Recent Comments

Jeshi la Polisi Mkoani Mbeya lawamani kwa mauaji

Na Steven Samwel – Mbeya.

Jeshi la Polisi mkoani Mbeya, linatuhumiwa kuhusika na mauaji ya kijana muuza machungwa katika Soko la Sido ambaye ni Mkazi wa Mtaa wa Iyela II, jijini Mbeya, anayesadikiwa kufariki katika mazingira ya kutatanisha.

Kifo cha kijana huyo aliyefahamika kwa jina la Allen Mapunda mwenye umri wa miaka 20, kimetokea wakati ndugu wa marehemu wakiwa katika Hospitali ya Rufaa Kanda ya Mbeya.

Imeelezwa kuwa kabla ya umauti, marehemu alikamatwa Machi

24 mwaka huu majira ya saa nne usiku katika eneo la kucheza pull lililopo Mtaa wa Maendeleo, na kumpeleka hadi kituo kikuu cha Polisi ambapo alikaa kwa siku moja na kesho yake alidhaminiwa na ndugu ambao waliamua kumpeleka hospitali kwa ajili ya matibabu kutokana na kuwa na majeraha inayodhaniwa kuwa ni ya kipigo.

Kwa mujibu wa mama mlezi ajulikanaye kama Alice Mapunda, amesema marehemu alionekana na majereha mkononi na kichwani ambako alikuwa akivuja damu huku akilalamikia kupata maumivu.

Kufuatia kifo hicho, baadhi ya vijana wa Iyela waliamua kuandamana kupinga tukio hilo wakidai kuwa linahusishwa na Polisi hivyo walianza kuwatafuta polisi wanaoishi eneo la Kata hiyo na viongozi wa Mtaa kwa nia ya kulipa kisasi.

Miongoni mwa viongozi walikumbwa na kadhia hiyo ni Mwenyekiti wa Iyela II, Boaz Kyejo ambaye dirisha la nyumba yake lilivunjwa na vijana hao wakimtuhumu kuhusika kuwaita Polisi kwa ajili ya kufanya doria ya kuwamata vijana wa Kata hiyo hivyo na hatimaye kuhusikana na kifo cha Marehemu.

Kwa upande wake, mama Mdogo wa Marehemu Bi. Justina Kilasa alisema kuwa marehemu hakuwa na tabia mbaya hivyo kitendo cha kukamatwa kwa madai ya kuhusikana na uhalifu sio cha kweli, kutokana na marehemu kuwa na tabia njema.

Akizungumzia tukio hilo Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Mohammed Mpinga, amesema uchunguzi juu ya kifo hicho unaendelea na kwamba taarifa rasmi ataitoa mara baada ya uchunguzi kukamilika.