Na Emmanuel Lengwa, Mbeya
WANANCHI wa kijiji cha Ikombe kilichopo pembezoni mwa Ziwa Nyasa kata ya Matema, Wilayani Kyela, wanakabiliwa na adha kubwa ya usafiri kutokana na kutokuwepo kwa barabara ya aina yoyote inayoingia wala kutoka kijijini hapo.
Ili waweze kusafiri wananchi hao wanalazimika kutumia mitumbwi ya kienyeji kwenda maeneo mbalimbali ikiwemo makao makuu ya kata, Matema na hata makao makuu ya wilaya yaliyoko mjini Kyela.
Wakuzungumza na mwandishi wa habari hii kijijini hapo, wananchi hao wanasema hupata shida zaidi kusafirisha wagonjwa kwenda kwenye kituo cha afya kwa ajili ya matibabu kwa kutumia mitumbwi hiyo ya asili.
Bw. Imeatus Mwambeleko, ambaye ni mkazi wa eneo hilo anasema kuwa, wananchi wanaoumia zaidi ni wanawake wajawazito ambao nao hulazimika kutumia usafiri huo wa mitumbwi ya asili kwenda kujifungua katika kituo cha afya Matema.
âHapa hatuna usafiri mbadala zaidi ya hii mitumbwi, wakati ziwa linapochafuka kwa kuwa na mawimbi makali, akina mama wajawazito wanaohitaji kujifungua, huwa hatarini zaidi na baadhi yao walishakufa kwa kukosa usafiri wa kwenda hospitalini,â anasema Bw. Mwambeleko.
Anafafanua kuwa hata kama ziwa liko kwenye hali ya utulivu, bado kuna tatizo la vyombo vya usafiri kuwa duni, na hivyo kutumia muda mrefu kufika hospitalini.
Kama mgonjwa atabahatika kusafiri na boti za abiria zinazofika kijijini hapo mara chache, anaweza kutumia muda wa dakika 45 hadi Matema, lakini kama usafiri utakaotumika utakuwa ni mitumbwi ya asili, hutumia muda mrefu zaidi wa takribani saa mbili hadi tatu, anafafanua Bw. Mwambeleko.
Mkazi mwingine wa kijijini hapo, Bw. Issa Solomon anasema kuwa kadhia ya usafiri imekuwa ya muda mrefu kutokana na viongozi wao kutobuni au kuwa na mipango ya kuwatatulia tatizo hilo.
Anasema kuwa ingawa kijiji hicho kimezungukwa na safu za milima ya Livingstone pande zote isipokuwa upande wanaopakana na Ziwa Nyasa, bado kuna uwezekano wa kupenyeza barabara hadi kijijini hapo kama Serikali itakuwa na nia ya dhati ya kuwasaidia.
âUpo uwezekano wa kupitisha barabara kutoka Matema mpaka hapa kijijini, lakini ukweli ni kwamba barabara hiyo itakuwa na mzunguko mrefu kidogo, lakini kama wana nia ya kutusaidia ni afadhali ikawepo kwa ajili ya matumizi ya dharura kuliko hali ilivyo hivi sasa, ambapo baadhi ya watu wanakufa kwa kukosa usafiri kwenda kufuata huduma hospitalini,â anasema Bw. Solomon.
Akizungumza na wananchi hao kwenye mkutano wa kampeni uliofanyika kijijini hapo, mwenyekiti wa chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Wilaya ya Kyela, Bw. Saadat Mwambungu amewataka wananchi hao kutumia kura yao kwa kuwachagua viongozi wa upinzani ili wakasimamie suala hilo.
Alisema kuwa Jimbo la Kyela halijawahi kuongozwa na chama cha upinzani, hali ambayo inasababisha chama cha Mapinduzi (CCM) kubweteka na kutosikiliza na kuyafanyia kazi matatizo ya msingi ya wananchi kwa muda wote waliokaa madarakani.
âKama mnataka matatizo yenu yapate ufumbuzi, umefika wakati wa kuionyesha Serikali ya CCM kuwa mmechoka kuivumilia, chagueni viongozi kutoka vyama vya upinzani watawasaidia kushughulikia matatizo yenu,â alisema Mwambungu.
Kwa upande wake mgombea ubunge katika jimbo la Kyela kupitia Chadema, Bw. Abraham Mwanyamaki, alisema akipewa ridhaa ya kuliongoza jimbo hilo atahakikisha katika siku zake 100 za mwanzo kukaa madarakani, ananunua boti ya kisasa kwa ajili ya kusaidia kutoa huduma ya usafiri katika kijiji hicho ikiwa ni hatua ya awali ya kushughulikia tatizo sugu la wananchi hao.
Alisema baada ya kununua boti hiyo kama ufumbuzi wa muda mfupi, sasa ataanza kujenga hoja ili Serikali iliitenge bajeti ya kujenga barabara kuelekea kijijini hapo.
âMkituchagua viongozi wa upinzani, tutahakikisha tuyashughulikia matatizo yenu kikamilifu, tunahitaji kurejesha heshma ya akina mama ambao wamekuwa wakidhalilika na hata kupoteza maisha wakati wa kujifungua, lakini pia kulinda uhai wa kila mwananchi wa eneo hili awe na uwezo wa kupata huduma za afya kwa wakati,â alisema Bw. Mwanyamaki.
Recent Comments