NA FLORENCE SANAWA, MTWARA
MGOMBEA urais kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) chini ya mwamvuli wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), Edward Lowassa, amesema kama akichaguliwa kuwa rais, ataunda tume ya kuchunguza na kushughulikia mikataba yote ya gesi.
Akihutubia mamia ya wananchi waliofurika kwenye viwanja vya Mashujaa mkoani Mtwara jana, Lowassa alisema kama wananchi wakimpa ridhaa ya kuongoza Tanzania, atakahakikisha wanapatikana wataalamu kutoka ndani na nje ya nchi watakaoshughulikia masuala ya gesi.
âMimi najua gesi ndiyo kila kitu, nikipata ridhaa, cha kwanza nitahakikisha wataalamu wakubwa na wadogo wanahakikisha nchi inanufaika.
âNachukia umasikini, ndiyo maana nitasimamia mikataba ya gesi ili vijana, wanawake wapate ajira ili kuondokana na umasikini katika nchi yetu,â alisema Lowassa.
Naye Waziri Mkuu mstaafu, Fredrick Sumaye, alisema Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimeshindwa kuwaletea maendeleo wananchi, na kuwataka waiondoe madarakani kwa kumpa ridhaa Lowassa aongeze nchi.
Alisema CCM haina sababu ya kuendelea kuwa madarakani, kwa sababu imepewa ridhaa muda mrefu bila kumaliza kero za wananchi.
Sumaye alisema CCM imeshindwa kabisa kumaliza tatizo la rushwa na ufisadi, hivyo kuendelea kuwapa nafasi tena ni kuwalaghai wananchi ambao wameshachoshwa kuongozwa na chama hicho.
âCCM wameshindwa, walisema wakiingia madarakani wanawake na watoto watapata huduma za afya bure, lakini mpaka sasa hakuna kilichofanyika.
âUkiangalia shule zetu zina hali mbaya, miundombinu mibovu, hatuoni sababu ya kuendelea kuwapa madaraka tena,â alisema Sumaye.
Katika hatua nyingine, Sumaye alimtaka mgombea urais wa CCM, Dk. John Magufuli, kuacha kutumia falsafa ya M4C kwa vile ni mali halali ya Chadema.
âKama anapenda kutumia neno hili, aje ajiunge Chadema ili aweze kulitumia kwa uhuru zaidi,â alisema Sumaye.
Kabla kuanza mkutano huo, eneo la Bima Sokoni lilionekana kujaa umati mkubwa wa wananchi ambao walikuwa wamebeba mabango ya Lowassa.
Kutokana na hali hiyo, shughuli nyingi za kijamii zilisimama huku maduka mengi yakifungwa.
Lowassa na msafara wake waliwasili eneo la mkutano saa 10:42, lakini ghafla umeme ulikatika hadi saa 11:30 alipopanda jukwaani.
Recent Comments