Recent Comments

CHADEMA: HATUWEZI KUWA WATULIVU TENA KWA POLISI KUTUZUGA WANAFANYA UCHUNGUZI –

By ObyMack David Jun 10, 2020
    CHADEMA kupitia kwa Makamu Mwenyekiti wake (Bara), Tundu Lissu imetoa tamko baada ya Mwenyekiti wa Chama hicho ambaye pia ni Kiongozi wa Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe kuvamiwa na watu wasiojulikana na kujeruhiwa

    Lissu amesema “Shambulio hili ni mfululizo wa mashambulio dhidi ya Viongozi na Wanachama wa CHADEMA ambayo yamekithiri katika Utawala wa Rais Magufuli. Ni la pili dhidi ya Kiongozi wa Juu wa CHADEMA kufanywa katika mazingira yanayofanana”

    Amekumbushia tukio la yeye kushambuliwa kwa risasi nyingi katika eneo hilo la ‘Area D’ ambapo Mbowe naye ameshambuliwa nje ya makazi yake ndani ya eneo la makazi ya Serikali, eneo lenye ulinzi mkubwa ila kama ilivyokuwa kwa wakati wake, na sasa Walinzi wote waliondolewa

    Amesema japo Vyombo vya Usalama vimewataka kuwa watulivu hawawezi kwani imekuwa ni utamaduni kwa Tanzania ya Magufuli kuwafanyia vitendo vya kihalifu halafu kuwazuga na kuwatuliza kwa ahadi ya kufanya uchunguzi.

    Amesema “Kauli za kuwadharau na kuwakejeli waliofanyiwa uhalifu kwa lengo la kuhamisha mjadala zimeanza tena. Tunawasikia viongozi wa Serikali na wapambe wao kuwa Mbowe hakushambuliwa bali alianguka mwenyewe na alikuwa amelewa. Mara wanahoji alikuwa wapi usiku wa manane hadi ashambuliwe na wengine wanahoji kwanini alikuwa mwenyewe bila mlinzi binafsi”

    Amesisitiza kuwa kunywa pombe na kulewa sio kosa kwa Sheria za Tanzania na wala haihalalishi mashambulizi dhidi ya yeyote na hakuna tangazo la hali ya hatari linalokataza mtu kutembea usiku hivyo kauli hizo ni za kufifisha uzito wa jambo na kuhalalisha Polisi kutofanya upelelezi

    #Siasa