*Mkurugenzi Tehama aondolewa
* Maofisa watoa kauli tofauti
NA SHABANI MATUTU, DAR ES SALAAM
MKURUGENZI wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama) wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Dk. Sisti Cariah ameondolewa kwenye nafasi hiyo, imefahamika.
Taarifa za uhakika kutoka ndani ya NEC ambazo MTANZANIA ilizipata juzi na jana zimeeleza kuwa mkurugenzi huyo ambaye ni mtu muhimu katika Tume ameondolewa katika siku za karibuni huku kukiwa hakuna taarifa ya wapi alikohamishiwa serikalini.
Chanzo hicho cha ndani ya tume kimesema mkurugenzi huyo ameondolewa siku tano zilizopita huku zikiwa zimesalia siku 25 tu kufikia Uchaguzi Mkuu Oktoba 25 wakati idara hiyo ya Tehama ikiwa ndiyo ina orodha nzima ya Watanzania wanaotarajiwa kupiga kura.
âNi kweli mkurugenzi huyo wa Tehama ameondolewa na nafasi yake imechukuliwa na aliyekuwa msaidizi wake (bila kumtaja) na nafasi nyingine zinaendelea kusukwa upya.
Hadi jana tovuti ya Tume hiyo hadi ilikuwa ikionyesha kuwapo mkurugenzi mmoja tu ambaye ni Mkurugenzi wa Uchaguzi wa NEC, Ramadhan Kailima, huku ukiwapo unaosomeka kwamba kurugenzi nyingine zinaendelea kusukwa upya.
Tume hiyo ina kurugenzi saba ambazo ni Elimu ya mpiga kura na habari, Uchaguzi, Ununuzi, Uhasibu, Ukaguzi, Utawala na Tehama.
MTANZANIA lilipomtafuta Mkuu wa Kitengo cha Habari wa NEC, Clarence Nanyaro kupata ufafanuzi wa suala hilo alisema:
âNdugu yangu hakuna mkuu yeyote wa idara aliyehamishwa hadi sasa lakini ngoja nifuatilie zaidi nitakupa jibu zuri kwa kutumia simu ya mezani.â
Baada ya dakika chache alipiga simu lakini aliendelea kusisitiza kwamba anaamini idara hizo hazijafanyiwa marekebisho.
Hata hivyo alisema hazisimamiwi na wakurugenzi bali zinasimamiwa na wakuu wa idara.
âWatu wengi wamekuwa wakiwaita wakuu wa idara hizo kama wakurugenzi jambo ambalo si sahihi na hata hivyo wote bado wapo,â alisema Nanyaro na kuongeza:
âSina taarifa za kuhamishwa Dk. Cariah kwa kuwa hadi jana (juzi) alikuwa kazini akiwajibika hadi saa nne usiku tulipoachana.
Alipoulizwa kuhusu tovuti ya NEC kuwa na ujumbe unaoonyesha kufanyika marekebisho ya wakuu wa kurugenzi zote saba, alisema suala hilo aulizwe Mkurugenzi wa Uchaguzi, Ramadhan Kailima kwa kuwa ndiye mwenye mamlaka ya kuzungumzia wafanyakazi wa Tume.
MTANZANIA lilipomtaka asaidie kupata jibu hilo kutoka kwa bosi wake huyo alisema kwamba wakati huo mkurugenzi huo alikuwa kwenye mkutano na wawakilishi wa Umoja wa Ulaya (EU). Aliahidi kutoa jibu baadaye kama angeonana na Kailima na kukata simu.
Baadaye Nanyaro alipiga tena simu na kusema kwamba taarifa zilizokuwa zikielezea mabadiliko ya viongozi wa kurugenzi za Tume zilitokana na viongozi hao saba kutowasilisha picha zao kwa ajili ya kuziingiza taarifa hizo kwenye tovuti.
âNapenda kusema wakurugenzi wote saba wapo kazini; katika Idara ya elimu ya mpiga kura na habari, Uchaguzi, Ununuzi, Uhasibu, Ukaguzi na Utawala akiwamo Dk. Cariah wa Tehama ambaye alikuwa kazini hadi juzi na alitoka muda wa saa nne usiku,â alisema Nanyaro.
Kauli ya Jaji Lubuva
Wakati Nanyaro akisema hivyo, juzi Mwenyekiti wa NEC, Jaji Mstaafu Damian Lubuva, alipoulizwa na Mtanzania alikiri kuwa Mkurugenzi huyo wa Tehama, Dk. Cariah, amehamishwa.
Hata hivyo dakika chache baadaye Jaji Lubuva alipiga simu kwa mhariri wa gazeti hili akikanusha taarifa yake hiyo ya awali akisema hakuna mkurugenzi yeyote aliyehamishwa katika Tume yake tofauti na mabadiliko yaliyofanywa na Rais Jakaya Kikwete katika nafasi ya mkurugenzi wa uchaguzi iliyokuwa inashikiliwa na Julius Malaba ambaye aliteuliwa kuwa jaji hivi karibuni.
âNakwambia ndugu yangu, Mbowe na Chadema waache kutapatapa, wanaingilia utendaji wa Tume na serikali nawaomba wasiendelee kupotosha umma, â alisema Jaji Lubuva.
Alichosema Mbowe
Akizungumza kwenye mkutano wa kampeni uliofanyika Uwanja wa Himo Polisi mkoani Kilimanjaro juzi, Mwenyekiti Mwenza wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), Freeman Mbowe aliituhumu Serikali kwa kile alichokiita uchakachuaji wa NEC kwa kubadilisha wakurugenzi wote na kuweka wapya kutoka idara nyeti za usalama.
Mbowe ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) alidai viongozi hao wa Tume wameondolewa na serikali lengo likiwa ni kuiba kura.
âMtu mwenye wajibu wa sheria wa kusimamia uchaguzi ni Tume ya Taifa ya Uchaguzi, baada ya CCM kuona Lowassa (Mgombea Urais wa Chadema, Edward Lowassa), anashinda wameamua kuandaa mazingira ya kuchakachua Tume yenyewe.
âWalianza kumuondoa Mkurugenzi wa Tume Malaba (Julius) mwezi mmoja uliopita katika mazingira ya kutatanisha wakaleta mwingine, wiki mbili zilizopitaâ¦. wakurugenzi wote wamewangâoa na kuwaingiza wengine.
âTume kwa sasa siyo huru huku Serikali ya CCM pia ikiingiza wanajeshi kwenye tume hiyo. Namuuliza Mkuu wa Majeshi atueleze hao wanajeshi huko wameenda kufanya nini?â aliuliza Mbowe
Mbowe alisema pia kuwa CCM imeanza mkakati mwingine wa kutengeneza kura bandia na tayari zimepelekwa mkoani Kilimanjaro, Mamlaka ya Barabara (Tanroads) ambayo iko chini ya Magufuli ndiyo inasambaza kura hizo,â alidai Mbowe.
Mwenyekiti mwenza huyo wa Ukawa alisema hakuna mkakati wowote ovu utakaopangwa na CCM bila Umoja huo kuujua kwa sababu kila inachokipanga asubuhi wao wanakipata mchana.
âMnaopanga nao mchana, usiku tunakuwa nao. Kikwete wewe ni rais wa nchi usifikiri una usalama sana kama utaharibu uchaguzi wa nchi hii. Watanzania ndiyo wataamua, Kikwete na familia yako hamtatuchagulia mtu, tumia majeshi, tumia vyote unavyotaka, tutapiga kura na kuzilinda kwa gharama yoyote⦠nimesema haya nitoe onyo kwa CCM,â alisema Mbowe.
Akiwa kwenye mkutano wa kampeni katika Kata ya Kahe kwenye Viwanja vya Shule ya Oria, Mbowe alisema kila mtu atakayejaribu kuzuia mabadiliko na kuwa wakala wa Chama cha Mapinduzi (CCM) kwa sababu ya masilahi binafsi, mafuriko yatamkumba.
âMabadiliko tunayozungumzia hapa yako kwa vyama vyote, mtu yeyote atakayekuwa wakala wa kuitetea CCM kwa sababu ya ubinafsi mafuriko lazima yamkumbe, tuna kila sababu ya kupigania mabadiliko,â alisema Mbowe.
Alisema mabadiliko ambayo Ukawa unayapigania yanamgusa kila Mtanzania bila kujali dini yake wala kabila lake hivyo ni vigumu mtu kuyahujumu.
OP Mtanzania
Recent Comments