina Lwidino ⦠(endelea).
Kwenye utafiti huo, mgombea urais wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Edward Lowassa anayeungwa mkono na vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA) akitajwa kupata asilimia 25.
Vyama vinavyounda UKAWA ni pamoja na Chadema yenyewe, Chama cha Wananchi (CUF), NCCR-Mageuzi pamoja na NLD.
Pia utafiti huo umeonesha, Dk. Magufuli anapendwa zaidi vijijini kuliko mijini huku Lowassa akipendwa zaidi mijini kuliko vijijini,pia Dk. Magufuli anapendwa zaidi na wanawake kuliko wanaume na Lowassa akipendwa zaidi na wanaume kuliko wanawake.
Akitoa matokeo ya utafiti huo mbele ya wananchi na vyombo vya habari katika Ukumbi wa Makumbusho jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi Mtendaji wa taasisi hiyo, Aidan Eyakuze amesema njia iliyotumika kufanya utafiti huo ni ya kupigia simu kwa watu 1848 ambao walichaguliwa kutoka maeneo mbalimbali Tanzania.
Utafiti huo unaonesha kuwa, CCM inaweza kuchaguliwa na wananchi kwa asilimia 66 huku mgombea wake Dk. Magufuli anaweza kuchaguliwa kwa asilimia 65. Utafiti huo pia umeeleza CCM ndio chama kilicho karibu zaidi na wananchi.
âTuliwauliza Watanzania iwapo Uchaguzi Mkuu ungefanyika mwaka huu mngechagua chama gani? Na asilimia 66 wakasema wangechagua CCM huku asimia 24 wakisema wangechagua Chadema.
âLakini pia tulipowauliza kuhusu mtu katika nafasi ya urais, asilimia 65 walisema Magufuli na Lowassa asilimia 25 huku vyama vingine vikiambulia asilimia zingine ikiwemo asilimia 3, na wengine ailimia 7 walisema hawajui wa kumchagua.â anaeleleza Eyakuze.
Alipoombwa kutoa ufafanuzi juu ya njia zilizotumika kufanya utafiti huo, mkurugenzi huyo amesema waliwahoji watu 1848 kutoka maeneo 200 tofauti Tanzania Bara kwa kuwachagua âkibahati nasibuâ.
Pia ameeleza, watu hao waliwapatia simu za mkononi pamoja na chaji ya kutumia mwanga wa jua (solar) ili kuwawezesha kupigiwa simu mara kwa mara na kuhojiwa juu ya masuala husika.
âUtafiti wetu wa 27 Tanzania Bara tulifanya kwa kutumia simu za mkononi âmobile phone panel surveyâ ambapo tuliwapatia simu wananchi na kuwapa chaji ili kuepuka tatizo la umeme na tulikuwa tukiwapigia mara kwa mara ili kupata mawazo yao ambayo matokeo yake ndio haya,â aefafamua.
Aidha utafiti huo pia umeonesha kuwa changamoto za Watanzania zimebadilika kulingana na takwimu za miaka mitatu iliyopita ambapo mwaka 2012, 2013, 2014 changamoto kubwa zilikuwa uchumi lakini kwa mwaka 2015 wananchi wametaja afya, elimu na maji kuwa changamoto kubwa zaidi.
Akitoa maoni kuhusu na utafiti huo, mmoja kati ya wageni waalikwa kwenye tukio hilo, Maria Sarungi amesema, utafiti huo hauwezi kuathiri uamuzi wa wapiga kura katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 25 mwaka huu.
Hata hivyo ametaka UKAWA kutoa elimu zaidi kwa wapiga kura wao ili wafahamu kuwa jina hilo (UKAWA) halitaonekana katika karatasi za kupigia kura kwani tafiti zinaonesha wengi hawajui.
Mkurugunzi wa Mtandao wa Kutetea Haki za Binadamu (THDRC), Onesmo Ole Ngurumwa katika mahojiano yake na waandishi wa habari baada ya kutoka nje ya ukumbi huo amesema ânawapongeza sana Twaweza kwa ujasili walionao wa kuweza kusimama na kuyatangaza matokeo ya utafiti huo bila uoga.
âKwanza waandishi pamoja na wananchi mnatakiwa kufanya uchunguzi ni kwa nini taasisi nyingi mwaka huu hazikufanya utafiti wa uchaguzi wa mwaka huu? Ni kutokana na ugumu na hali ya kisiasa iliyopo sasa hivi inatisha na kutia uoga hata kutangaza matokeo kwani siku hizi wananchi wameamka,â amesema.
Hata hivyo, Olengurumwa amewataka Twaweza kuwa tayari kuyajibu maswali yote ambayo yataulizwa na wananchi kuanzia leo baada ya kutangaza utafiti huo.
Recent Comments