Arusha. Wakati Mbunge wa Arusha Mjini (Chadema), Godbless Lema akisema haogopi kusema ukweli, Mkuu wa mkoa huo, Mrisho Gambo amemtahadharisha kuwa hataacha kumchukulia hatua iwapo atamtukana Rais John Magufuli na Serikali yake.
Lema ambaye ameanza kufanya mikutano ya hadhara katika jimbo lake jana kwenye Soko Kuu la Arusha mjini alisema haogopi kusema ukweli hata kama akipingwa na baba yake mzazi.
âTaifa lipo kwenye mgawanyiko mkubwa, wakuu wa wilaya na mikoa wanafanya maamuzi kwa maelekezo kutoka ngazi za juu,â alisema.
Aliongeza kuwa hali ya demokrasia nchini ni mbaya kwa kuwa hakuna usawa na kuwataka viongozi kuomba hekima wanapopata mamlaka ya uongozi.
Kadhalika amezungumzia hatua ya kujiuzulu kwa Diwani wa Muriet, Credo Kifukwe akisema kuwa Chadema haihitaji jeshi la watu wengi bali la wachache wenye umoja. âNimeteswa sana katika mji wa Arusha, lakini nawataka wafuasi wa Chadema msilipize kisasi kwa wanaohama chama. Leo wapinzani hawaruhusiwi kufanya siasa, lakini Rais anazunguka nchi nzima,â alisema.
Mbunge huyo alisema Tanzania inahitaji demokrasia ya kweli na amani ya nchi haiwezi kutunzwa na polisi isipokuwa kwa upendo wa Watanzania.
Pia, alimtaka Gambo kujipanga wakati wa uchaguzi mdogo wa madiwani kwa kuwa Chadema imejipanga kikamilifu. Katika mkutano huo, Lema aliwapandisha jukwaani madiwani wawili wa Chadema jijini Arusha, Obeid Mengâroriki wa Kata ya Terat na Ruben Ngowi wa Kimandolu huku akisema amesikia wanataka kujiuzulu nyadhifa zao.
Hata hivyo, madiwani hao waliposimama walisema wao hawana bei ya kuweza kununuliwa na mtu yeyote.
Wakati Lema akiyasema hayo, Gambo alisema Serikali ya Awamu ya Tano imejipambanua katika utendaji wake, hivyo mwanasiasa yeyote hataruhusiwa kutoa matamshi yenye kumdhihaki Rais na Serikali.
Akizungumza katika mkutano na viongozi wa madhehebu ya dini uliofanyika jana kwenye ukumbi wa mikutano wa AICC alisema: âTumempa mbunge wa jimbo hili (Arusha Mjini) kibali cha kufanya mikutano na wananchi wake kwa sababu ni kiongozi aliyechaguliwa na wananchi, hatuna sababu ya kumzuia, ila hatutakubali kusikia kwenye mikutano yake akimtukana Rais wetu na Serikali yake. Akifanya hivyo tutamshughulikia.â
âMtu yeyote anayetaka kuichezea Serikali na kutaka kukwamisha ajenda zake tutawangâoa iwe kwa greda au kwa namna nyingine yoyote, Rais Magufuli alipita nchi nzima akitoa ahadi zake na wamemchagua sasa wamwache atekeleze alichowaahidi wananchi.â
Gambo alitumia mkutano huo kuzungumzia kadhia ya rambirambi zilizotolewa kufuatia ajali ya wanafunzi wa Lucky Vincent iliyopoteza maisha ya watoto na wafanyakazi wapatao 35 na baadaye Meya wa Jiji la Arusha, Kalist Lazaro na Lema kutilia shaka matumizi yake.
Recent Comments