Na Asifiwe George, Dar es Salaam
ASKOFU wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Josephat Gwajima, amesema tabia ya baadhi ya watu kumuita majina mengi ikiwa ni pamoja na âmshengaâ, ni kielelezo dhairi kuwa sasa ni wakati wa mabadiliko na kwamba bila mshenga ndoa haiwezi kuwapo.
Askofu Gwajima aliyasema hayo jana kwenye Ibada iliyofanyika kwenye kanisa la Ufufuo na uzima lililopo Ubungo.
Matamshi hayo ameyatoa ikiwa imepita takribani wiki moja tangu aliyekuwa Katibu Mkuu wa Chadema, Dk. Wilbrod Slaa aseme kwamba kiongozi huyo wa dini ndiye mshenga aliyemkutanisha Mgombea Urais wa Ukawa, Edward Lowassa na yeye.
âLakini niwaeleze kuwa hakuna mtu ambaye ananiweza mimi Gwajima ndiyo mana hivi sasa wanahaha kwa kuniita majina mengi; mara Mshenga, mara nani⦠lakini ieleweke kuwa hii ni saa yetu ya mabadiliko ambayo Mungu anataka kutupatia taarifa.
â Wakati nakuja kanisani nilipofika hapa maeneo ya Ubungo kwenye stendi za daladala watu waliibuka na kuanza kupiga kelele wakiniita mshenga⦠mshengaâ¦.
âSasa hii ni ishara tosha, maana ndoa bila mshenga haiwezi kuwa ndoa na mshenga ndiye mwenye jukumu la kuunganisha kuwa kitu kimoja, na ikitokea kuna ugomvi anao uwezo wa kusuluhisha na kuweka mambo sawa,â alisema Gwajima.
Awali akianza mahubiri yake, Askofu Gwajima alisema anatambua kanisani hapo walikuwapo waandishi wa habari waliokuwa wanaosubiri atoe kauli ya kumjibu Dk Slaa, lakini hatofanya hivyo kwa kuwa kanisa ni sehemu ya kuhubiri Neno la Mungu na siyo uwanja wa siasa.
Kwa sababu hiyo alisema atazungumza kila kitu kesho kwenye Hoteli ya Landmark mkutano ambao utarushwa moja kwa moja na televisheni.
âNajua hapa kuna waandishi wa habari wamekuja, wanataka kujua jinsi nilivyokuwa mshenga, lakini kanisa langu siyo sehemu ya majibizano, nitafanya mkutano Jumamne kwa saa moja.
âMuda huo unatosha kabisa kufafanua jinsi nilivyokuwa mshenga na matangazo hayo yatarushwa moja kwa moja katika televisheni zote kuanzia saa 7:00 mchana hadi saa 8:00, hivyo msiwe na wasiwasi.
Alisema katika maisha yake hajawahi kuona mchungaji akiongoza nchi bali anachotambua kazi yake ni kuhubiri injili na kuwapatia waumini mafundisho mema.
Askofu Gwajima alisema mwanzoni mwa Januari mwaka huu kanisa hilo lilifunga siku 30 kwa ajili ya kutafuta kiongozi wa kuongoza nchi hivyo kiongozi atakayeapishwa mwaka huu atakuwa nao kwa sababu kanisa lilifunga na kuomba kwa ajili yake.
Alisema baadhi ya viongozi kusimama mbele ya vyombo vya habari na kusema kuna mgombea urais ambaye ameletwa na Gwajima ni ishara nzuri.
â Hivi mlishawahi kuona mtu anasimama kabisa kwenye vyombo vya habari na kusema mambo haya, ukiona dalili kama hizi ujue ndiyo tayari wamesha kwisha,â alisema.
Alisema wakati wa uongozi wa Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere, wahubiri wakubwa wa Injili walikuwa ni Askofu Imanuel Lazaro na Dk. Moses Kulola.
âMmoja alikuwa wa Tanzania Bara na mwingine Zanzibar, walikuwa wakihubiri injili , Nyerere baada ya kuona watu wanahamasika sana na mahubiri yao na kumiminika kwenye mikutano yao, alisema huenda wangeleta mapinduzi ya siasa hivyo aliona ni bora kuwasambaratisha.
âPamoja na kuwasambaratisha lakini kila mmoja alikwenda kuhubiri anapopajua na watu waliendelea kuhamasika, sasa wakati huu ni wa Gwajima kuwa mshenga, ukiona muumbaji ameonekana ujue lazima waliopo watapotea, hii ni saa ya ufufuo na uzima.
âNamuona Roho Mtakatifu awatembelee Lowassa (Edward Lowassa, Mgombea Urais wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) na Magufuli (John Magufuli Mgombea urais wa (CCM), na atakayeshindwa akae pembeni lakini kanisa la ufufuo na uzima litabaki palepeleâ.
âKwa sasa kila mtu apeleke bidhaa zake sokoni na kuzinadi kwa kuwa walaji wapo, walaji hao waamue wenyewe kuchagua bidhaa itakayomfaa kwa lengo la kupata kiongozi atakayeweza kusimamia misingi yote ya dini bila ubaguzi wowote. Muisilamu ahubiri kwa dini yake, Mkristo naye ahubiri kwa dini yake lakini siyo kiongozi mbaguzi,â alisema.
Baada ya kutoa kauli hiyo aliendelea na mahubiri na katikati yake akasema, âlakini niwaeleze kitu, si mnakumbuka yule mtoto aliyekuja kupiga magoti hapa mbele ya madhabahu ya kanisa hili Januari mosi mwaka huu, sasa yule ni msaliti,â alisema na kanisa likashangalia huku waumini wakipiga kelele za âsema babaaaaaâ, â msaliti mkubwa huyooâ .
Katika kanisa hilo waumini walionekana kuvaa nguo na vitambulisho vilivyokuwa na picha ya Mgombea Urais wa Ukawa, Edward Lowassa, huku vingine vikiuzwa katika kanisa hilo.
Recent Comments