Na Steven Samwel – Dar es Salaam.
Imeelezwa kuwa Tanzania ndiyo nchi inayoongoza kwa fursa kubwa za maendeleo ya kiuchumi na biashara kuliko nchi nyingine za Afrika Mashariki, na kutolea mfano wa sekta moja tu ya usafiri na usafirishaji ambayo inaweza kuwa na mchango mkubwa kiuchumi.
Tanzania imezungukwa na nchi 8 ambazo hazina bahari, hivyo fursa ya usafirishaji kwa kutumia bandari, reli, maziwa na anga, zikitumiwa vizuri, zinaweza kuipaisha Tanzania kiuchumi na kujiendesha, bila kutegemea sekta nyingine zozote.
Mkurugenzi Mkazi wa Taasisi ya TradeMark East Africa, Ofisi ya Tanzania, Bw. John Ulanga, amesema hayo wakati wa hafla ya utiaji saini mkataba wa ufadhili wa Dola za Marekani Milioni 1.3, ambazo ni karibu Shilingi Bilini 3 za Kitanzania, kwa Taasisi ya Central Corridor Transport Facilitation Agency, inayoshughulikia mizigo inayopitia Bandari ya Dar es Salaam, kuelekea nchi za Uganda, Rwanda, Burundi na Jamhuri ya Demokrasia ya Kongo, kwa kutumia njia ya Ukanda wa Kati.
Kwa upande wake, Katibu Mtendaji wa Central Corridor, Capt. Diodonne Dukundane, ameishukuru TradeMark kwa ufadhili huo na kueleza fedha hizo zitasaidia sana katika kutimiza majukumu ya CCTTFA ikiwemo uhamasishaji wa matumizi ya Bandari ya Dar es Salaam kwa kuelezea faida za Bandari ya Dar es Salaam ukilinganisha na bandari nyingine.
Nae Naibu Mkurugenzi wa TradeMark East Africa Tawi la Tanzania, Bi. Monica Hangi, anaeleza umuhimu wa msaada huu kwa Tanzania na nchi majirani za Tanzania.
Kama sekta ya usafiri na usafirishaji tuu inaweza kuendesha nchi na kuleta maendeleo makubwa, tukijumlisha na sekta nyingine zote, ikiwemo gesi, Tanzania ya viwanda, kilimo, ufugaji na uvuvi, ni kweli Tanzania inaelekea kuwa ni nchi ya uchumi wa Kati, kama kila mtu atajituma na kufanya kazi kwa bidii.
Recent Comments