RAIS Jakaya Kikwete amezindua kiwanda cha kupasua kokoto za ukubwa mbalimbali kwa wastani wa meta za ujazo 2,000 kwa siku katika kijiji cha Pongwe, Msungura wilayani Bagamoyo mkoani Pwani.
Uzinduzi huo uliofanyika juzi, ulienda sambamba na tafrija ndogo ya kumuaga Rais Kikwete anayetarajiwa kustaafu hivi karibuni, mbele ya Balozi wa Uturuki nchini, Yasemin Eralp na Waziri wa Ulinzi na Kujenga Taifa, Dk Hussein Mwinyi.
Akitoa maelezo kuhusu kiwanda hicho, Mkuu wa Shirika la Uzalishajimali la Jeshi la Kujenga Taifa (Suma JKT), ambaye pia ndiye Mkuu wa JKT, Meja Jenerali Raphael Muhuga, alisema kokoto hizo kwa bei ya kiwandani, zitauzwa kwa Sh 30,000 kwa meta moja ya ujazo.
âBei nje ya kiwanda itategemea umbali wa kutoka eneo la kuhifadhi kokoto mpaka zinapopelekwa kwa kuwa itahusisha gharama za usafirishaji,â alisema Meja Jenerali Muhuga. Kwa mujibu wa Mkuu huyo wa JKT, kiwanda hicho ni sehemu ya miradi mingine mikubwa zaidi itakayotekelezwa na Suma JKT kwa kushirikiana na wabia wa ndani na nje ya nchi, ambapo kwa sasa hatua nzuri imeshafikiwa kuelekea kuanzishwa kwa Kiwanda cha Dawa kwa kushirikiana na kampuni ya Malaysia.
Kiwanda hicho kimejengwa kwa ubia kati ya Suma JKT yenye asilimia 30 ya hisa, sawa na Sh bilioni 1.68 ya mtaji na Kampuni ya Anit Asfalt, inayomiliki asilimia 70 ya hisa, sawa na mtaji wa uwekezaji wa Sh bilioni 3.92.
Akizungumza baada ya uzinduzi huo, Rais Kikwete alisema amekwenda katika uzinduzi huo kushuhudia mafanikio ya mradi wa kuzalisha kokoto, yaliyopatikana baada ya Suma JKT kuthubutu jambo linaloonesha kuwa viongozi hao ni watendaji.
âMmetekeleza vizuri agizo langu nililowataka muanzishe miradi tofauti tofauti, njia mbali na kiwanda hiki kuna mradi mwingine wa kuunganisha matrekta ambao ni tofauti na huu uliopo wa kuuza matrekta,â alisema Rais.
OP Habari Leo
Recent Comments