UKIWAULIZA wanamuziki wanaokwenda kushuti video zao Sauzi kwamba wanavutiwa na nini hasa, majibu yao yanafanana; watakwambia wanatafuta âqualityâ, ambayo hutokana na hali nzuri ya hewa, lokesheni za kuvutia pamoja na kile wanachosema âconnectionsâ, wakimaanisha madairekta wa huko wanawauza kwa media za nje.
Wanaamini hali ya hewa ya Sauzi ni nzuri kuliko Bongo na inatoa video zenye ubora mzuri kuliko akiifanyia hapa nyumbani na imani yao ni kuwa madairekta wa hapa hawawezi kuwatangaza nje ya nchi.
Majibu kama haya nimewahi kuyapata kutoka kwa wasanii wengi, wakiwemo Joh Makini, Nay wa Mitego, Bill Nas, Chegge na wengineo.
Kuhusu hali ya hewa
Ukianza na hali ya hewa, si kweli kwamba Tanzania nzima hakuna sehemu zenye hali ya hewa nzuri kama Sauzi. Kama ni baridi mbona kuna Arusha, Moshi, Mbeya, Iringa. Ni baridi lipi hilo linalohitajika kutoa video kali? Msikariri au kufuata mkumbo, kwamba kwa kuwa msanii fulani kashutia Sauzi, basi na nyie mshutie huko, fanyeni utafiti!
Lokesheni
Hata kuhusu lokesheni, siamini kwamba Bongo hakuna sehemu kali na vivutio kuliko wanavyokimbilia Sauzi. Niseme tu wazi, mbali na kuwa mwandishi âprofessionalâ yangu nyingine ni Tour Guide and Tour Operator (Muongoza Safari na Muandaaji wa Safari za Kitalii).
Nimetembelea maeneo mengi yenye vivutio vizuri sana Tanzania. Na ninathubutu kusema kwa wasanii wa Tanzania, wana uwezo wa kutumia hata mikoa miwili pekee ya Arusha na Kilimanjaro kupata hata zaidi ya kile wanacho-kimbilia bondeni, wakiamua kushirikiana vyema na madairekta wa Bongo.
Kuhusu âconnectionsâ
Mbali na kuwakimbilia madairekta hao wanaoamini wana-connection zaidi wanapaswa kuangalia hali halisi. Binafsi ninaamini kazi nzuri zinajitangaza. Mfano mzuri angalia video ya Wimbo wa Darassa, Muziki, ambayo imeshutiwa hapa Bongo na kijana wa nyumbani Hanscana, halafu angalia video ya Nay wa Mitego iitwayo Saka Hela, iliyoshutiwa Sauz na dairekta wa nje, halafu jiulize ipi kati ya video hizi imefanya vizuri na kufika mbali.
Jibu utaona video ya Darassa ingawa imeshutiwa Bongo, imefika mbali zaidi kuliko hiyo ya Nay iliyoshutiwa na dairekta anayeaminika kuwa na koneksheni zaidi. Hata hivyo, kina Msafiri, GQ, Hanscana, Nick Dizzo, Khalfani na wengine wengi video zao siku hizi zinafika mbali jambo ambalo linaonesha kuwa wana koneksheni nzuri.
Pongezi Bonge la Nyau
Mwanamuziki anayefanya poa kwenye Bongo Fleva, Bonge la Nyau ameachia mitandaoni video ya Wimbo uitwao Homa ya Mapenzi alioufanyia Sharobaro Records na kumshirikisha Barakah The Prince .
Awali, alipanga video ya wimbo huo akaifanyie Sauzi, lakini baada ya kutafakari vizuri akaona hakuna kipya anachoweza kukipata huko zaidi ya gharama, kwani Bongo kuna lokesheni nzuri zaidi.
âNilipofikiria vizuri kuhusu hilo, nikaamua kumshirikisha dairekta Msafiri aliyeniambia mambo mazuri tunaweza kuyapata hapahapa kuliko Sauzi, tena kwa gharama ndogo. Tukaamua kwenda Arusha kwenye Hifadhi ya Taifa ya Ngorongoro na kushuti video kali, ambako hata baadhi ya gharama tulipunguziwa,â anasema Bonge la Nyau.
Bonge la Nyau anasema alitumia kiasi cha shilingi milioni kumi, ambacho ni gharama za dairekta, lokesheni, malazi ya timu yake, usafiri na mambo mengine, tofauti na gharama alizotumia Nay wa Mitego katika wimbo wake wa Saka Hela ambao alitumia shilingi milioni 60.
Lakini mbali na yote, Bonge la Nyau ametangaza na kuvitumia vyema vivutio vyetu vya utalii. Amethibitisha kuwa Bongo kuna lokesheni na hali ya hewa nzuri kuliko hata Sauzi. Pia amechangia katika pato la taifa kwa gharama alizotumia Ngorongoro.
Pongezi kwake na dairekta Msafiri, ikiwa wasanii wote wakifanya kama wao si ajabu siku zijazo wasanii kutoka nje wakaja Bongo kushuti video zao, kama alivyofanya French Montana kutoka Marekani kwenda kushuti video Uganda, kwa kuwa wasanii wa nchi hiyo wanavitumia vyema vivutio walivyonavyo kuvitangaza.
Recent Comments