Recent Comments

BEI YA PARACHICHI YAPOROMOKA NGARA

By Mwafrika Dec 15, 2023

NA, ANKO G

Bei ya zao la Parachichi Wilayani Ngara mkoani Kagera yazidi kuporomoka kufikia kati ya Tsh 30,000 na Tsh 40,000 kwa Parachichi za kisasa (Kubwa) kutoka Tsh 75,000 bei iliyotumika mwezi Oktoba 2023.

Vilevile Parachichi za kianyeji zimeporomoka kufikia Tsh 17,000 kutoka Tsh 25,000 bei iliyo tumika mwezi Oktoba 2023.

Hatahivyo simamia.com imemtafuta Katibu wa chama cha wakulima wa Parachichi wilayani Ngara Bw. Godfrey Nyange ambae ameieleza simamia.com kuwa bei hiyo imeporomoka kutokana na zao hilo kuongezeka kwa wingi pamoja na uingizwaji wa parachichi nyingi kutokea nchi jirani ya Burundi.

Lakini pia Nyange ameieleza simamia.com kuwa sababu nyingine ni serikali ya wilaya ya Ngara kutoweka utaratibu wa bei elekezi kwa mkulima jambo linalopelekea madalali kuwakandamiza wakulima.

Pia simamia.com imemtafuta mkulima wa zao la Parachichi na mkazi wa Kijiji cha Ibuga Kata ya Kabanga Bw.Joseph Balindiye ambae ameieleza simamia.com kuwa tatizo la kuporomoka kwa bei linatokana na serikali kuweka msisitizo kwa wakulima kulima zao hilo kwa wingi lakini ikiwa haijaandaa masoko ya uhakika ya zao hilo.

Balindiye ameongeza kwa kusema kuwa uingizwaji wa parachichi zinazo toka nchi jirani ya Burundi zinaingizwa Kwa wingi na kuuzwa bei ndogo ambapo wafanya biashara hukimbilia parachichi hizo kwa unafuu wa bei huku wakiziacha zinazo zalishwa wilayani Ngara.

Balindiye amemalizia kwa kuiambia simamia.com kuwa kuna haja ya serikali kuweka usinamizi mzuri katika zao hilo kwa kutafuta masoko ya uhakika na kuweka bei elekezi laasivyo wakulima watang’oa zao hilo kama walivyo wahi kufanya kwa zao la Kahawa kutokana na hasara wanayo ipata kwasasa.

Bila serikali kutafuta suruhu kinacho endelea kwasasa itapelekea wakulima wa zao hilo kuwa masikini kwani serikali inapata ushauru wake huku wakulima wakipata hasara na kuzidi kuwa masikini.