Kigoma. Teknolojia ya matumizi ya mfumo wa Tehama katika mahakama umeelezwa kurahisisha usajili wa mashauri ambapo kwa kipindi cha mwaka 2021 mahakama imefanikiwa kusajili mashauri kwa asilimia 72 kupitia mfumo huo wa mtandao na kupunguza changamoto kwa wananchi wa mkoa wa Kigoma kusafiri umbali mrefu kufuata huduma za mahakama.
Naibu msajili wa mahakama kuu kanda ya Kigoma Arnold Kirekiano  alieeleza hayo jana wakati wa kikao cha pili cha baraza la watumishi wa mahakama kanda ya Kigoma ambapo amesema kwa sasa mfumo huo umekuwa na manufaa makubwa katika utendeji kazi wa mahakama.
âKulingana na Jiografia ya mji wa Kigoma maeneo mengine ni vigumu kufikika hivyo wakazi wa maeneo hayo wanapata fursa ya kutumia simu zao kujua taarifa zinazoendelea ikiwemo kujua siku ya kusikiliza shauri na ratiba nzima ya usikilizaji wa mashauriâ alisema
Kirekiano ametoa wito kwa wananchi kutumia huduma hiyo kurahisisha upatikanaji wa taarifa kwa wakati na kupunguza gharama lakini pia mahakama itatumia huduma hiyo kufanya mawasiliano ya wananchi kuendesha kesi zao kupitia simu za mkononi.
Katika kudhibiti utendaji na uwajibikaji mahakama kuu kanda ya Kigoma imekuwa ikisimamia nidhamu ya watendaji ambapo watumishi ambao wamekuwa wakikiuka utaratibu wa sheria na kanuni za kiutumishi ikiwemo kujihusisha na vitendo vya rushwa  na kuichafua idara ya mahakama wamekuwa wakichukuliwa hatua
Moses Mashaka ambaye ni mtendaji wa mahakama kuu kanda ya Kigoma amesema mahakama inaendelea na jitihada za kuhakikisha kunakuwa na nidhamu kwa watumishi ambao wanatakiwa kuwajibika kuwahudumia wananchi ili kupata haki zao za kimsingi kwa wakati muafaka.
Baadhi ya wakazi wa mkoa wa Kigoma James Minani na Samwel Maenad wameipongeza mahakama kwa kuanzisha mfumo wa huo na kuomba serikali kuimarisha mifumo ya mawasiliano ya hasa maeneo ya vijijini ili kuwasaidia wananchi kunufaika na mfumo huo
Recent Comments