Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
WAKATI mgombea urais wa Chama cha Mapinduzi (CCM) aliyeibuka mshindi kwenye uchaguzi mkuu uliofanyika nchini Tanzania Oktoba 25 mwaka huu, anaapishwa kesho, imebainika kuwa kampeni kubwa zilifanyika kupitia mitandao ya kijamii.
Hata hivyo kampeni hizo za mitandani badala ya kuelezea sera za vyama na nini wagombea wanadhamiria kufanya iwapo watachaguliwa, imebainika kuwa, makundi mbalimbali yakiwemo ya mashabiki wa vyama tofauti, wapiga propaganda na hata watu binafsi walikuwa wakitumia mitandao hiyo kutoa taarifa za upotoshaji, kashfa, uzushi, kejeli, matusi na udhalilishaji.
Utafiti usio rasmi uliofanywa na mwandishi wa habari hii, kwenye mtandao wa kijamii wa WhatsUpp, umeonyesha kuwa, ndani ya siku moja tu, Jumapili Oktoba 18, 2015, wiki moja kabla ya kufanyika kwa uchaguzi, jumla ya meseji 475 zilitumwa kwenye akaunti ya mtu mmoja.
Kwa mujibu wa utafiti huo, asilimia 95 ambayo ni sawa na meseji 451 zilihusu kampeni za uchaguzi wakati meseji zilizotumwa kwenye akaunti hiyo zilizohusu masuala mengine ya kijamii, ni asilimia tano tu ambayo ni sawa na meseji 24.
Utafiti huo unaonyesha kuwa meseji zilizotumwa ziligawanyika katika makundi kadhaa zikiwemo; zile zinazowaunga mkono ama kuwakejeli wagombea ama wapiga debe wao, zinazounga mkono ama kukejeli vyama, zinazoonyesha majigambo baina ya wafuasi wa vyama tofauti pamoja na meseji zilizolenga kuelimishana juu ya uchaguzi.
Meseji nyingine zililenga kupashana habari juu matukio yanayohusiana na uchaguzi wakati nyingine zilitoa ushauri na tahadhari juu ya kuzingatia kanuni za uchaguzi na adhabu kwa watakaokiuka. Mgawanyiko wa meseji hizo uko kama ifuatavyo:
Kashfa/kejeli dhidi ya Lowassa 85
Kumuunga mkono Lowassa 58
Kejeli dhidi ya CCM 44
Kutambiana/majigambo 39
Kumuunga mkono Magufuli 37
Kejeli dhidi ya Kingunge 34
Kupashana habari za uchaguzi 33
Kuelimishana juu ya uchaguzi 32
Kashfa/ kejeli kwa Chadema 29
Kejeli dhidi ya Magufuli 27
Kejeli dhidi ya Sumaye 25
Kupeana ushauri, maonyo 8
Utafiti huo unaonyesha kuwa, wanasiasa walioongoza kwa kutupiwa kejeli na kashfa ni mgombea wa chama cha upinzani cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) anayeungwa mkono na umoja wa katiba ya wananchi Tanzania (UKAWA), Bw. Edward Lowassa. Kwa mujibu wa utafiti huo, meseji za kumkejeli Lowassa zilizotumwa kwa siku hiyo zilikuwa ni 85.
Meseji za kejeli dhidi ya Lowassa nyingi zilizungumzia afya yake huku baadhi ya watumaji wakienda mbali kwa kudai kuwa hana sifa ya kuongoza nchi kutokana na matatizo ya kiafya aliyonayo. Meseji hizo zilidai kuwa mgombea huyo alikuwa anashindwa kuongea wakati wa mikutano ya kampeni wakati mwingine akiishia kuzungumza kwa dakika chache na kuwaacha wafuasi wake na kiu.
Sambamba na suala la afya, meseji dhidi ya Lowassa zilimhusisha na ufisadi anaodaiwa kutenda wakati akiwa kiongozi katika nafasi mbambali Serikalini zikiwemo za uwaziri na uwaziri mkuu, nafasi aliyoachia baada ya kuhusishwa na kashfa ya Richmond.
Licha ya meseji za kejeli, utafiti unaonyesha kuwa, wapo Watanzania wengi waliokuwa wakimuunga mkono Bw. Lowassa. Kwa mfano, kati ya meseji zilizotumwa siku hiyo, 58 zilimuunga mkono Bw. Lowassa, idadi ambayo ni kubwa ikilinganishwa na ile ya waliokuwa wakimuunga mkono mpinzani wake wa karibu, Dk. John Pombe Magufuli ambaye meseji za kumuunga mkono ni 37.
Walalahoi walimpaisha Lowassa
Baadhi ya watumaji wa meseji walimuona Bw. Lowassa kama kiongozi pekee anayeweza kuleta mabadiliko ya kweli nchini Tanzania wakati wengine walisema mvuto wake ulitokana na kujiweka karibu na makundi ya watu wenye kipato cha chini kama akinamama wanaouza chakula maarufu kama mamalishe, waendesha pikipiki maarufu kama bodaboda pamoja na wafanya biashara wadogo wadogo wanaojulikana kama Machinga.
Jumla ya meseji 44 zilikejeli Chama cha Mapinduzi (CCM) kwa madai mbalimbali yakiwemo ya viongozi wake kuhusishwa na ufisadi, ubadhirifu na matumizi mabaya ya fedha za umma, upitishaji wa mikataba mibovu ya uwekezaji pamoja na mgawanyo mbovu wa raslimali za taifa ambao umepelekea watu wachache kunufaika wakati wengi wanazidi kuishi kwenye umaskini wa hali ya juu.
Hata hivyo meseji 39 zilihusu majigambo miongoni mwa wafuasi na mashabiki vya vyama tofauti huku kila mmoja akinadi mgombea wake kuwa ndiye anayefaa kuchukua dola.
Kwa mujibu wa utafiti huo, meseji zilizomuunga mkono mgombea wa Chama cha Mapinduzi, (CCM), chama ambacho kimekuwa madarakani tangu Tanzania ilipopata uhuru, ni 37 wakati zile zilizomkejeli ni 27 tu, ukilinganisha na mpinzani wake mkubwa, Bw. Lowassa ambaye meseji za kumkejeli zilikuwa 85 wakati zilizomuunga mkono zilikuwa 58.
Kingunge, Sumaye nao walichafuliwa
Wanasiasa wengine ambao walirushiwa meseji za kashfa ni Kingunge Ngombale Mwiru, ambaye meseji zilizomhusu ni 34 na zote zilijaa kashfa na kejeli. Waziri Mkuu wa awamu ya tatu, Bw. Frederick Sumaye, meseji zilizomhusu ni 25 na zote zilikuwa ni za kumchafua wakati hakuna hata moja ilikuwa ya kumuunga mkono. Kingunge, ni mwanasiasa mkongwe aliyekuwa mshauri wa chama tawala kwa miaka mingi lakini alijiengua na kuingia upinzani baada ya mchakato wa kuteua mgombea urais wa CCM uliomtupa nje Bw. Lowassa. Bw. Sumaye alikuwa miongoni mwa makada wa CCM waliochukua fomu kuwania nafasi ya urais lakini na yeye alitoswa. Baadaye aliamua kuhamia upinzani huku akilaumu utaratibu uliotumika kumpata mgombea.
Meseji nyingine 33 zilizotumwa, watumaji walipashana habari mbalimbali juu ya masuala ya uchaguzi kama namna ya kupiga kura, umbali wa kukaa baada ya upigaji kura, wakati meseji 32, watumaji walielishana juu ya masuala kadhaa ya uchaguzi. Meseji nane, watumaji walipeana tahadhari kuhusu kanuni za uchaguzi.
Uchaguzi mkuu wa rais, wabunge na madiwani ulifanyika nchini kote Oktoba 25 mwaka huu. Zaidi ya Watanzania milioni 22 walijiandikisha kupiga kura na vyama vinane vilisimamisha wagombea wa nafasi ya urais.
Bw. John Magufuli wa CCM aliibuka kidedea kwenye uchaguzi huo kwa kupata asilimia 58 wakati mpinzani wake wa karibu, Bw. Lowassa alipata asilimia 39 ya kura zote zilizopigwa.
Recent Comments