KATIBU Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF), Maalim Seif Sharif Hamad amemkingia kifua Rais Dk. John Magufuli kwa uamuzi wake wa kumteua Mwenyekiti wa Chama cha ACT-Wazalendo, Anna Mghwira kuwa Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro.
Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Maalim Seif alisema Rais Magufuli hajakosea kwa uteuzi huo kwa kuwa hapangiwi nani amweke wapi na nani asimweke.
âUteuzi ni haki yake, wala hatuingilii maamuzi yake kwa sababu kuteua au kutoteua ni yeye na kuteua ACT na kuacha vyama vingine huenda yeye mwenyewe ana yake moyoni na kwamba hajaamua kufanya hivyo.
âMimi sikuingia katika moyo wake na kwa kufanya hivyo si jambo geni kwa kuwa wapo waliopita waliwapa wapinzani ubunge, lakini pia ni Rais wa kwanza kuingiza mtu wa chama kingine kwenye serikali katika utendajiâ¦si jambo baya kwa maana linaweza jenga upya Serikali,ââ alisema.
Alisema Rais Magufuli ametumia mfumo ambao pia hutumiwa na nchi za Bara la Ulaya na Marekani, ambapo Rais Mstaafu wa Marekani, Barack Obama naye aliutumia.
âSiwezi kushangaa kwani inaweza ikatokea siku akamteua Naibu Katibu Mkuu wangu, Joran Bashange kuwa Waziri wa Nishati na Madini,â alisema Maalim Seif huku waandishi na maofisa wa chama hicho wakiangua kicheko.
UVCCM
Nao Umoja wa  Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM),  umesema hatua ya Rais Dk. Magufuli kumteua Anna Mghwira kuwa Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro ni kitendo cha kijasiri na cha kizalendo kwa sababu  hakuna alipokosea.
Pamoja na hali hiyo, umoja huo umesema uteuzi wa nafasi ya RC Mghwira, ni wazi ataisimamia na kuongoza kwa hekima, busara na uzalendo kwa masilahi ya Taifa.
Kauli hiyo, imetolewa  Dar es Salaam jana na Kaimu Katibu Mkuu wa UVCCM, Shaka Hamdu Shaka.
Alisema uteuzi huo, usiibue nongwa na kuonekana kuna jambo limekosewa.
Pamoja na hali hiyo Shaka, alisema Katiba ya nchi hairuhusu mgombea binafsi na kwamba kila mgombea urais, udiwani au ubunge hutokana na chama cha siasa ila anaposhinda urais huwa na mamlaka ya kuteua mtu yeyote ili mradi awe Mtanzania bila ubia.
Alisema Rais Dk. Magufuli, ana haki na wajibu wa kumteua mtu yeyote atakayeona anafaa kushika nafasi atakayomteua ilimradi aliyeteuliwa awe ana hisia za uchapakazi, mpenda umoja na mzalendo.
Shaka alisema katiba ya CCM imetamka ikiwa kutakuwa na mkuu wa mkoa anayetokana na CCM atashiriki vikao vya Kamati ya Siasa ya Mkoa wakati wa vikao lakini kwa suala la Mghwira lipo tofauti kwani anatokana na chama kingine na ikiwa ataona kuna haja ya kujiunga na CCM basi naye atapata fursa ya kushiriki vikao hivyo.
âIla kwa sasa hasa baada ya kuripoti katika eneo lake la kazi hatoweza kuhudhuria vikao vya Kamati ya Siasa ya Mkoa kwa kuwa si mwana CCM ila kama ataona kuna haja ya kujiunga na CCM hazuiwi na atakuwa na haki ya kuhudhuria vikao vyote.
âKwa hili Rais Dk. Magufuli anabaki kuwa nembo ya demokrasia ya kweli nchini kwetu kwa kushirikisha wapinzani kwenye nafasi nyeti za utendaji.
âViongozi wa Serikali wakiteuliwa hula viapo vya utii ambavyo vimeandikwa kisheria katika medani za uendeshaji Serikali, mteule wa Rais hali kiapo cha kisiasa bali huapa kiapo cha kutumikia nchi na watu wake kwa mujibu wa sheria za nchi na Katiba,â alisema Shaka.
Recent Comments